Mapato ya ATCL yaongezeka

Muktasari:
Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, (PIC) imesema mapato ya Shirika la Ndege Nchini (ATCL), yameongezeka kutoka Sh58 bilioni mwaka 2018/2019 hadi kufikia Sh239 bilioni mwaka 2021/2022.
Dodoma. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, (PIC) imesema mapato ya Shirika la Ndege Nchini (ATCL), yameongezeka kutoka Sh58 bilioni mwaka 2018/2019 hadi kufikia Sh239 bilioni mwaka 2021/2022.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Septemba 5, 2022 na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Jerry Silaa mara baada ya kuchambua taarifa ya ATCL na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).
“Pia Shirika limekuwa likipata ongezeko la mapato kuanzia 2017/18 walipata Sh53 bilioni, 2018/19 Sh111 bilioni, 2019/20, Sh157 bilioni, mwaka 2020/21 ilipata Sh Sh174.5 bilioni na mwaka 2021/22 ilipata Sh239 bilioni,” amesema Silaa.
Amesema hasara ya shirika hilo imepungua kutoka Sh48 bilioni kwa mwaka fedha 2018/2019 hadi Sh27 bilioni kwa mwaka 2021/2022.
“Ukiangalia wanafanya vizuri na hasara imekuwa ikipungua walianza mwaka 2018/19 hasara ilikuwa Sh48 bilioni mwaka 2020/21 Sh36 bilioni, mwaka 2021/22 ilikuwa Sh27 bilioni,”amesema Silaa.
Pia amesema kila siti ya ndege inavyoingiza faida imeongezeka kutoka Sh251,000 kwa mwaka 2019/20 hadi Sh283,000 kwa mwaka 2020/21.
“Hesabu walizofunga 2020/21 wamefunga na faida ya Sh45 bilioni ikilinganishwa na Sh18 bilioni za mwaka uliotangulia,”amesema Silaa.
Kuhusu mtaji, Silaa ambaye pia ni mbunge wa Ukonga, amesema ATCL lina madeni makubwa kushinda mali zake.
Amesema kamati hiyo imeshauri Serikali kuharakisha mchakato wa kuhamisha umiliki wa ndege 11 kwenda ATCL ili shirika hilo liweze kuondokana na mtaji hasi.
Amesema ndege hizo 11 zina thamani ya Sh1.47 trilioni hivyo mali hizo zikihamishwa itasaidia kuondokana na kuwa na mtaji hasi na kukodisha kwa gharama kubwa.
“Mtaji hasi ni Sh239 bilioni yaani Shirika lina madeni makubwa kushinda mali zake na ndio eneo lililotajwa zaidi ya CAG akikabidhi ripoti yake,”amesema.