Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Mkuu awapa maagizo maofisa mikopo vyuoni

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu cha Waislamu MUM yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho leo Juni 20, 2025. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Wakati chuo kikuu cha waislamu MUM kikiazimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake viongozi mbalimbali wa kiislamu na Serikali wamemkumbuka na kumshukuru Rais mstaafu hayati Benjamin Mkapa kwa uamuzi wake akiwa Rais wa kutoa majengo yaliyokuwa chuo cha Tanesco na kuwapa waislamu kwa ajili ya kuanzisha chuo hicho.

Morogoro. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza maofisa wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu waliopo katika vyuo mbalimbali nchini kutoa elimu ya pamoja kwa wanafunzi kuhusu ujazaji sahihi wa fomu za mikopo kwa njia ya mtandao, badala ya kutoa maelezo kwa mtu mmoja mmoja.

Amesisitiza kuwa njia hiyo itaongeza ufanisi, kuokoa muda na kuwasaidia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo, Juni 20, wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Waislamu wa Mkoa wa Morogoro (MUM).

Amesema kuwa wapo baadhi ya wanafunzi wenye sifa za kupata mikopo ya elimu ya juu, lakini hukosa fursa hiyo kutokana na kukosea au kutokujaza fomu za mikopo kwa usahihi, hali inayowanyima nafasi ya kuendelea na masomo.

“Maafisa mikopo msisubiri mpaka mwanafunzi aje ofisini baada ya kukosa mkopo. Andaeni mhadhara kama huu wa leo, zungumzeni nao, muwaelekeze namna ya kujaza fomu kwa usahihi ili wapate mikopo,” amesema Majaliwa.

Pia, amesema mpango huo sasa unapanuliwa hadi kuboresha mazingira ya watoto wenye mahitaji maalum, akiwataka wazazi kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu na badala yake wawapeleke shule.

“Tunapeleka fedha kwenye halmashauri zote nchini kwa ajili ya kuwahudumia watoto wenye ulemavu. Mtoto mwenye ualbino apewe kofia, miwani, na mwenye ulemavu wa miguu apewe kiti mwendo. Hakuna mlemavu aliyepata elimu na kushindwa kufanya kazi,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya vyuo vikuu na kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu.

Amesema kutoka Sh464 bilioni mwaka 2021/22, bajeti imeongezeka hadi Sh787.4 bilioni kwa mwaka 2024/25.

Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Mussa Assad, amesema chuo kilipoanzishwa mwaka 2005 kilikuwa na programu mbili na wanafunzi 167, lakini sasa kina programu 32 na wanafunzi zaidi ya 5,000. Pia kipo katika maandalizi ya kuanzisha shahada za uzamivu na kampasi jijini Dar es Salaam ili kuongeza udahili.

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya MUM, Dk Ramadhani Dau, ameeleza kuwa moja ya changamoto ni uchache wa mabweni, hali inayowalazimu baadhi ya wanafunzi, hasa wa kike, kukodisha vyumba nje ya chuo.

Maadhimisho hayo pia yalihudhuriwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally, ambaye ametoa wito kwa Watanzania wote, Waislamu na wasiokuwa Waislamu, kusaidia chuo hicho kuendelea kutoa wataalamu na viongozi bora wa baadaye.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alizindua Mfuko wa Jamii wa Chuo Kikuu cha MUM (MUM Community Fund), ambapo alichangia Sh100 milioni, na akisoma salamu za Rais Samia Suluhu Hassan alisema ametoa mchango wa Sh100 milioni kwa ajili ya mfuko huo.

Mmoja wa wahitimu wa MUM, Mugini Singira, alimshukuru hayati Rais Benjamin Mkapa kwa kuwaruhusu kutumia majengo ya zamani ya Tanesco kuanzisha chuo hicho ambacho sasa kimetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.