Prime
Marekani kujiondoa WHO pigo kwa nchi maskini

Muktasari:
- WHO ambayo imeanzishwa mwaka 1948 huku Marekani ikiwa miongoni mwa nchi waasisi ikiwa na nchi wanachama 193, kwenye taarifa yake inaeleza kuwa, miaka saba imekuwa ikifanya maboresho ya utendaji wake
Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kujiondoa katika Shirika la Afya Duniani (WHO) umeibua mjadala miongoni mwa wadau wa afya nchini.
Wadau wanasema hatua hiyo ni pigo kwa mataifa yanayoendelea nan chi maskini, ikiwamo Tanzania, inayotegemea msaada mkubwa wa WHO katika kukabiliana na changamoto za afya.
Hatua hiyo ya Marekani inakuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus yaliyolenga kujadili udhibiti wa Ugonjwa wa Marburg uliojitokeza nchini.
WHO iliahidi msaada wa Dola 3 milioni za Marekani kwa Tanzania kudhibiti ugonjwa huo, pamoja na Dola 50,000 kwa ajili ya uchunguzi.
Athari za kujiondoa WHO
Wakizungumza na gazeti hili, wadau wa masuala ya afya nchini, wamesema Marekani kujiondoa WHO ni pigo kwa mataifa yanayoendelea ikiwamo Tanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphfta) Dk Egina Makwabe amesema ni pigo kubwa si kwa Tanzania peke yake bali kwa dunia nzima.
Dk Makwabe amesema Marekani inachangia asilimia 30 ya bajeti ya WHO, “ukiangalia upande wa chanjo pale Gavi (Shirika la kimataifa linalozalisha chanjo) ule mpango wa kutoa chanjo kwa nchi maskini Marekani ndiyo ilikuwa mchangiaji mkubwa.”
Amesema imekuwa ikitoa fedha nyingi kushughulikia magonjwa kama kifua kikuu, ukoma, Ukimwi na tiba kwa waviu, hayo yote yamekuwa yakishughulikiwa na Taifa hilo, likichangia fedha nyingi kwa asilimia kubwa.
“Inawezekana inajitoa, lakini tusubiri huenda itatoa mchango wake moja kwa moja, lakini kama inajitoa na kusitisha msaada itakuwa kilio kikubwa.
“Kwani inasaidia katika kushughulikia mifumo ya wafanyakazi, baadhi ya dawa za Ukimwi, kifua kikuu, chanjo na matunzo ya programu mbalimbali,” amesema Dk Makwabe.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Mugisha Nkoronko amesema tamko la Marekani limepokewa kwa mshtuko duniani kote.
“Hili ni Taifa kubwa kiuchumi, linapojiondoa uanachama WHO na kuagiza michango yote iliyokuwa katika mchakato wa kutolewa isitishwe inatafakarisha na tunashindwa kujua sababu iliyoifanya Ikulu ya Marekani kufikia maamuzi haya,” amesema Nkoronko.
Dk Nkoronko amesema ijapokuwa Rais Trump ameeleza sababu kadhaa ikiwamo uwezo mdogo ambao WHO ilionyesha katika kushughulikia Uviko-19 Marekani na kwamba limeona halina uwezo kushughulikia magonjwa na kuifanya Marekani ijitoe.
“Shirika kwa sasa liko katikati ya mtanziko (njia panda) kushughulikia watu bilioni nane ambao sasa afya zao ziko shakani kama asilimia 30 ya mapato itaondoka. Binafsi naitafsiri hii kama vita ya kiuchumi miongoni mwa mataifa mawili makubwa Marekani na China,” amesema.
“Marekani ni nchi mwanzilishi, imekuwa na mchango mkubwa wa kifedha kuifanya dunia kuwa mahali salama, hatujasikia kitaaluma na kiteknolojia. Tunadhani demokrasia inaweza kutumika kunusuru hili, lakini hii ni ‘wake up call’ mataifa yote yana jukumu la kuweka fedha WHO wote tuwajibike kuifanya dunia kuwa mahala salama pa kuishi.”
