Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikopo kausha damu ilivyowazindua bodaboda Dodoma

Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde akizungumza katika uzinduzi wa Chama cha Kuweka na Kukopa (Sacoss) cha waendesha bodaboda.

Muktasari:

  • Waendesha bodaboda na bajaji jijini Dodoma wameanzisha chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos) ikiwa ni hatua ya kupambana na mikopo kausha damu na umiza.

Dodoma. Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma (Umapido), Chacha Marwa amesimulia jinsi mikopo umiza, kausha damu ilivyosababisha waanzishe Chama cha Kuweka na Kukopoa (Sacoss).

Changamoto ya mikopo umiza, komandoo, pasua moyo, kichefuchefu, kausha damu imekuwa ikitajwa kuwa chanzo cha kufilisika, kujiua, kuvunjika kwa ndoa na kupata magonjwa ya akili baada ya wakopaji kushindwa kulipa kutokana na masharti magumu.

Tayari Serikali chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wamezindua mfumo mpya wa kifedha unaolenga kuondoa changamoto zinazowakabili watumiaji wa huduma za kifedha ikiwemo suala la mikopo umiza na kausha damu.

Akizungumza leo Jumanne, Juni 10, 2025 katika uzinduzi wa Saccos hiyo, Marwa amesema wazo la kuanzisha chama hicho lilianza mwaka 2017 lakini limekuja kufanikiwa 2025.

“Tumenuia kwamba mikopo ilikuwa inatuumiza, inaitwa kaushadamu. Mheshimiwa mgeni rasmi nikwambie hakuna watu wanakopa kama maofisa usafirishaji (bodaboda) na kausha damu inatutesa  kweli,”amesema.

“Unakopa laki moja unarudisha laki tatu hivi kweli ni haki. Mimi nikasema siwezi kuongoza chama cha namna hii, watu wanamalizwa na kausha damu. Nikasema tunaweza tukaanzisha Saccos,”amesema.

Baadhi ya waendesha bodaboda walioandamana kabla ya uzinduzi wa Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos).

Amesema waliamua kuanza na kidogo walichonacho na leo hii wanazindua wakiwa na zaidi ya Sh11 milioni.

Amesema mikopo hiyo itawapa nafasi waendesha bodaboda hao kununua pikipiki na bajaji zao wenyewe badala ya kuendesha za watu.

Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, amewataka waendesha bodaboda kutumia fursa hiyo kwa kujiunga na chama hicho ili waweze kumiliki vyombo vyao vya moto.

“"Naomba nitoe rai kwa wasiokuwa wanachama kuitumia fursa hii ya kujiunga lengo tunataka muendeshe bodaboda zenu na lengo sio kausha damu bali kuwaongezea damu na hili mimi nitalisimamia kwa nguvu zangu zote, nataka kuwainua kiuchumi," amesema Mavunde.

Mavunde amesema pia ameliomba Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya Udhibiti Ardhi (Latra) kuwa karibu na  bodaboda ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kuacha kuwakamata bila sababu za msingi.

"Nawaomba Polisi muwafanye hawa marafiki zenu natamani kuona ofisa usafirishaji akimuona askari asimkimbie amuone rafiki yake,"amesema Mavunde na kushangiliwa na bodaboda hao.

Aidha, Mavunde amechangia Sh10 milioni kama mtaji kwa Saccos hiyo na kujenga ukuta wa ofisi ya chama hicho iliyopo Kata ya Makole jijini Dodoma.

Naye Meneja wa Benki ya Taifa ya Ushirika (COOP Bank),Yahaya Kiyabo amesema kupitia benki hiyo kuna fursa mbalimbali wamewapatia bodaboda.

Amezitaja fursa hizo kuwa  pamoja na huduma ya kufungua akaunti ambapo kuna akaunti maalumu kwa bodaboda kwa kulipa Sh5,000 na anapewa zawadi ya fulana na lita tatu za mafuta.

Amesema anayefungua akaunti  ikitokea amefariki dunia wanatoa mkono wa pole usiopungua Sh1 milioni na huduma ya bima kubwa na ndogo.

"Tumekubaliana kuwapatia bima ya afya na mchakato unaendelea lengo ni kuhakikisha ofisa usafirishaji anafanya kazi yake bila changamoto yoyote," amesema Kiyabo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amewataka wasafirishaji hao kuwa makini kwenye uendeshaji wao kwa kuyapenda maisha yao na kuchukua tahadhari.

 “Mtusaidie kuchukua tahadhari. Kesho utachukua mkopo kupitia Saccos utakuwa na bodaboda ya kwako, hesabu ni ya kwako mwenyewe unaendesha kukimbilia wapi? Uwepo wa Saccos hii ni hatua muhimu ya kupunguza ajali za barabarani na harakaharaka za maofisa usafirishaji,”amesema.

Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amewataka bodaboda  kutii  sheria bila shuruti ambapo amedai  hakuna sababu ya kuanza kukimbizana kwani wote ni ndugu.

"Nawaomba mtoe taarifa za uhalifu na wahalifu, msijihusishe na uhalifu, tuendelee kudumisha amani tuache kufanya vurugu,"amesema Kamanda Katabazi.