Maduka matano yateketea kwa moto Tabora

Muktasari:
Moto huo umezuka usiku wa manane na kuteketeza maduka matano yaliyokuwa na bidhaa mbalimbali.
Tabora. Moto mkubwa umezuka usiku wa manane na kuteketeza maduka matano yaliyokuwa na bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo, vifaa vya saluni na chakula, katika eneo la Salmini, Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora.
Shuhuda wa tukio hilo, Saidi Ali, ambaye ni dereva wa bodaboda, amesema kuwa wakati akiendelea na shughuli zake saa nane usiku, alipita katika eneo hilo akiwa na wenzake na waliona moto mkubwa ukiwaka kwenye maduka hayo.
"Sisi tumepita hapa usiku tuko mbio tunawahi abiria ndio tunaona moto mkubwa unawaka hapa sokoni nikakimbilia zimamoto kuwaita, wenzangu wengine wakakimbilia polisi ili tupate na ulinzi kabisa," amesema shuhuda huyo.
Mahasini Ali, shuhuda mwingine wa tukio hilo, amesema walikumbwa na mshangao mkubwa baada ya kuona moto tayari umeenea kwenye eneo la biashara bila kujua ulianzia wapi.
"Mimi nilikimbilia polisi kutoa taarifa, mwenzangu akaenda zimamoto. Tulikuwa na haraka sana kila mmoja akatafuta msaada kwa njia aliyodhani ni ya haraka zaidi, ili kuokoa mali za watu.
“Hali ya maisha ilivyo sasa, mtu anapopata hasara ya aina hii ni maumivu makubwa sana," amesema Mahasini.
Kwa upande wake Kelvin Fanuel, ambaye alikuwa kinyozi katika moja ya fremu zilizoteketea, amesema moto huo umemrudisha nyuma kimaisha kwani biashara hiyo ilikuwa tegemeo lake kuu kwa familia.
"Yaani sijui nianzie wapi, hii biashara ndiyo kila kitu kwangu. Sina shughuli nyingine ya kuingiza kipato. Kwa kweli nahisi kuchanganyikiwa," amesema Kelvin huku machozi yakimtoka.
Ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Meja Hassani Mande amesema moto huo tayari umedhibitiwa na juhudi za uchunguzi zinaendelea ili kubaini chanzo.
"Moto umetekeza fremu tano. Katika eneo hilo kulikuwa na matoroli, masufuria na dalili za uwepo wa majiko ya kupikia. Tutaendelea na uchunguzi. Tunawaomba wananchi kushirikiana kwa karibu na kutoa taarifa mapema pindi majanga ya namna hii yanapotokea," amesema Meja Mande.
Amesema kwa sasa, mamlaka zinaendelea kuchunguza ili kuhakikisha hatua za tahadhari zinawekwa ili kuzuia majanga kama haya siku zijazo.