Tume kukusanya data bidhaa za madini zinazoingizwa nchini

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akifungua jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, lililofanyika jijini Mwanza
Muktasari:
- Lengo ni kubaini bidhaa zinazohitajika zaidi migodini ili kuhamasisha uzalishaji wake hapa nchini.
Mwanza. Tume ya Madini inaendelea na mchakato wa ukusanyaji wa takwimu kuhusu bidhaa zote zinazoagizwa na migodi kutoka nje ya nchi.
Akizindua Jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, lililofanyika jijini Mwanza leo Juni 17, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema lengo ni kubaini bidhaa zinazohitajika zaidi migodini ili kuhamasisha uzalishaji wake hapa nchini.
"Nimeshaelekeza Tume ya Madini watuletee mipango ya manunuzi (procurement plans) ya migodi yote ili tujue ni bidhaa gani zinahitajika sana. Tukizifahamu, ni rahisi kwa watu wetu kuanza kujiandaa kupitia taasisi za kifedha na kuanza kuzalisha bidhaa hizo wenyewe," amesema Mavunde.
Amesema njia hiyo itaifanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma kwa migodi ya Afrika Mashariki, Kati, na hata nchi nyingine.
Amewaomba Watanzania wachangamkie fursa hiyo, akieleza kuwa endapo vifaa vya migodini vitaanza kuzalishwa nchini, manufaa yatakuwa makubwa kwa Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk Janet Lekashingo amesema takwimu zitakazokusanywa zitajumuisha mahali bidhaa zilipotokea, aina ya bidhaa hizo na gharama za manunuzi.
“Ni muhimu wafanyabiashara waanze kuwasiliana na viwanda hivyo ili kuingia ubia na kuanzisha uzalishaji hapa nchini. Bila takwimu huwezi kupanga jambo lolote kwa ufanisi,” amesema Dk Lekashingo.
Amebainisha kuwa kwa sasa ushiriki wa Watanzania katika sekta ya migodi umefikia wastani wa zaidi ya asilimia 75, lakini wengi bado ni wachuuzi.
"Sasa ni wakati wa kwenda hatua nyingine mbele kuwa wazalishaji, kuanzisha viwanda vya bidhaa zinazotumika migodini, nchini na hata kwa soko la kimataifa," amesema.
Ujanja wa teknolojia
Waziri Mavunde amefichua kuwa kumekuwepo na ujanjaujanja unaofanywa na baadhi ya wageni wanaoingia ubia na wazawa kwa jina tu, hali inayokwamisha uhamishaji wa teknolojia.

Baadhi ya washiriki waliohudhuria jukwaa la Nne la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, lililofanyika jijini Mwanza.
"Tulipotunga sheria na kanuni tulisema kuwa kwa huduma au bidhaa ambazo hazipatikani nchini kwa urahisi, kampuni kutoka nje inalazimika kuingia ubia na kampuni ya Kitanzania. Lakini sasa kuna ujanja kampuni ya uchimbaji inakwenda kuingia ubia na kampuni ya stationery (kampuni ya vifaa vya ofisini)," amesema Mavunde.
Amesema ujanja huo unavunja Kanuni ya 4(b) ya Sheria ya Madini, ambayo inasisitiza kuwajengea uwezo Watanzania kupitia ushiriki wa sekta binafsi.
“Naelekeza kanuni ya nane, kifungu kidogo cha sita, ifanyiwe marekebisho ili kuhakikisha yeyote anayekuja kufanya kazi nchini aingie ubia na kampuni yenye shughuli husika ili kuwe na uhamishaji halisi wa teknolojia, si maigizo,” ameagiza waziri huyo.
Amewataka wote wanaopata fursa za kutoa huduma migodini kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
“Kuna baadhi yenu si waaminifu, mnafanya kazi na kampuni zinazoheshimu viwango vya kimataifa. Hakuna ujanjaujanja kwenye sekta ya madini. Kama huwezi, tafuta kazi nyingine. Huku hakuna ujanjaujanja,” amesema.
Mavunde amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025, Wizara kupitia Tume ya Madini ilipokea na kupitia mipango 1,444 ya ushirikishwaji wa Watanzania, sawa na ongezeko la asilimia 80.27 ikilinganishwa na mipango 801 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita.
Awali, Kamishna wa Tume ya Madini na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania, Dk Theresia Numbi amesema jukwaa hilo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya sita kuhakikisha sekta ya madini inachangia ipasavyo katika pato la Taifa na inahusishwa na sekta nyingine za kiuchumi.
"Ushirikishwaji wa Watanzania unahakikisha vipaji, rasilimali na biashara zao zinashirikishwa kikamilifu katika mnyororo wa kuongeza thamani wa madini nchini. Huu si sera tu, bali ni mkakati wa ukuaji endelevu," amesema Dk Numbi.