Trump kuzuia mapenzi ya jinsia moja yawa nafuu kwa Uganda

Muktasari:
- Mwaka 2023, Bunge la Uganda lilipitisha sheria inayotoa adhabu kali kwa vitendo vya uhusiano wa jinsia moja, huku sheria hiyo ikiungwa mkono na wabunge 389 na mmoja pekee kupinga.
Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kusaini amri ya kiutendaji inayopinga mapenzi ya jinsia moja umeonekana kuwa nafuu kwa Uganda, nchi ambayo tayari imeweka sheria kali kupinga vitendo hivyo.
Nafuu hiyo inakuja kutokana na Uganda kuwa ilikuwa imebanwa na utawala uliondoka madarakani wa Rais Joe Biden, aliyeitaka Serikali ya Rais Yoweri Museveni kuifuta sheria hiyo.
Trump, aliyeapishwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani jana, januari 2025, ameahidi kufuta sera za utawala wa Rais wa 46, Joe Biden, zilizokuwa zikihamasisha mapenzi ya jinsia moja.
Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa, Trump amesisitiza kwamba Marekani inatambua jinsia mbili pekee: mwanaume na mwanamke.
Ametangaza kuwa nyaraka rasmi za Serikali, kama pasipoti na viza, zitarejea kutumia neno “sex” (jinsia ya kike au kiume) badala ya “gender” (ambalo linajumuisha jinsia mbalimbali na tabia binafsi za kijinsia, ikiwa ni pamoja na wale wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja).
Trump katika taarifa yake amesema ametengua amri kadhaa za utawala wa Biden, ikiwemo ya kuwalinda wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Idadi ya wanajeshi wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja ndani ya jeshi la Marekani ni kati ya wanajeshi 9,000 hadi 14,000.
Nafuu kwa Uganda
Sheria ya Trump inakuja wakati ambapo Uganda tayari imeweka msimamo mkali dhidi ya mapenzi ya jinsia moja. Mwaka 2023, Bunge la Uganda lilipitisha sheria inayotoa adhabu kali kwa vitendo vya mahusiano ya jinsia moja.
Sheria hiyo, iliyoungwa mkono na wabunge 389 huku mmoja pekee akipinga, ina mamlaka mapana ya kukabiliana na wanaoshiriki au wanaojitambulisha na jamii ya LGBTQ.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, yeyote anayeshiriki vitendo vya jinsia moja au kujitambulisha kama mwanachama wa LGBTQ anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 10 jela.
Pia, sheria hiyo inatoa adhabu ya kifo kwa “ushoga uliokithiri,” ikiwa ni pamoja na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kupitia uhusiano wa jinsia moja.
Rais Biden alaami sheria ya Uganda
Baada ya Uganda kupitisha sheria hiyo, Rais Joe Biden aliikosoa vikali akidai inakiuka haki za binadamu na kuhatarisha maendeleo ya kiuchumi ya Uganda.
Katika taarifa rasmi, Biden alisema, “Hakuna mtu anayestahili kuishi kwa kuhofia maisha yake au kufanyiwa vitendo vya ukatili na ubaguzi. Sheria hii ni makosa.”
Aidha, alihimiza sheria hiyo kufutwa mara moja na kusema kwamba vitendo kama hivyo vinahatarisha uhusiano kati ya Uganda na mataifa mengine yanayopinga ubaguzi wa kijinsia.
Sababu za Uganda
Kwa upande wake, Uganda ilisema msimamo wake mkali unalenga kulinda maadili na utamaduni wa Taifa.
Rais Museveni alieleza kuwa mapenzi ya jinsia moja ni mwenendo wa upotovu na ukiukaji wa maadili ya jamii ya Kiafrika.
Sheria hiyo inagusa pia wale wanaowasaidia watu wa LGBTQ. Kwa mfano, wamiliki wa nyumba au vyumba vya burudani watakaowakodisha wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wanaweza kufungwa hadi miaka saba jela.
Wengine wanaoguswa na sheria hiyo ni waandishi wa habari na watengenezaji wa filamu wanaoeneza taarifa zinazohamasisha mapenzi ya jinsia moja; wanaweza kupigwa faini ya Sh100 milioni za Uganda.
Zimbabwe iliwahi kupinga
Uganda si nchi pekee barani Afrika yenye msimamo mkali dhidi ya mapenzi ya jinsia moja. Zimbabwe, chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais Robert Mugabe, ilichukua hatua kali dhidi ya wanadiplomasia wa kigeni waliokuwa wakipigia debe mapenzi ya jinsia moja.
Mugabe, ambaye sasa ni marehemu, aliwahi kutangaza kwamba ndoa inaweza kuwa kati ya mwanamke na mwanamume pekee.
Aidha, aliishutumu Ulaya kwa kile alichokiita “kukosa maadili” na kudai kwamba mapenzi ya jinsia moja hayana nafasi katika jamii.