Moto wateketeza maduka 17, gari la zimamoto laongeza kilio

Muktasari:
- Hili ni tukio la nne la moto kutokea katika eneo la Katoro na Buseresere, maeneo ambayo yana shughuli nyingi za kibiashara zikiwemo za jumla na rejareja.
Geita. Zaidi ya maduka 17 pamoja na stoo za kuhifadhia bidhaa vimeteketea kwa moto usiku wa Juni 10,2025 katika eneo la Buseresere, Wilaya ya Chato mkoani Geita, huku chanzo cha moto huo kikidaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.
Tukio hilo limetokea saa tatu usiku, juhudi za kuuzima moto huo zilichelewa kutokana na kukosekana kwa gari la zimamoto katika eneo hilo lenye shughuli nyingi za kibiashara.
Kwa mujibu wa mashuhuda, gari la kwanza la zimamoto kutoka makao makuu ya Mkoa Geita lilifika eneo la tukio saa tano kasoro usiku, hali iliyochangia moto huo kusambaa na kuharibu mali za mamilioni ya fedha.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buseresere, Kasezero Athuman akizungumza na Mwananchi Digital akiwa eneo la tukio mapema leo Jumatano Juni 11, 2025 amesema moto huo ulianza ndani ya duka ambalo mchana kulikua na shughuli za uchomeleaji geti.

“Baada ya kuona moshi mkubwa tulipiga simu ofisi za zimamoto maana maduka mengi yalikuwa yameshafungwa, wananchi walianza kuuzima lakini ulikua ukisambaa kwa kasi na zimamoto walichelewa kufika, hata hivyo hadi sasa hatuwezi kusema hasara kiasi gani imepatikana lakini ukweli ni kubwa,” amesema Athuman.
Amesema hii ni mara ya nne moto kulipuka katika eneo hilo na kila wakipiga simu Zimamoto huchelewa kufika kuuzima kwa sababu hakuna gari.
“Tunaomba waweke gari eneo hili, hapa ni sehemu kubwa ya biashara maduka ya jumla na rejareja yako mengi, kuna haja ya kuwepo na kituo cha zimamoto au waweke gari moja hapa hata kama ni dogo, itakuwa rahisi kudhibiti matukio haya badala ya kusubiri moto utokee ndio waje wazime tena kutokea Geita mjini,” amelalamika kiongozi huyo.
Mwananchi imezungumza na Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Hamis Dawa ambaye amesema walipata taarifa rasmi saa nne kasoro usiku, wakati moto huo ulianza saa mbili na nusu usiku.
“Umbali kutoka Geita mjini hadi Buseresere ni takriban kilomita 40. Hili pamoja na kuchelewa kwa taarifa kutoka kwa wananchi ndilo lililosababisha ucheleweshaji wa huduma ya kuuzima moto, niwasihi wananchi watoe taarifa mapema maana eneo hili hatuna ofisi ya Zimamoto,” amesema Dawa.
Hata hivyo, amesema askari wa Kikosi cha Zimamoto kwa kushirikiana na gari la zimamoto kutoka Uwanja wa Ndege wa Chato na lingine la mgodi wa GGM walifanikiwa kuudhibiti moto huo saa tisa usiku, baada ya kufanya kazi ya zaidi kwa saa sita.
Kwa sasa, shughuli zinazoendelea ni kuzima moto mdogo uliobaki chini ya vifusi ili kuzuia kusambaa tena.
Hili ni tukio la nne la moto kutokea katika eneo la Katoro na Buseresere, maeneo ambayo yana shughuli nyingi za kibiashara zikiwemo za jumla na rejareja.
Wakizungumzia baadhi ya wafanyabiashara waliopoteza mali zao, wameitaka Serikali kuangalia upya mipango ya usimamizi wa maafa na kuweka gari la zimamoto kwenye kituo cha karibu, hususan katika eneo la Katoro au Buseresere.
Abel Melkiori amesema hasara iliyosababishwa na moto huo ni kubwa kwa sababu duka lake ni la bidhaa mbalimbali za jumla, huku akisema kwa tathimini ya haraka ameunguliwa na mali za Sh25 milioni.
“Moto umeteketeza lakini vibaka pia wameiba mali nyingi sana walikua wanakuja kama wasamaria kuokoa kumbe walikua wanabeba bidhaa na kutokomea, mimi nauza mafuta na vocha na bidhaa nyingine nauza bidhaa mchanganyiko,” amesema Melkiori.
Amesema tukio la moto si la kwanza kutokea eneo hilo, yamewahi kuungua maduka mengine tisa na hakuna juhudi zilizofanyika kuweka gari la zimamoto jirani.
Mfanyabiashara mwingine, Alis Wanjara amesema alifunga duka lake saa tatu usiku na kurudi nyumbani, lakini muda mfupi baadaye alifuatwa na dereva bodaboda akimtaka waondoke wote waende dukani kwake kuna moto.
“Nilitoka mbio hadi dukani, nilipofika kufungua jengo lilikuwa limeshawaka, watu walisaidia kuhamisha vitu lakini baada ya muda mfupi moto ulisambaa eneo lote, duka hili mtaji wake ni Sh30 milioni kati ya hizo, Desemba mwaka jana nilikopa benki Sh15 milioni ambazo niliongezea mtaji lakini mali zote zimeteketea,” amesema Alis kwa uchungu.