Moto wateketeza maduka zaidi ya 20 Mwenge

Baadhi ya maduka yaliyoteketea moto eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Moto uliozuka katika eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam umeteketeza zaidi ya maduka 20 ya bidhaa mbalimbali.
Dar es Salaam. Moto ambao chanzo chake hakijajulikana umeteketeza maduka zaidi ya 20 eneo la Mwenge jijini hapa.
Moto huo umezuka usiku wa kuamkia leo Jumanne Desemba 5, 2023 ikiwa ni miezi miwili tangu moto mwingine ulipotokea katika eneo la Mnadani Kariakoo Oktoba 1, mwaka huu na kuteketeza maduka na vibanda vya wafanyabiashara.
Akizungumzia ajali hiyo, Lucy Mbona ambaye aliyeunguliwa na duka la viatu, amesema hali hiyo imeacha simanzi kwake.
Amesema si bidhaa pekee moto huo umeteketeza hadi fedha alizoziacha dukani hapo.
Amesema ni utaratibu wake kuacha fedha dukani, kwa kuwa asingeweza kutembea nazo wakati wote.
"Jana nilipanga kuzipeleka benki, sijui nini kumetokea nafikiri Mungu alipanga nisizipeleke, hatimaye zimeungua," amesema.
Lucy amesema taarifa kuhusu janga hilo aliipata saa sita usiku na alipofika katika eneo hilo alishuhudia vitu vikiungua na hakukuwa na juhudi zozote za uokoaji.
Serikali lawamani
Licha ya eneo ilipotokea ajali hiyo kuwa karibu na Kituo cha Polisi, Lucy amesema walipoona moto huo waliwasha gari na kuondoka na hawakurejea tena.
Kinachomsikitisha ni kile alichoeleza, gari la kuzima moto lilifika katika eneo la tukio wakati kila kitu kilikuwa kimeshateketea.
"Wamekuja kama ushahidi kwamba wanafanya juhudi, lakini hakukuwa na kitu kilichobaki kila kitu kiliungua na wamekuja hawana maji ya kuzima moto," amesema.

Fedha zikiwa zimeteketea baada ya moto ambao chanzo chake hakijafahamika kuteketeza maduka zaidi ya 20 eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam.
Lucy ameeleza kuwa hakulikatia duka lake bima, hivyo hana tumaini la kurejesha chochote.
Ramadhani Issa aliyeshuhudia ajali hiyo, amesema moto ulivyoanza walifanya jitihada mbalimbali za kuuzima, huku baadhi yao wakiwasiliana na kikosi cha zimamoto na uokoaji.
"Moto ulianza kwenye moja ya fremu, tulishtukia moshi mkubwa lakini baadaye ulianza kusaamabaa kwa kasi kabla ya zimamoto kufika ingawa moto ulikuwa umeteketeza vitu kwa kiasi kikubwa," amesema Issa.