Mbarawa awashukia ‘miungu watu’ Tasac

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na watendaji na watumishi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac).
Muktasari:
- Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa awataka wafanyakazi kuwa wamoja, ili kuongeza ufanisi, huku akiahidi kuwashughulikia watumishi wababe.
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema ‘atasafisha’ baadhi ya watendaji wa Shirika la Wakala wa Meli nchini (Tasac) wanaojifanya ‘miungu watu’ huku wakiwakandamiza wengine.
Waziri Mbarawa amesema hayo leo, Alhamisi Novemba 23, 2023 alipozungumza kwenye kikao kazi cha shirika hilo kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kueleza hayo, Profesa Mbarawa amesema Tasac kuna shida mahali, kwani kwa nyakati tofauti amekuwa akipokea malalamiko kuhusu utendaji wa watumishi wa taasisi hiyo.
“Nimekuja kusikiliza changamoto zenu, lakini nataka niwaambie jambo moja wale waliojifanya ‘miungu watu’ Tasac wanaondoka hilo halina mjadala. Kuna mtu yeye kila siku anahamisha watu…Hili sio shirika lako, unaamuaje kila siku unahamisha watu?” amehoji Mbarawa na kuongeza;
“Tumepewa dhamana sisi ndio viongozi, lazima tukae na watu, si kuamua fulani unaondoka, hata ukienda katika kampuni za familia watu hawafukuzwi hivyo. Nasema wazi kama upo unaondoka utajua mwenyewe, narudia mara tatu unaondoka huna cha kujitetea, bora uondoke ili taasisi iwe salama.”
Katika kuonyesha amechukizwa na hatua za mtendaji huyo, Profesa Mbarawa amesema: “Hatutaki kumuonea mtu, lakini hatutaki watu wawe juu ya wenzao, wote ni wafanyakazi wa Serikali, lazima tusimamie sheria na taratibu.”
Wazir huyo mwenye dhamana ya Uchukuzi nchini amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha viongozi wake wanawaweka watumishi pamoja, badala ya kuwagawa hali itakayosababisha kushusha ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi.
“Nimekuja kuwapa ujumbe wanaojifanya wababe muda wao umekwisha, tunataka kuleta maendeleo ya nchi, siyo wote ni wabaya lakini kuna changamoto, bora zaidi tufanye leo ili kesho tuwe salama zaidi,” amesema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum amewataka watumishi na watendaji kutumia kikao hichokueleza changamoto zao.
“Hii ndiyo fursa, ikitokea nafasi kama hii tuitumie. Sitegemei kesho au kesho kutwa unakuja ofisini kwangu unaniletea maneno wakati mwenye mamlaka amekuja kuwasilikiliza,” amesema Salum.
Mmoja wa wafanyakazi wa Tasac, Kapteni Alex Katama amesema baadhi ya watumishi wanaondoka katika taasisi hiyo kutokana na kutopandishwa vyeo, licha ya kufanya kazi vizuri na wakiuliza wanaambiwa ni miongozo ya Serikali.
Akijibu suala hilo, Profesa Mbarawa amesema kila mwenye sifa anastahili kupanda cheo, hakuna sababu ya kuzuia suala hilo na kama kuna taratibu za kisheria ziwasilishwe wizarani zitafanyiwa kazi.
Kuhusu uhaba wa wakaguzi katika taasisi hiyo, Profesa Mbarawa amesema hilo ni kosa la Tasac, si wizara yake, akitolea mfano mashirika mengi likiwemo la Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCCA), ambao wana wakaguzi wengi, licha ya kutumia gharama kubwa.
“Nyie Tasac hamsomeshi, wenzenu wanasomesha. Ni aibu fedha mnapata lakini hamsomeshi, kikubwa utaona watu wanakwenda London, hizi taarifa utazisikia kila mwaka. Somesheni watu msiwe wachoyo, taasisi haitojengwa na watu ambao kila siku wanakwenda London,” amesema na kuongeza;
“Hamsomeshi kwa sababu ni wabinafsi, mkienda London mnakuwa sita hadi saba, Mohamed (Mkurugenzi Mkuu), wasaidie hawa. Yaani nyie mtu aandika kwenye magropu kuwa anamuamisha huyu na yule hamsemi, kwanini asiandike barua hawa na wale kusoma.”