Prime
Prince Harry, Wakenya 30,000 kutimuliwa Marekani

Muktasari:
- Miongoni mwa uamuzi tata ambao Rais Donald Trump anatarajiwa kusaini ni kumtimua Marekani, Prince Harry, mwana wa kifalme wa Uingereza aliyekiri hadharani kutumia dawa za kulevya
Dar es Salaam. Kuapishwa kwa Donald Trump kuwa Rais wa 47 wa Marekani na ahadi yake ya kusaini amri za kiutendaji takriban 200, huenda kukawaondoa nchini humo Prince Harry, Wakenya 30,000 na wahamiaji wengine wanaoishi kinyume cha sheria.
Kufukuzwa kwa Prince Harry, Wakenya na wahamiaji wengine haramu kutoka mataifa mengine ni kutokana na ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni na jana Jumapili kwenye mkutano wake wa hadhara.
Trump aliahidi baada ya kuapishwa atasaini amri za kiutendaji takriban 200 ikiwamo ya kuwafukuza nchini humo wahamiaji wasio na vibali.
Rais huyo aliyeapishwa leo, aliahidi kuwa amri hizo zitakazoanza kutekelezwa hivi karibuni, zitaleta mabadiliko makubwa na kuishangaza dunia.
Amesema hatua ya kuwafukuza wahamiaji haramu ni mojawapo ya ahadi zake za kampeni alizolenga kutekeleza siku ya kuapishwa kwake.
Rais huyo mpya amesema hatua hiyo inalenga pia kuboresha usalama wa Taifa na kuhakikisha rasilimali za Marekani zinatumiwa kwa manufaa ya wananchi wake.
Miongoni mwa uamuzi tata ambao Trump anatarajiwa kusaini ni pamoja na kumtimua Marekani, Prince Harry, mwana wa kifalme wa Uingereza aliyekiri hadharani kutumia dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa sheria za Marekani, matumizi ya dawa za kulevya ni kosa la jinai linaloweza kusababisha mtu kufukuzwa nchini humo, hasa kwa raia wa kigeni.
Wakenya 30,000 kuathirika
Hatua ya kusaini amri hizo za kiutendaji itawaathiri moja kwa moja wahamiaji haramu wapatao 30,000 kutoka Kenya ambao wanaripotiwa kuishi Marekani bila vibali halali.
Idadi hiyo ya Wakenya ni kutokana na takwimu za sensa ya mwaka 2024 ya Marekani, ambayo ilibainisha kwamba, Wakenya wengi wanaishi nchini humo kinyume cha sheria.
Hata hivyo, idadi ya wahamiaji haramu kutoka Kenya kukimbilia Marekani si jambo jipya, kwa sababu takwimu za Idara ya Uchumi na Jamii ya Umoja wa Mataifa za mwaka 2020 zinaonyesha Marekani ilikuwa na jumla ya wahamiaji 157,000 kutoka Kenya.
Idadi hiyo inaiweka Kenya katika nafasi ya tano kati ya nchi za Afrika zenye idadi kubwa ya wahamiaji wanaoishi Marekani.
Nigeria inaongoza orodha hiyo kwa kuwa na wahamiaji wengi zaidi kutoka Afrika.
Pia, takiwmu za idara ya uchumi na jamii ya Umoja wa Mataifa za mwaka 2020 zinaonyesha Marekani ina idadi kubwa ya wahamiaji Wakenya wanaoishi Marekani ambao ni 157,000, ikifuatiwa na Uingereza yenye wahamiaji 139,000.
Takwimu hizo zinaiweka Kenya kuwa nchi ya tano ya Afrika yenye wahamiaji wengi nchini Marekani. Nigeria ndiyo inaongoza kwa idadi kubwa ya wahamiaji nchini Marekani.
Ili kufanikisha lengo lake hilo, Trump alitangaza watakaoshika nafasi za uwaziri kutimiza lengo hilo kama Gavana wa Dakota Kusini, Kristi Noem ambaye alisema atakuwa Waziri wa Usalama wa Ndani huku akisubiri kuthibitishwa na Bunge la Seneti.
Trump katika kampeni zake zote za uchaguzi hoja yake kubwa ilikuwa suala la wahamiaji haramu na hasa kutokana na ongezeko la idadi ya wahamiaji haramu.
Suala la kuwaondoa wahamiaji haramu nchini Marekani kutamkwa na Trumpa si geni, itakumbukwa alipokuwa Rais wa 45 alifukuza wahamiaji 1.5 milioni waliokuwa mpakani na ndani ya Marekani.
