Rungu la Mchengerwa lawafikia DED Kibaha, Ifakara

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa
Muktasari:
- Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amewasimamisha kazi Wakurugenzi wa Halmashauri za Kibaha (Pwani) na Ifakara (Morogoro) kuanzia jana Novemba 20, 2023 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha mkoani Pwani, Butamo Ndalahwa pamoja na wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Morogoro, Lena Nkaya kupisha uchunguzi.
Kusimamishwa kwa wakurugenzi hao kumekuja baada ya Mchengerwa kupokea taarifa ya awali ya timu iliyoundwa kuchunguza tuhuma za kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo katika halmashauri zao kwa nyakati tofauti.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo Novemba 21, 2023 na kitengo cha mawasiliano cha wizara hiyo, wakurugenzi hao wamesimamishwa kuanzia jana Novemba 20, ili kupisha uchunguzi wa kina juu ya tuhuma hizo.
Taarifa imeeleza kuwa timu iliyoundwa na katibu mkuu wa wizara hiyo kwa maelekezo ya Mchengerwa imebaini mapungufu ikiwemo kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo.
“Mchengerwa amewasimamisha kazi kwa kuzingatia Kanuni ya 37 (1) na 38 (1) ya kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2022 ili kupisha uchunguzi. Vilevile Waziri ameendelea kusisitiza kuwa hatosita kuchukua hatua stahiki kwa atakayethibitika kushindwa kusimamia majukumu yake ,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, amewasisitiza wakurugenzi wote wa mamlaka za Serikali za mitaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo.