Mbunge atoa kioja akiuliza swali kuhusu tohara

Muktasari:
Serikali imesema licha ya faida ya tohara kwa wanaume, haiwezi kuwalazimisha kutahiriwa.
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia ameitaka Serikali itoe agizo kuwa tohara kwa wanaume ni lazima ili kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Wakati akisema hayo, Mbunge Konde, Khatib Said Haji ametaka wabunge wanawake watoe ushahidi kuhusu wanaume waliofanyiwa tohara.
Ghasia aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne amesema leo Jumanne kuwa, Serikali inaweza kulazimisha mambo mengine kufanyika, hivyo amehoji inashindwa nini kuwabana wanaume wote na kuhakikisha wanatahiriwa.
Amesema iwapo watatahiriwa watapunguza gharama za Serikali katika kuwahudumia wanaougua Ukimwi.
Katika swali la nyongeza, mbunge wa Konde, Khatib alimtaka Spika aruhusu wabunge wanawake watoe ushahidi ili uwe uthibitisho wa kile alichosema kwamba, wanaume waliofanyiwa tohara wamekuwa wakinogesha mambo fulani.
“Mheshimiwa Spika, Bunge la Zimbabwe waliamua kuweka sehemu ya tohara nje na kwa kuwa imethibitika kuwa wanaume waliofanyiwa tohara wamekuwa rijali zaidi, hivyo tuwaombe wabunge wanawake watoe ushahidi huo kama ni kweli,” amesema Khatib.
Spika wa Bunge, Job Ndugai alikataa swali la Khatib lisijibiwe akisema haliko katika mtindo wa maswali ya kibunge.
Hata hivyo, aliingiza utani akisema utafika wakati wa kuwakagua kauli iliyosababisha wabunge kuangua kicheko.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla amesema upo ukweli wa tohara kwa wanaume kupunguza maambukizi ya VVU kwa asilimia 60.
"Naomba sana wanawake mlioolewa na wanaume ambao hawajatahiriwa, washawishini kwa upole, tena kwa upendo ili wakatahiriwe," amesema Dk Kigwangalla.
Katika jibu la swali la Mbunge Ghasia, Naibu Waziri Kigwangalla amesema si rahisi kwa Serikali kuagiza tohara kuwa lazima kwa wanaume wote nchini ijapokuwa ina faida kiafya.
Amesema wizara iliweka mkakati wa kubaini mikoa ya kipaumbele ambayo haina utamaduni wa kutahiri ambayo ni Iringa, Njombe, Tabora, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera na Mara.
Dk Kigwangalla amesema elimu kuhusu tohara imefikishwa kwa wananchi kwa kiasi kikubwa na kwamba, Serikali kwa kushirikiana na wadau katika mikoa ya kipaumbele imekuwa ikifanya hivyo kabla ya tohara kufanyika katika vituo vya kutolea huduma.
Amesema Serikali iliendesha kampeni ya tohara maarufu kama “dondosha mkono sweta” ambayo iliwezesha elimu kuhusu tohara kutolewa kupitia matangazo na vipindi vya redio na runinga, mabango, machapisho, vijarida, filamu na waelimisha rika.
Pia, amewataka wananchi kuacha kufanyiwa tohara mitaani, badala yake waende katika vituo vya afya ambako kuna wataalamu.