Hujuma chanzo moto Kariakoo

Muktasari:
- Kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, imebaini chanzo cha moto kilichoteketeza maduka na vibanda vya wafanyabiashara Kariakoo ni hujuma na sio ajali.
Dar es Salaam. Ripoti ya chanzo cha moto ulioteketeza vibanda vya biashara eneo la Mnadani Kariakoo Oktoba mosi, mwaka huu imeonyesha chanzo cha moto huo ni hujuma na imependekeza wafanyabiashara wasirejee eneo hilo.
Hata hivyo, wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi walisema wanapinga mapendekezo ya kamati ya wao kuondolewa eneo hilo na kutafutiwa lingine.
Mapendekezo ya kuondolewa kwa wafanyabiashara hao yamo kwenye ripoti ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, iliyokabidhi ripoti yake jana na kiongozi huyo alisema kamati hiyo ilihusisha vyombo vya ulinzi na usalama na hakuwahi kuweka hadharani majina ya wajumbe wake.
Oktoba 2, mwaka huu Chalamila aliwaahidi wafanyabiashara hao kuwa ataunda kamati itakayofanya kazi kwa siku saba kuchunguza tukio la moto huo.
Kamati hiyo iliyokuwa na watu saba ilibaini hujuma miongoni mwa wafanyabiashara zilizosababishwa na mgogoro kati yao na uongozi uliopo ndicho chanzo.
Akieleza kilichomo ndani ya ripoti hiyo jana mbele ya waandishi wa habari, Chalamila alisema uchunguzi umehusisha eneo la tukio na kufanya mahojiano ya kina na mashuhuda, wamiliki wa majengo yanayozunguka eneo hilo, wafanyabiashara, walinzi wa zamu na kupitia picha za kamera zilizorekodiwa kabla na baada ya tukio.
"Maelezo ya waliohojiwa, wakiwamo wafanyabiashara na walinzi wa Mnadani yalionekana kuwa yamepangwa na hayaakisi uhalisia wa tukio husika, pia namna moto ulivyoanza na kuongezeka kwa kasi kwa kuangalia kupitia kamera za CCTV," alisema Chalamila.
Mbali ya hilo, alisema uchunguzi wa kamati umebaini changamoto zilizojitokeza wakati wa kupambana na moto, ikiwamo ukosefu wa msukumo wa maji ya kuzima moto eneo la Kariakoo siku ya tukio.
Nyingine ni uhaba wa maji katika visima vya kuzima moto na kwamba, vilivyopo ni vichache visivyotosheleza Mkoa wa Dar es Salaam.
"Kumekuwa na ujenzi holela eneo la Kariakoo Mnadani, ambao haujahusisha uwekaji wa miundombinu ya njia za dharura na kuwapo ujenzi uliotumia mbao uliochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa moto kwa kasi," alisema.
Chalamila alisema eneo hilo pia lilihusisha uuzaji wa vifaa asilia ya vimiminika vinavyowaka na kulipuka vyenye mgandamizo wa gesi.
Alisema pia kulikuwa na ucheleweshaji wa kutoa taarifa ya wito wa tukio la moto kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Kuhusu hasara ya mali iliyoteketea, Chalamila alisema baada ya kamati kubaini chanzo cha moto wataanza tathimini ya mali na majengo kujua ni madhara kiasi gani yalitokea.
Moto uliteketeza maduka na vibanda kadhaa katika eneo hilo lililotumika kuuza vifaa vya magari vilivyotumika. Pia ilidaiwa lilitumika kuuza vilivyoibwa kwenye magari ya watu.
Mapendekezo ya kamati
Alisema kamati imependekeza wafanyabiashara hao watafutiwe eneo lingine la kufanyia biashara hiyo kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu.
Kamati imeshauri halmashauri kuzingatia sheria zinazoelekeza upangaji wa mji na majengo kwa kuacha njia za dharura wazi baina ya jengo na jengo, pia waliokiuka na kuziba njia wachukuliwe hatua za kisheria.
Imependekeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kufanya mapitio ya kampuni ya Kariakoo Auction Mart, ili kupata uhalali wa umiliki na namna ya uendeshaji wake.
"Inapaswa kuwekwa mipango madhubuti ya uendelezaji wa eneo hilo kwa kuweka miundombinu ya kisasa inayofanana na mazingira ya kibiashara katika mji ili Serikali ipate mapato na kutoa elimu kwa wamiliki wa majengo na wafanyabiashara kukata bima," inaeleza ripoti hiyo.
Wafanyabiashara
Aliyewahi kuwa kiongozi wa Kariakoo Mnadani, Siasa Mohamed alisema kama ni hujuma lazima ijulikane nani aliyefanya na akamatwe, lakini wafanyabiashara wabaki eneo hilo kwa kuwa ni lao na wana hati miliki.
Mfanyabiashara katika eneo hilo, Juma Said alisema haiwezekani wao kuondolewa na iwapo ni suala la hujuma atafutwe aliyefanya hujuma hiyo.
"Kaangalie hatimiliki ya Kariakoo Mnadani utaona kila kitu hadi kodi ya Serikali tunalipa. Viongozi tuliwashtaki kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa ni wezi, hatukubali labda aje Rais au Waziri Mkuu."
Naye Moshi Mahita alisema, "Kama taarifa inashauri tuondolewe huu ni uonevu, kuna kipindi wafanyabiashara walihamishwa Gerezani na kupelekwa Tabata, kwetu ilishindikana kwa kuwa ilionekana ni eneo letu rasmi," alisema.