Maoni ya wadau nyongeza ya mshahara, kodi na elimu zatajwa

Muktasari:
- Mjadala kuhusu ongezeko la kima cha chini cha mshahara umeibua maoni tofauti, huku baadhi ya wadau wakiona faida kubwa katika ongezeko hili kwa ajili ya ustawi wa watumishi wa umma na uchumi kwa ujumla.
Dar es Salaam. Wadau wa sekta mbalimbali wameeleza maoni tofauti kuhusu ongezeko la kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma, lililotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Ongezeko hili la asilimia 35.1, ambalo litaanza kutumika Julai mwaka huu 2025, linatarajiwa kuleta mabadiliko katika maisha ya watumishi wa umma, huku wengine wakiunga mkono hatua hiyo na wengine wakipinga.
Katika mjadala wa Mwananchi X Space, ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), baadhi ya wadau walieleza kuwa ongezeko hili ni hatua muhimu kwa ustawi wa watumishi wa umma na jamii kwa ujumla, huku wengine wakitahadharisha athari za kifedha na kiuchumi zinazoweza kutokea.
Mchangiaji wa mjadala, Privatus Naikole, amesema ongezeko la mshahara kwa watumishi wa umma litachochea ukuaji wa uchumi na kusaidia kuondoa umaskini kwa jamii nzima.
Ameeleza kuwa, kwa wafanyakazi, ongezeko hilo litaongeza uwezo wao wa kifedha, na hivyo kusaidia kuinua uchumi wao.
Naikole amesema kwa nyongeza hiyo tija itakuwa kwa jamii yote, kwani mzunguko wa fedha utaongezeka, na kila mwananchi atafaidika.
Ametoa mfano wa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikubwa vilivyo karibu na makazi, akisema kuwa kipindi cha kupokea mikopo yao kinachangia kuongezeka kwa shughuli za biashara, na hivyo kusaidia kupunguza umaskini katika jamii.
"Wanaoishi jirani na vyuo, wanapata fedha vyuo vikifunguliwa, na hata bajaji na daladala wanapata faida kutokana na wanafunzi kupokea mikopo. Hali hii inachangia kuondoa umaskini," amesema.
Kuhusu watumishi wa umma, Naikole amesema kwamba ongezeko la mshahara litawapa morali na ari ya kufanya kazi, jambo linaloimarisha ufanisi na weledi katika utendaji wao.
Ameongeza kwamba, "kwa watumishi, ongezeko hili litachochea uchumi wao na kisaikolojia, na kuwapa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii na ufanisi zaidi."
Mchangiaji na mjasiriamali, Mbaruku Kanyama amesema ongezeko la mshahara litakuwa na tija kwa jamii kwa sababu litaongeza uwezo wa manunuzi wa watumishi wa umma, na hivyo kusaidia kuongeza mnyororo wa thamani kwa wajasiriamali, ikiwemo wafanyabiashara wadogo kama mama lishe.
Amesema: "Ongezeko la mshahara linaweza kuchochea uchumi, kwa kuwa watumishi wa umma watakuwa na uwezo mkubwa wa kununua bidhaa na huduma, jambo litakalosaidia kuongeza mahitaji sokoni."
Kwa upande wake mchangiaji Sady Chavara, akizungumzia nyongeza hiyo amesema ongezeko la mshahara linaweza kuwa na tija, ingawa amesisitiza kuwa mafanikio ya mtu hayawezi kupimwa kwa kiwango cha mshahara pekee.
"Ongezeko hilo litakuwa na tija kubwa, lakini mafanikio yanategemea zaidi tabia ya mtu na jinsi anavyotumia kile anachopokea.
“Hata mtu anayepokea mshahara wa Sh5 milioni anaweza kushindwa kufanikiwa, wakati mwingine mtu anayepokea milioni moja anaweza kuwa na mafanikio makubwa," amesema.
Makene Naluyaga ameeleza kuwa ongezeko la mshahara linaweza kutokuwa na tija endapo kiwango cha kodi ya mshahara kitaendelea kuwa kilekile.
"Endapo mshahara utaongezeka lakini kodi yake ikabaki vilevile, mtumishi wa umma ataona ongezeko hilo halileti faida kwa sababu atachukuliwa sehemu kubwa ya mshahara kama kodi, na hivyo pesa atakayopokea itakuwa ndogo kuliko alivyotarajia," amesema.
Kwa upande mwingine, Said Rashid ameeleza wasiwasi wake kuwa ongezeko la mshahara linaweza kupelekea kupanda kwa bei za bidhaa na huduma muhimu.
"Ongezeko hili linaweza kuwa na athari za moja kwa moja kwa mwananchi wa kawaida, kwani bidhaa, nauli, mafuta, na huduma nyingine za kijamii zinaweza kupanda bei kwa sababu ya ongezeko la mishahara," amesema.
Kwa upande wake mchangiaji Peter Kahindi, ameishauri Serikali kuboresha mfumo wa upangaji wa viwango vya mishahara kwa watumishi wa umma, akieleza kuwa mfumo wa sasa unawafaidi zaidi wale wenye elimu ya chini.
Kahindi amesema kuwa ongezeko la mshahara kwa watumishi wa shahada linakuwa dogo ukilinganisha na kwa wale wa ngazi za cheti, jambo ambalo linaweza kuwatia moyo wafanyakazi wa ngazi za chini tu na kuathiri ari ya watumishi wenye elimu ya juu.
Kwa upande mchangiaji mwingine, Mbaruku Kanyama amesema kwamba ongezeko la mshahara halina uhusiano wa moja kwa moja na kupanda kwa bei za bidhaa, akisisitiza kuwa bidhaa kama sukari na mafuta zinapanda kwa sababu ya uhitaji na upatikanaji wake sokoni, siyo kwa sababu ya ongezeko la mishahara.
Amesema bei za bidhaa zimekuwa zikiongezeka hata kabla ya ongezeko la mishahara na kwamba mshahara pekee hauwezi kuathiri bei za bidhaa.
Mchangiaji mwingine, Sady Chavara, ameeleza kuwa ongezeko la mishahara lililofanywa na Rais Samia litachochea mnyororo wa thamani katika sekta ya ujasiriamali, hasa kwa wafanyabiashara wadogo kama mama lishe.
Amesema ingawa ongezeko hilo litakuwa na tija, mafanikio ya kifedha ya mtu yatategemea tabia na matumizi yake, siyo kiwango cha mshahara anachopokea.
Yusuph Mohamed, kwa upande wake amesema kuwa matumizi yasiyo ya lazima ndiyo chanzo kikuu cha kumalizika kwa mshahara.
Ameeleza kuwa matumizi ndiyo yanayotofautisha watumishi wanaopokea mishahara midogo na wale wanaopokea mingi.
Mohamed amesema kuwa watu wanaopokea mishahara midogo mara nyingi wana mipangilio bora ya matumizi kulingana na kipato chao, tofauti na wale wanaopokea mishahara mikubwa ambao hutumia zaidi ya kipato chao.
Kwa upande wake mchangiaji Sai Teki, ameshauri Watanzania wapewe elimu ya uchumi ili waweze kutumia vyema ongezeko la mshahara na kulibadili kuwa na tija katika maisha yao.
Amesema baadhi ya watumishi, hususan walioko vijijini kama walimu, wanaongezewa majukumu bila kupewa rasilimali za kutosha, hali inayowalazimu kutumia mshahara mdogo kugharamia majukumu ya Serikali ikiwamo bando la kuwasilisha taarifa za kikazi kidijitali, jambo linalowadhoofisha kifedha.