Majaliwa ataka taasisi za fedha ziwaamini wachimbaji wadogo

Muktasari:
- Serikali imezindua mitambo na vifaa vya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo Tanzania na kuzitaka taasisi za kifedha kupanua wigo kwenye eneo hilo.
Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za fedha nchini kuwaamini wachimbaji wadogo kwa kuwapa mikopo ili waondokane na changamoto ya mitaji ambayo walikuwa wanaipata kutokana na kutegemea utabiri wa waganga wa kienyeji katika shughuli zao.
Majaliwa ameyasema hayo leo Jumanne, Juni 24, 2025, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mitambo ya wachimbaji wadogo na vitendea kazi vya Shirika la Madini Taifa (Stamico).
Kwa mara ya kwanza Oktoba 21, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mitambo mitano ya uchorongaji na vifaa vingine vyenye thamani ya Sh9.17 bilioni kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini.

Akizungumza Majaliwa amesema ni imani yake kuongezeka kwa mitambo na vifaa, kutaongeza mafanikio makubwa katika sekta ya madini kwa kuwezesha wachimbaji hao kupata taarifa za uhakika za jiolojia juu ya uwepo wa mashapo ya madini.
“Mitambo hii mipya itaongeza kasi ya uchimbaji wa uhakika na kuleta nafuu wa gharama za uchorongaji, hali itavutia wachimbaji wengi zaidi kuingia katika sekta ya madini kwa sababu sasa mnakwenda kufanya kazi yenye uhakika,”amesema.
Majaliwa amesema matumaini yake kupitia taarifa za jiolojia za uhakika wachimbaji wadogo wataweza kuaminika na kukopesheka na taasisi za fedha kwa ajili ya kukuza mitaji yao.
Ametoa wito kwa mabenki na taasisi nchini kwa mkakati wa Serikali wa kuwawezesha kuwafikia na kukopesheka, wapanue wigo na kufungua madirisha ya mikopo kwa ajili ya wachimbaji wadogo madini.

“Hii itaondoa changamoto ya muda mrefu ya wachimbaji wadogo kukosa mitaji na kutoaminika kwao sasa wachimbaji wadogo nchini Tanzania wanaaminika kwa sababu wanaweza kufanya kazi yao kwa uhakika,”amesema.
Aidha, Majaliwa amewaonya walengwa kutokwenda kutumia mitambo na vifaa kwa shughuli isiyokusudiwa kama kukodisha kuchimba mtaro na badala yake viende kwenye shughuli zilizokusudiwa kwa wachimbaji wadogo.
Kuhusu uchaguzi mkuu, Majaliwa ametahadharisha kuwa makini na ushawishi wa wagombea na vyama vya siasa wakati wanapofika kwao kuomba kura.
Ametaka wajiridhishe na ushawishi kabla ya kuupokea kwamba unalenga katika kuendeleza amani na utulivu ndani ya nchi.
“ushawishi wowote ambao unalugha ambayo haileti amani na utulivu huo ni wa kuepukana nao, nasema hili kwa sababu madhara ya lugha hizo mmeona kupitia vyombo vya habari kwa mataifa yaliyopoteza amani,”amesema.
Majaliwa amewataka kuamini kuwa uchaguzi mkuu, utakuwa wa uwazi, haki na amani.
Naye Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema Mkoa wa Dodoma kunajengwa viwanda vipya vitano kwa ajili ya kuchenjua madini ya metal yakiwemo shaba.
“Kusudi letu badala ya kulitoa jiwe la shaba nchini kwenda nje ya nchi (likiwa malighafi) sasa litachenjuliwa hapa Dodoma.Malengo yetu ni kuifanya Tanzania kuwa kinara wa uzalishaji wa bidhaa za shaba hasa copper ambayo sasa ina uhitaji mkubwa sana,”amesema.
Amesema sasa wanajenga Kiwanda cha Chumvi mkoani Lindi ambacho kitakamilika Agosti na kuanza kufanya kazi.
Pia wamesema wanajenga jengo mkoani Arusha kwa ajili ya kuchakata madini ya vito ikiwemo Tanzanite yaweze kuongezwa thamani na ifanyike hivyo na Watanzania.
Aidha, Mavunde amesema hadi kufikia leo sekta ya madini imeingiza katika Mfuko Mkuu wa Serikali Sh1.04 trilioni sawa na asilimia 100 ya malengo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Dk Venance Mwasse amesema uzinduzi huo ni mwendelezo wa Serikali katika kusaidia wachimbaji wadogo.
“Kwenye tukio hili kuna uzinduzi kwa ajili ya wachimbaji wadogo lakini pia kwa ajili ya Stamico ambapo vyote kwa ujumla wake vina thamani ya jumla ya Sh12.4 bilioni,”amesema.
Kuhusu mkaa wa mkaa rafiki Briquettes, Dk Mwasse amesema watagawa makotena nchi zima kwa kikundi cha Wanawake na Mama Samia kwa ajili ya kuuza mkaa huo unaozalishwa na shirika lake.
Pia, amesema wataingia mkataba ya mashirikiano kati ya shirika lake na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) kwenye maeneo ya matumizi wa mkaa huo katika vyuo vyote na kutoa mafunzo kwa kikundi cha Wanawake na Samia.
Rais wa Chama cha Wachimba Madini (Femata), John Bina amesema wachimbaji wa madini nchini Tanzania hivi sasa wanakaribia kuwa milioni saba ambapo wakulima na wafugaji nao wameanza kujishughulisha na shughuli hizo.

“Zamani wachimbaji walikuwa wakichimba kwa kuwasikiliza waganga wa kienyeji lakini leo mganga wa Kienyeji mkuwa ni Waziri wa Madini na Mkurugenzi wa Stamico sasa madini ni sayansi na biashara,”amesema Bina.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dk Mathayo David ameiomba Serikali kuendelea kutoa fedha kwa wakati kwa Wizara ya Madini kwa kadri zinavyotengwa na Bunge ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini Tanzania (Tawoma), Semeni Malale amesema kabla ya kupatiwa mashine mwaka 2023, walikuwa na uwezo wa kuponda kokoto wa mtu mmoja mifuko minne lakini sasa wanaweza kuponda mifuko kati ya 200 hadi 400 kwa siku.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mkoa huo una wachimbaji wadogo 3,215, wakubwa ni 11 na 200 wanafanya utafiti na kuwa vitachangia katika kuongeza ufanisi kwenye uchimbaji.