Kauli ya WHO
WHO ambayo imeanzishwa mwaka 1948 huku Marekani ikiwa miongoni mwa nchi waasisi ikiwa na nchi wanachama 193, kwenye taarifa yake inaeleza kuwa, kwa kipindi cha miaka saba imekuwa ikifanya maboresho ya utendaji wake.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo, inaeleza kuwa WHO ina matumaini na Serikali ya Trump itatafakari kuhusu mazungumzo yatakayoendeleza ushirikiano kati ya Marekani na WHO kwa ajili ya kulinda afya za mamilioni ya watu duniani.
Amri ya kujitoa WHO
Rais Trump kwa amri yake amesema Marekani itasitisha kutoa fedha, usaidizi au rasilimali za Serikali ya Marekani kwa WHO.
Marekani ndiye mchangiaji mkuu WHO kwa kutoa fedha nyingi na watalaamu wa afya kwa kutumia taasisi zake za Serikali.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO, Marekani katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023 imetoa Sh3.25 trilioni.
Marekani mbali na kuchangia fedha pia, inatoa wataalamu na ujuzi kwa kupitia taasisi zake kama vile idara ya afya na huduma za binadamu, Kituo cha Kudhibiti Maradhi cha Marekani (CDC), Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Shirika la Kulinda Mazingira la Marekani (EPA) na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na (PEPFAR).
Wachangia wengine wakubwa wa WHO kwa mwaka 2022-2023 ni Ujerumani Sh2.16 trilioni, Bill & Melinda Gates Foundation Sh2.10 trilioni, Gavi Sh1.21 trilioni, Kamisheni ya Ulaya Sh1.18 trilioni, Uingereza na Northern Ireland Sh1trilioni.
Wengine ni Canada Sh516.46 bilioni, Rotary International Sh448.1 bilioni, Japan Sh422.79 bilioni na Ufaransa Sh407.6 bilioni.
Siyo kauli ngeni
Marekani ilipendekeza kujiondoa kutoka WHO mwaka 2020 kwa sababu ya shirika hilo kushughulikia vibaya janga la Uviko-19 lililoibuka kutoka Wuhan, China na shida nyingine za kiafya za ulimwengu.
Trump katika muhula wake wa kwanza wa Urais, aliilalamikia WHO kushindwa kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa ushawishi usiofaa wa kisiasa wa nchi wanachama wa WHO.
"WHO inaendelea kudai malipo yenye kutaabisha isivyo haki kutoka Marekani, mbali na uwiano na malipo yaliyotathiminiwa ya nchi nyingine. China, yenye idadi ya watu bilioni 1.4, ina asilimia 300 ya wakazi wa Marekani, lakini inachangia karibu chini ya asilimia 90 ya WHO," amesema.
Amesema Marekani inakusudia kujiondoa kutoka kwa WHO ambapo barua ya kujitoa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyotiwa saini Januari 20, 2021, ilibatilisha ombi la Marekani la Julai 6, 2020.
Rais Trump kwa amri yake amesema Marekani itasitisha kutoa fedha, usaidizi au rasilimali za Serikali ya Marekani kwa WHO.
Pia, Trump ameamrisha kuwarejesha nyumbani na kuwapa kazi upya wafanyakazi wa Serikali ya Marekani au wakandarasi wanaofanya kazi katika nafasi yoyote WHO.
Amesema Serikali ya Marekani itatafuta washirika wa kimataifa wanaoaminika na wenye uwazi ili kuchukua shughuli muhimu zilizofanywa hapo awali na WHO.
Pia, ameishutumu WHO kwa kuruhusu ugonjwa wa Uviko -19 kushindwa kudhibitika na kupuuzia hatari ya ugonjwa huo, ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu duniani.
Rais Trump ameilaumu China kwa kujaribu kuziba mlipuko huo na kuishtumu WHO kwa kushindwa kuiwajibisha China.
Pia, amelishutumu shirika hilo kwa kuipendelea China, sehemu ya shutuma hizo zikiwa ni kutokana na upingaji wake mkali wa hatua ya Marekani kuwazuia wasafiri kutoka China kuingia nchini humo huku akiita ugonjwa huo ni ''virusi vya China.”