Mashuhuda wasimulia ajali iliyoua wanakwaya sita

Same. Mashuhuda wa ajali iliyoua wana kwanya sita na kusababisha majeruhi 23 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mmeni, Dayosisi ya Pare, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, wameeleza namna ajali hiyo ilivyotokea.
Ajali hiyo imetokea leo Machi 30, 2025 saa nne asubuhi, Barabara ya Bangalala, wilayani humo wakati wana kwanya hao wakitokea Chome kuelekea Vudee kwa ajili ya shughuli ya uinjilishaji.
Sambamba na ajali hiyo pia, kulitokea ajali nyingine eneo la Njoro Wilayani humo iliyohusisha basi la Kampuni ya Osaka lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar es salaam na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 53 ambao wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Same na wengine wamehamishiwa Hospitali ya KCMC.
Akizungumza na Mwananchi, shuhuda wa ajali hiyo, ambaye pia ni miongoni mwa waimbaji wa kwaya hiyo, Eliazina Edson amesema wakati gari linapanda mlima lilipata hitilafu na kuanza kuserereka na kuangukia kwenye maporomoko ya milima ya Pare.
"Tulikuwa tunatokea Mmeni Chome baada ya kualikwa na wenzetu wa Ndolwa, hivyo hatukuweza kufika kutokana na ajali iliyotukuta,” amesimulia mwanakwaya huyo na kuongeza;
“Wenzetu wengine wamevunjika na wengine wamefariki hapo hapo.”
Shuhuda mwingine, Mwajuma Omari amesema wakati akiwa nyumbani kwake alisikia mngurumo wa gari na alipotoka nje alisikia watu wakipiga kelele kuashiria kuna tatizo na aliposogea alishuhudia watu wengi wakikimbilia eneo la tukio.
"Mjukuu wangu aliniambia bibi toka nje kuna gari limedondoka, nilipotoka nilisikia watu wanapiga yowe huko mlimani, tuliposogea eneo la tukio tukakutana na hii ajali,” amesema Omary.
Akizungumzia kupokea miili na majeruhi, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dk Alex Alexandra amesema wamewapokea majeruhi 75 na miili ya watu saba waliokuwa kwenye magari tofauti.
"Leo tumepokea majeruhi 75 ambao wametoka kwenye gari mbili tofauti, basi la kwanza lilipata ajali saa saba usiku likiwa na majeruhi 53 lakini asubuhi ya leo tumepata majeruhi 23 waliokuwa kwenye Coaster na miili sita, wanaume wawili na wanawake wanne na asubuhi kifo kilikuwa kimoja hivyo vifo vimekuwa saba,” amesema Dk Alexander.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amesema hilo ni kubwa kwa kuwapoteza watu saba na majeruhi 75 ambao wanaendelea kupatiwa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Same na baadhi KCMC.
"Siku ya leo kwetu haikuwa nzuri kutokana na ajali mbili zilitokea, tumepoteza wanakwaya sita na mwananchi mwingine ambaye alifariki kwenye ajali ya basi iliyotokea usiku na majeruhi 75,” amesema DC Mgeni.
Hata hivyo amemshukuru mganga mkuu wa wilaya hiyo, kwa kufanya kazi tangu ajali hizo zilipotokea na kuhakikisha majeruhi wanaendelea na matibabu.
Aidha, ametoa angalizo kwa madereva wanaotumia barabara ya Same, kuhakikisha wanakuwa waangalifu kutokana na Wilaya hiyo kuwa na upepo mkali.
"Naendelea kuwaomba madereva kuwa waangalifu wanapobeba abiria, wakumbuke wamebeba roho za watu, wawe waangalifu wanapokuwa kwenye barabara zetu za Same,” amesema Mgeni.
Ndani ya siku 164, Barabara ya KIA-Moshi-Same imesababisha vifo vya watu 25 kuanzia Oktoba mwaka jana mpaka Machi 30 mwaka huu.
Oktoba 22, mwaka jana, waimbaji watano wa Kwaya ya Umoja ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Wazo Hill, Mkoani Dar es Salaam, nao walifariki dunia huku wengine 20 wakijeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Caoster kuacha njia na kupinduka eneo la Kirinjiko, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Ajali hiyo ilitokea ikiwa zimepita siku tano tangu itokee ajali nyingine iliyoua watu 14 na majeruhi kadhaa usiku wa Oktoba 18, mwaka 2024 katika daraja la Kikafu lililopo Wilaya ya Hai, Kilimanjaro pia.
Ajali hiyo ilitokea baada ya lori kugongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Coaster iliyokuwa imebeba abiria kutoka Moshi kwenda jijini Arusha.
Wananchi wafunguka
Amon Paul, mmoja wa wakazi wa mkoa huo, amesema ajali nyingi zinazotokea katika Wilaya ya Same husababishwa na upepo mkali unaovuma kwenye barabara kuu ya Moshi-Same-Dar es Salaam, hasa katika maeneo fulani ya wilaya hiyo, hali ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu.
"Barabara kuu za Same ni hatari sana. Haipiti wiki bila kusikia ajali, mimi mwenyewe niliwahi kupata ajali eneo la Kirinjiko, lakini kwa neema ya Mungu tulinusurika," amesema.
Mtumiaji mwingine wa barabara hiyo, Agnes Kawau amesema changamoto kubwa katika Wilaya ya Same ni wembamba wa barabara, jambo alilosema ni moja ya chanzo cha ajali nyingi.
Ameiomba Serikali ichukue hatua za haraka za kupanua barabara hiyo ili kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara.