Bandari Lagosa yafikia asilimia 96, kukuza uvuvi

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.
Muktasari:
- Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kukamilika kwake ni fursa ya kiuchumi na huduma mbalimbali na mataifa ya Burundi, Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Kigoma. Ujenzi wa Mradi wa Bandari ya Lagosa wilayani Uvinza katika Mkoa wa Kigoma unatarajiwa kukamilika Aprili mwakani sasa umefikia asilimia 96.
Hatua hiyo imeelezwa leo Jumatatu, Oktoba 9, 2023 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ambaye amesema mradi huo utakuwa fursa kwa wananchi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Amesema itakapokamilika bandari hiyo, itachagiza kuimarika kwa shughuli za uchumi hasa kilimo, uvuvi na biashara.
"Nawapongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa ujenzi wa bandari hii, kazi iyofanyika hadi sasa ni nzuri na inahitaji kukamilishwa ili ianze kuhudumia wananchi mapema mwakani," amesema.
Hata hivyo, amesema bandari hiyo itafungua fursa ya soko la huduma katika mataifa jirani ya Burundi, Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
"Serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya bandari na meli ili kunufaika na fursa hizi za kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla," amesema.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo, Naibu Mkurugenzi wa TPA, Mhandisi Juma Kijavara amesema wakandarasi wanatarajia kurejea kazini baada ya wiki mbili kukamilisha mradi huo.
"Changamoto iliyochelewesha mradi ni kuongezeka kwa kina cha maji katika Ziwa Tanganyika, wataalamu wametushauri hatua za kuchukua na tumekubaliana nao kuanza kazi mara moja," amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dina Mathamani ametaka mradi huo ukamilike kwa wakati ili kuwahudumia wananchi na kuwa chanzo cha mapato kwa wilaya hiyo.
Umbali kutoka bandari hiyo hadi Mji wa Kalemie nchini Congo ni takribani kilomita 88, jambo linalotarajiwa kuvutia wafanyabiashara wengi kutoka Congo.