Pia, wakati wa utawala wa Joe Biden anayeondoka madarakani, naye aliwafukuza wahamiaji takriban milioni 1.1 huku Rais wa 44 Barack Obama yeye akiwafukuza wahamiaji takriban milioni tatu.
Inakadiriwa kwa sasa Marekani ina zaidi ya wahamiaji haramu milioni 11.
Hatua hii ya Trump imeibua hisia mseto kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na makundi mbalimbali ya haki za binadamu.
Wakosoaji wa sera zake wanasema hatua hizo zinaweza kusababisha mgawanyiko wa familia na kuongeza changamoto kwa wahamiaji wanaotafuta maisha bora nchini Marekani.
Hata hivyo, wafuasi wa Trump wanaona kuwa hatua hizo ni muhimu kwa masilahi ya Taifa na kudhibiti uhamiaji holela.
Kwa upande mwingine, wachambuzi wa kisiasa wanaona kuwa hatua ya kumtimua Prince Harry kutoka Marekani inaweza kuzua mvutano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Uingereza.
Kwa muda mrefu, nchi hizi mbili zimekuwa na uhusiano wa karibu katika masuala ya kidiplomasia, kiuchumi na kijeshi.
Hivyo, uamuzi huu unaweza kuwa na athari kubwa zaidi ya kisiasa kuliko inavyodhaniwa.
Katika miezi iliyopita, Trump alisisitiza mara kadhaa kuwa Serikali yake itachukua hatua kali za kukabiliana na uhamiaji haramu kama sehemu ya mpango wake wa kuimarisha uchumi na kulinda ajira za Wamarekani.
Hata hivyo, wachumi wengine wanaonya kuwa hatua kama hizo zinaweza pia kuwa na athari hasi kwa sekta mbalimbali zinazotegemea wahamiaji, kama vile kilimo, ujenzi na huduma za afya.
Kwa Wakenya wanaoishi Marekani kinyume na sheria, hali hii inazidi kuwa ngumu.
Wengi wao walihamia nchini humo kwa matumaini ya kutafuta maisha bora, lakini sasa wanakabiliwa na hatari ya kurejeshwa nchini mwao.
Baadhi ya wahamiaji hao wameeleza hofu yao, wakisema kurejeshwa Kenya kutawafanya waanze maisha upya katika mazingira magumu.
Hali hii pia imefungua mjadala kuhusu hatua ambazo Serikali ya Kenya inapaswa kuchukua ili kusaidia raia wake walioko Marekani.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanapendekeza kuwa, Serikali ya Kenya inapaswa kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na Marekani ili kuhakikisha raia wake hawadhulumiwi wakati wa utekelezaji wa amri hizi za kiutendaji.
Katika kipindi cha kampeni zake, Trump alijipatia umaarufu mkubwa miongoni mwa wafuasi wake kwa kuahidi sera kali za uhamiaji.
Ahadi zake zimewavutia Wamarekani wengi waliokuwa wakilalamikia ongezeko la wahamiaji haramu, lakini pia zimezua maswali mengi kuhusu haki za binadamu na utu.
Katika hatua ya kuonyesha msimamo wake, Trump amesisitiza kuwa utekelezaji wa amri hizi hautakuwa na huruma kwa wale wanaokiuka sheria za Marekani.
“Hatua hizi si dhidi ya mtu binafsi au jamii fulani, bali ni kuhusu kulinda Taifa letu na kuhakikisha usalama wa kila Mmarekani,” alisema Trump wakati wa hotuba yake ya kwanza akiwa Rais wa Marekani.
Huku utekelezaji wa amri hizi ukisubiriwa, ni wazi kuwa hatua za Trump zitakuwa na athari kubwa, si tu kwa wahamiaji, bali pia kwa uhusiano wa Marekani na mataifa mengine.
Hali ya wasiwasi inazidi kuongezeka miongoni mwa jumuiya za wahamiaji, ambazo sasa zinaishi kwa hofu ya kukamatwa na kufukuzwa.
Mabadiliko haya yanayotarajiwa chini ya uongozi wa Trump yanaonyesha jinsi sera za uhamiaji zinavyoweza kuwa na athari kubwa kwa maisha ya watu na uhusiano ya kimataifa.
Kwa sasa, dunia inasubiri kuona jinsi mambo yatakavyobadilika chini ya utawala mpya wa Rais Donald Trump.