Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumizi ya umeme Tanga, Arusha yapaa, Tanesco yasaini mkataba kuyakabili

Muktasari:

  • Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limetia saini ya makubaliano ya uendelezaji na ujenzi wa njia za umeme na Kampuni za Gridworks ya Uingereza na Larsen & Tourbo ya India kutoka Chalinze kupitia Segera mpaka Tanga, na kutoka Chalinze, Segera, Same na Kisongo.

Dar es Salaam. Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limetia saini ya makubaliano ya uendelezaji na ujenzi wa njia za umeme na Kampuni za Gridworks ya Uingereza na Larsen & Tourbo ya India.

Mkataba huo unahusisha utekelezaji wa miundombinu hiyo kutoka Chalinze kupitia Segera mpaka Tanga, na kutoka Chalinze, Segera, Same na Kisongo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande amesema hatua hiyo ni kufuatia kuongezeka kwa matumizi ya umeme katika mikoa ya Tanga na Arusha kwa sababu ya viwanda na shughuli za uchumi kuongezeka hivyo kusababisha njia za kupitisha umeme kuzidiwa.

"Kwa kipindi cha muda mrefu tumechelewa kutekelezeka miradi kama hii kwa kukosa fedha lakini kwa mara ya kwanza tunasaini makubaliano na sekta binafsi kuendeleza sekta hii," amesema Chande.

Chande ameongeza shirika la Larsen & Tourbo (L&T) litaendeleza na kujenga njia hizo kisha Tanesco litalipa kidogo kidogo kurejesha gharama za ujenzi zilizotumika.

"Wakijenga tutaharakisha maendeleo kwa wananchi wa Tanga na Arusha badala ya kusubiri mpaka kibubu chetu kijae huku maendeleo yanachelewa," amesema.

Aidha amesema pande zote mbili zitaketi kupanga gharama za mradi huo na kukubaliana na pia ipo nafasi ya Tanesco kuchukua na kuendesha mradi huo endapo fedha zikipatikana.

"Tunatarajia mradi huu kutumia miezi 30 mpaka kukamilika kwake, miezi 12 kwa ajili ya Utayarishaji na miezi 18 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi," amesema.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Gridworks, Simon Hodson, amesema uwekezaji katika usafirishaji wa nishati ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na upatikanaji wake barani Afrika.

"Miundombinu ya usafirishaji umeme inahitaji mtaji ili kuongeza uwezo wake na kusaidia upatikanaji wa kiwango cha kutosha katika maeneo husika ili kukuza uchumi," amesema Hodson.

Naye Makamu wa Rais wa L&T, Rahul Sikka, amesema mradi huo ni fursa kwao Kwani utachukua jukumu muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa nishati na kutegemewa nchini Tanzania.

"Mradi huu utaimarisha mtandao wa usambazaji umeme unaounganisha maeneo muhimu ya nchi, kutengeneza njia ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuunda fursa kwa biashara zaidi kustawi, na kuboresha hali ya jumla ya maisha kwa jamii za wenyeji," amesema Sikka.