Prime
Heche ahoji Polisi kuzingira makazi yake na ya Lissu, Kamanda Muliro amshangaa

Muktasari:
- Muliro ashangaa madai ya Heche Polisi kutanda nyumbani kwake asema kwa kitendo hicho pekee alipaswa kushukuru kwa kulindwa kwani, amekuwa akipokea simu nyingi za shukurani kwa raia wanaopata huduma ya jeshi hilo.
Dar es Salaam. Wakati John Heche akisema askari Polisi wamezingira makazi yake na ya Tundu Lissu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amemshangaa makamu huyo mwenyekiti wa Chadema bara akisema alipaswa kushukuru na kupongeza hatua ya jeshi hilo kumuimarishia ulinzi.
Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi linafanya kazi katika maeneo mbalimbali bila ubaguzi kuimarisha ulinzi na wamekuwa wakipokea simu nyingi za wananchi kulishukuru kwa kuwasogezea ulinzi karibu.
“Hivyo Heche alipaswa kushukuru y kupelekewa ulinzi nyumbani na sio kulalamika.”

Heche kupitia mtandao wake wa X saa 2:21 asubuhi aliweka ujumbe ukisema: “Nimezingirwa nyumbani kwangu tangu saa 10 alfajiri ya leo. Askari wakiwa na magari manne wapo kwenye milango ya kuingilia.”aliandika Heche anayeishi Salasala.
Kabla ya ujumbe huo, saa 2:06 asubuhi, Heche aliandika: “Tangu saa sita usiku polisi wamezingira nyumbani kwa Lissu, wamejaribu kuingia ndani, lakini ndugu wamewaambia kama wanataka kufanya ukaguzi lazima mwenye nyumba awepo.”
Ujumbe huo wa Heche ulianza kusambaa mitandaoni huku baadhi ya picha zenye kuonesha askari wakiwa nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chadema, Lissu Tegeta, Dar es Salaam zilisambaa na kuibua mijadala.

