Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Moto wateketeza maduka 14 Dodoma

Baadhi ya maduka yaliyoungua na Moto Barabara ya Nane katika Mtaa wa Mwanagaza jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Rehema Menda  amesema tukio hilo limetokea leo, Jumanne Januari 21, 2025  saa 1:26 asubuhi

Dodoma.  Maduka 14 yaliyopo Barabara ya Nane, Mtaa wa Mwangaza, jijini Dodoma, yameteketea kwa moto huku uchakavu wa majengo ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia moto kusambaa.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Rehema Menda  amesema tukio hilo limetokea leo, Jumanne Januari 21, 2025  saa 1:26 asubuhi.

"Tumetumia mbinu mbalimbali kuokoa mali za wafanyabiashara na kama unavyoona, tumeokoa kwa kiasi kikubwa. Hadi sasa, hakuna mtu aliyepata madhara ya moja kwa moja, kama kuungua au athari ya moshi. Hata hivyo, mmiliki mmoja wa maduka, anayeitwa Kimaro, amekimbizwa hospitali kutokana na mshtuko," amesema Rehema.

Amesema athari ya moto imekuwa kubwa kutokana na bidhaa zilizohifadhiwa ndani ya vyumba, zikiwamo pafyumu, mapazia na vifaa vya pikipiki.

Rehema amesema jeshi hilo linaendelea kufanya ukaguzi kwa kuendesha operesheni ya kutambua nyumba chakavu ambazo baadhi zinatumiwa kama maghala kinyume na matumizi yaliyokusudiwa.

Amewataka wananchi kutumia majengo kwa matumizi sahihi ili kuepuka athari za moto. Rehema  amesema kuna vyanzo vya moto vinavyoweza kuchangia matukio kama hayo ikiwamo mlundikano wa muda mrefu wa vitu ambao husababisha upungufu wa hewa, hali inayoweza kuchangia moto kulipuka.

“Uwekaji wa vitu vingi kwa pamoja unasababisha moto kusambaa haraka kwa kuwa vitu hivyo vinatumika kama chakula cha moto,” amesema Rehema.

Mdogo wa mmoja wa wamiliki wa nyumba hiyo yenye  maduka iliyoungua, Julius Malya amesema alipokea taarifa za tukio hilo akiwa nyumbani.

Shuhuda wa tukio hilo, Debora Palanjo amesema asubuhi walipokuwa wakitoka kuchota maji, ghafla walisikia kishindo kikubwa kutoka kwenye moja ya maduka yaliyokuwa yamefunguliwa nusu mlango.

“Tuliona mtu akitoka nje akipiga kelele za moto. Tulipoangalia, tuligundua moto ulikuwa ukizidi kusambaa. Tulijaribu kumwaga maji, lakini haikusaidia. Ndipo tulipopiga simu Jeshi la Zimamoto wakaleta magari kwa ajili ya kuuzima,” amesimulia shuhuda huyo.

Shuhuda mwingine, Muksni Salim ameshauri Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupeleka magari zaidi ya moja pale panapotokea tukio la moto.

“Aina ya changamoto tuliyokumbana nayo hapa inadhihirisha umuhimu wa kuwa na magari zaidi ya moja. Gari la kwanza lilijitahidi kuzima moto, lakini maji yalipokwisha, moto uliendelea kuteketeza nyumba. Kama magari mawili au matatu yangeletwa mara moja, hali isingekuwa mbaya hivi,” amesema.

Hata hivyo, wamiliki wa maduka yaliyounguwa ambao walikuwa wakifarijiwa na ndugu zao, walikataa  kuzungumzia tukio hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ametoa pole kwa waathiriwa wa tukio hilo na kuhimiza wafanyabiashara na wamiliki wa majengo kukata bima za majanga ili kujilinda dhidi ya hasara kubwa.

Pia, amewasihi kuchukua tahadhari zaidi kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazosaidia kubaini na kuzuia moto.

Kuhusu hoja ya kuongeza idadi ya magari ya zimamoto kwenye matukio, Shekimweri amesema upelekaji wa vifaa hutegemea taarifa za awali kutoka eneo husika.

“Mitambo ya zimamoto imewekwa kwenye vituo mbalimbali ili kuhakikisha upatikanaji wake wa haraka unapohitajika. Katika tukio hili, baada ya kupima kiwango cha moto na hali ya shughuli za eneo hilo, waliamua kuleta magari mengine, na hatua hiyo ilichukuliwa mara moja,” amesema mkuu huyo wa wilaya.