Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh1.4 trilioni kutumika ujenzi mgodi wa dhahabu Sengerema

Muktasari:

  • Mgodi huo utaanza uzalishaji rasmi wa dhahabu katika robo ya kwanza mwaka 2027, huku ukitarajiwa kuzalisha ajira na mapato kwa Serikali.

Dar es Salaam. Kampuni ya Perseus ya nchini Australia imetangaza kuanza ujenzi wa mgodi wa dhahabu wa Nyanzaga uliopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

Mgodi huo utakaomilikiwa na Kampuni ya Ubia ya Sotta ambapo Kampuni ya Perseus ina umiliki wa hisa za asilimia 84 na Serikali ina umiliki hisa zisizofifishwa za asilimia 16. Mradi wa ujenzi wa mgodi huo  utagharimu Sh1.4 trilioni.

Kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu Aprili 28, 2025 mgodi huo mkubwa unatarajiwa kuanza kuzalisha rasmi dhahabu katika robo ya kwanza ya mwaka  2027,  huku ukizalisha ajira na mapato kwa Serikali.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu sekta ya madini itangazwe kuchangia asilimia 10 katika Pato la Taifa.

Aprili 23, 2025 akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alisema sekta ya madini imepiga hatua kubwa na ya kihistoria kwa mchango wake kufikia asilimia 10.1 kwenye pato la Taifa mwaka 2024.

Alibainisha lengo lililowekwa kwenye Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/2022-2025/2026 ni kuwa sekta hiyo ifikie asilimia 10 kwenye pato la Taifa.

"Ni jambo la kujivunia kuona kuwa juhudi za Serikali na wadau wa sekta hii zimezaa matunda. Mwaka 2023 tulikuwa na mchango wa asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa. Leo hii, tunazungumza kuhusu ongezeko hadi asilimia 10.1 kwa mwaka 2024," alisema Mavunde.

Hata hivyo mara baada ya kutoka kwa tangazo la leo Jumatatu, Waziri Mavunde, amesema ni taarifa njema kwenye kukuza sekta ya madini na ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imeweka mazingira mazuri yanayoendelea kuvutia uwekezaji mkubwa nchini.

"Kutolewa kwa tangazo hilo na Kampuni ya Perseus kumeleta matumaini makubwa na kukata kiu ya wananchi wa Sengerema ambao wameusubiri mradi huo kwa muda mrefu.

"Sasa ndoto yao inakwenda kutimia kwa kuona mradi mkubwa wa kuzalisha dhahabu unaanza ambao utasaidia upatikanaji wa mapato ya serikali, ajira kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Sengerema na nchi kwa ujumla," amesema.

Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya madini nchini ili kufanikisha azma yao na  kukuza uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

Hata hivyo shughuli za awali za kujenga mradi wa Nyanzaga zilizokuwa zinaendelea ni pamoja na kuanzishwa eneo la kufanyia kazi, ujenzi wa kempu pamoja na kutekeleza Mpango wa Utekelezaji wa Uhamisho (RAP) na kujenga makao mapya kwa watu walioathiriwa na mradi.

Aidha kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Perseus, Jeff Quartermaine amesema uamuzi wa kuwekeza kwenye mradi wa dhahabu ni hatua muhimu ya kufanya kazi pamoja na Serikali ya Tanzania, katika kufanikisha operesheni ya uchimbaji madini yenye hadhi ya kimataifa.

Amesema, mradi huo uliopatikana Mei 2024 kupitia kampuni ya OreCorp Limited, utakuwa wa kwanza katika mgodi mkubwa wa dhahabu nchini Tanzania katika kipindi cha miaka 17.

Wachumi wanena

Mwananchi limezungumza na wachumi juu ya hatua hiyo. Profesa Abel Kinyondo amesema ni habari njema kwa kuwa nchi inavutia wawekezaji.

"Dalili nzuri ya mazingira ya kibiashara katika sekta ya madini, kama mkataba hautabanisha ushirikishwaji wa maana wa wananchi kwenye huo uwekezaji, mafanikio hayatakuwa makubwa kama inavyotakiwa," amesema Kinyondo.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Mwinuka Lutengano amesema ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa kuwahi kufanyika nchini.

"Ni kweli pia, eneo la madini linahitaji mtaji mkubwa na teknolojia sahihi ili kuwekeza kwa tija. Tunahitaji uvumilivu kidogo ili kuja kupata na kuziona faida za moja kwa moja na matokeo mapana ya kiuchumi," amebainisha.

Mchumi Oscar Mkude amesema kwa ujumla ni fursa nzuri kiuchumi, kwani mradi wake utaongeza kwenye kiasi cha uzalishaji kwa mwaka na hivyo kuongeza mapato na ajira.


Hata hivyo, kwa mwenendo wa uchumi wa sasa, nchi  zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara hazipaswi kuendelea na namna hii ya uwekezaji.

"Lazima tuweke mkazo kisera kwenye kuongeza thamani.

"Pia, kuchimba pekee hakuzalishi kazi zenye ubora sana kama kungekuwa na kuongeza thamani / kuchakata madini hapa nchini na kuuza bidhaa za mwisho,"amesema

Ameongeza huo ndiyo uchumi utakaosaidia nchi zetu kutengeneza fedha na kupunguza athari za migogoro ya kiuchumi.

Aidha utasaidia kuongeza ajira bora zaidi na kutanua kupeleka nje bidhaa ambazo tunaziuza nje ya nchi.