Polisi wakiwa ndani ya gari lao wakiwa katika majukumu yao ya kuimarisha ulizi katika maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Jumatatu Aprili 28, 2025.
Tukio hilo limetokea ikiwa leo Jumatatu, Aprili 28, 2025 kulikuwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo inayomkabili Lissu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Tangu kuahirishwa kwa kesi hiyo Aprili 24, 2025 hadi leo Jumatatu kwa ajili ya kutoa uamuzi wa ama kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya mtandao ama la, viongozi mbalimbali wa Chadema akiwemo Heche walikuwa wakiwahamasisha wanachama na wananchi kufika Kisutu kufuatilia mwenendo wa kesi ya kiongozi huyo.
Uamuzi kesi hiyo itasikilizwa kwa njia ya mtandao ama Lissu kufikishwa kortini utatolewa. Katika kesi nyingine ya Lissu ya uhaini, Mahakama imekwisha kutoa uamuzi wa kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Alichokisema Muliro
Baada ya mijadala ya askari Polisi kuwapo nyumbani kwa Heche na Lissu, Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Kamanda Muliro ofisini kwake ambapo amesema, jeshi hilo muda wote linafanya kazi kwa weledi na halina ubaguzi katika kutekeleza majukumu yake.
Akijibu suala la Polisi kwenda kwa Heche amesema: "Jukumu la askari siku zote ni kuimarisha ulinzi sehemu mbalimbali, sehemu yeyote tunakohisi kuna viashiria vya uvunjivu wa amani.”
“Askari wakiwa kwako nadhani unapaswa kushukuru Mungu kwamba uko salama, kupata fursa ya askari kuja kwako huo ni upendeleo."
Kamanda huyo amesema taasisi hiyo ina watumishi wachache kulingana na ukubwa wa eneo wanalopaswa kusimamia na kufanya doria mara kwa mara.
"Kwembe kuna askari, Banana, Tegeta, Chanika kwa Zoo, Gongolamboto kote huko wapo, wakija kwako unashangaa nini badala ya kushukuru, kwamba Serikali imekujali kukuletea ulinzi na wananchi wanatupigia simu kutushukuru wewe unashangaa nini badala ushukuru," amesema.
Kulingana na maelezo ya Kamanda Muliro wenye tabia za uhalifu ni wale wote wanaokuja na mitazamo ya hofu baada ya Polisi kuzingira kwao.
"Wewe si muhalifu inakuaje unamuona askari unaanza kuwa na woga. Tunafanya kazi zetu kwa weledi bila kubagua nyumba hii anakaa kiongozi wa chama fulani kwamba tusiende kote tunaenda ili mazingira yetu yawe salama,” amesema.
"Nashangaa nyie mnaoshangaa au mnataka tufanye kazi kwa ubaguzi tuchague nyumba kwamba wewe ni chama gani? askari wakija kwako wewe lala na wakiwa wengi unapaswa kushukuru zaidi," amesema Muliro.
Kuhusu usalama wa mkoa huo amesema:"Maeneo yote Dar es Salaam hali ni nzuri, kama ambavyo tumekuwa tukifanya jana, juzi na wiki iliyopita, Dar es Salaam ni mji wa hekaheka, wa kiuchumi na kisiasa usalama umeimarishwa, kwa hiyo maeneo yote usalama umeimarishwa."
‘Wanatengeneza taharuki’
Baada ya maelezo hayo ya Kamanda Muliro, Mwananchi lilimtafuta Heche bila mafanikio kujua kinachoendelea kwake na tulimpata Naibu Katibu Mkuu Chadema-Bara, Amani Golugwa ambaye amesema kwa Heche walizingira eneo lakini kwa Lissu waligonga hadi geti kutaka wafunguliwe kwa ajili ya upekuzi.
"Walipokataliwa walikwenda kwa Mjumbe wa serikali ya mtaa na kumpigia kijana wa mwenyekiti (Lissu) afungue mlango lakini aliwakatalia kwa kuwa mwenye nyumba hayupo," amesema.
Kulingana na Golugwa amedai kwa Heche walikwenda kuzingira hoteli (jina tunalihifadhi) alikokuwepo kiongozi huyo na walishusha nguvu ya mawasiliano ya simu eneo hilo.
"Hata ofisi zetu za makao makuu ya Chadema zilikuwa zimezingirwa na Jeshi la Polisi. Kitendo hicho ni kuleta taharuki isiyokuwa na sababu za msingi," amesema
Amesema walipozingira kwa Heche hawakuleta taharuki kwa kiongozi huyo pekee bali hata wageni wengine waliokuwa wamelala katika hoteli hiyo.
Kuhusu kauli ya Kamanda Muliro kwamba Jeshi la Polisi lilienda kulinda usalama na wanapaswa kushukuru, Golugwa amejibu kwa kusema Muliro anafanya porojo kwenye masuala makini.
"Polisi walienda kwa Lissu kufanya upekuzi na unapoenda na Polisi wengi unaleta taharuki, kwa hiyo Muliro anafanya porojo si kwamba sisi tunapata hofu bali wanawatengenezea wananchi hofu lakini kusema Polisi walikuwepo kwa ajili ya kutulinda hapo anafanya porojo kwenye mambo siriazi," amesema
Ulinzi Kisutu
Katika mahojiano hayo, Kamanda Muliro amezungumzia ulinzi walioimarisha kwenye viunga vya ndani na nje ya Mahakama ya Kisutu, akisema wamefanya hivyo ili kuhakikisha kesi zote si hiyo ya Lissu tu zinaendelea kama zilivyopangwa.
Katika eneo hilo la Mahakama polisi waliovaa sare na wasio na sare wanafanya doria kwenye magari na mikononi wameshikilia silaha mbalimbali, zikiwemo bunduki na virungu.
Wananchi wa kawaida hasa wale wanaohisiwa kuwa makada wa Chadema pamoja na waandishi wa habari wamezuiwa kuingia ndani ya Mahakama hiyo, lakini hawataki kuona watu wakiwa wameketi eneo karibu na Mahakama hiyo.
Magari ya maji ya washawasha yameegeshwa upande wa makutano ya Hoteli ya Serena pamoja na ulinzi huo bado kuna baadhi ya makada wa Chadema wasiovaa sare walikuwa wanazunguka kuangalia uwezekano wa kuingia.

Polisi wakionekana kwa mbali wakiwa katika majukumu yao ya kuimarisha ulizi katika maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Jumatatu Aprili 28, 2025.
“Kesi zote zinapaswa kuendelea kwa hiyo watu wanafikiri wanataka yao pekee bila kujua ile Mahakama ina mashauri mengine yanayopaswa kusikilizwa kwa uzito uleule na kuwepo na utulivu,” amesema Kamanda Muliro.
“Na ina mahakimu, makarani, mawakili wa utetezi na waendesha mashtaka wa kesi zingine kwa hiyo unapokuja mtazamo kwamba sisi wote twende pale maana yake hutaki shughuli zingine ziendelee," amesisitiza.
"Wanasema sisi tutapajaza pale ndani ina maana wengine wasije Polisi tunalinda ili kesi zingine ziendelee na wanahitaji utulivu sasa ukitaka kuteka eneo lile liwe la kesi yako, wengine watashangaa na kujiuliza wewe ni nani unayetaka kesi yako ni kubwa na ya wengine si kubwa," amesema Muliro.
Muliro amesema kabla ya kesi ya Lissu mahakamani hapo kulikuwa na kesi zingine zilizopangwa kusikilizwa, mahakimu na waendesha mashitaka wapo kwa kazi hiyo.
"Hali ikiwa hiyo mmoja unataka kuteka eneo hilo liwe sehemu yako Jeshi la Polisi tunaingia kuimarisha ulinzi na hatuingilii shughuli za Mahakama, Polisi tunalinda usalama wote wapewe haki sawa, sasa ukitaka wewe kuiteka Mahakama hiyo nafikiri si sawa," amesema.