Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yasaini mkataba wa kihistoria kuongeza akiba ya dhahabu

Dodoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesaini mkataba na kampuni kubwa za uchimbaji dhahabu pamoja na Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Geita (GGR) ili kurahisisha ununuzi na usafirishaji wa dhahabu ndani ya nchi.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha akiba ya fedha za kigeni nchini.

Kampuni zilizohusishwa katika mkataba huo ni Geita Gold Mining (GGM), Shanta Gold, Buckreef Gold na Geita Gold Refinery (GGR).

Uamuzi huo umekuja wakati BoT ikiongeza kasi ya kununua dhahabu kutoka soko la ndani kwa ajili ya kukuza akiba ya taifa ya fedha za kigeni.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika leo Jumatatu Juni 16, 2025 jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema ununuzi wa dhahabu husaidia kuongeza akiba ya fedha za kigeni.

Hivyo amewataka wasafishaji wa ndani kuongeza uwezo wa uzalishaji na kufikia viwango vya kimataifa vinavyohitajika ili kupata ithibati kutoka Chama cha Soko la Dhahabu la London (LBMA).

“Ithibati kutoka LBMA itaongeza uaminifu wa dhahabu ya Tanzania katika masoko ya kimataifa na kuiwezesha kuuzwa kwenye masoko ya kifedha ya kimataifa,” amesema Dk Nchemba.

Amesema dhahabu inayotakiwa kutambulika kimataifa na kukubalika na benki kuu na taasisi za kifedha, lazima isafishwe kwa ubora wa juu na ithibitishwe na taasisi zinazoaminika kama Benki ya England.

Hivi sasa, dhahabu ya Tanzania inapelekwa nje kwa ajili ya kuthibitishwa kupitia mpango wa kubadilishana dhahabu.

Dk Nchemba amesema mkataba huo umezingatia Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, kinachowataka wachimbaji kuuza asilimia 20 ya dhahabu yao kwenye soko la ndani, likiwemo BoT ambayo ina haki ya kununua kwanza.

“Hatua hii itaunga mkono mpango wa BoT wa ununuzi wa dhahabu na kusaidia wasafishaji wa ndani kupata ithibati ya LBMA,” amesema Dk Nchemba.

Amekiri kuwepo kwa changamoto za kisheria na kikodi katika ununuzi wa dhahabu, zikiwamo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye huduma za usafishaji na changamoto za kuihifadhi dhahabu nje ya nchi, akiahidi kuwa serikali itayashughulikia kwa mujibu wa sheria.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema mktaba huo ni sehemu ya juhudi pana za kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje na kukuza uhuru wa kifedha kwa kutumia utajiri wa madini uliopo nchini.

Amesema BoT imevuka lengo lake la ununuzi wa dhahabu kwa mwaka wa fedha 2024/25, baada ya kununua tani 5.022 zenye thamani ya dola milioni 554 (Sh1.5 trilioni) hadi Juni 13, dhidi ya lengo la dola milioni 350 (Sh949.5 bilioni).

“Dhahabu imenunuliwa kwa bei shindani kutoka kwa wasafishaji watatu wa ndani bila malalamiko yoyote. Malipo hufanyika ndani ya saa 24 baada ya ununuzi,” amesema Gavana Tutuba.

Ameongeza kuwa kilo 162 za dhahabu zimehifadhiwa kwenye akaunti ya Tanzania katika Benki ya England, kilo 2,775 ziko katika tawi la BoT Mwanza na kilo 719 ziko katika tawi la Dodoma, huku dhahabu nyingine ikitarajiwa kusafirishwa kwenda nje kwa ajili ya uthibitisho.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Amesema mchango wa madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 9 mwaka 2015 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024/25, huku mapato ya serikali kutoka sekta hiyo yakipanda kutoka Sh162 bilioni hadi Sh753 bilioni na matarajio ni kufikia Sh1 trilioni.

“Ingawa mazungumzo ya awali na wachimbaji yalikuwa magumu, marekebisho ya Sheria ya Madini na kuanzishwa kwa kifungu cha asilimia 20 ya mauzo kwa BoT kumeleta utekelezaji rahisi,” amesema waziri huyo.

Amesisitiza dhamira ya serikali ni kuendeleza uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi, akibainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina viwanda vya usafishaji dhahabu vinane na akahamasisha wawekezaji wengine kujiunga.

Kwa mujibu wa wataalamu wa sekta, ithibati ya LBMA itasaidia kufungua fursa za dhahabu ya Tanzania kuingia katika masoko ya kifedha ya kimataifa hususan kwa wachimbaji wadogo ambao watapata bei nzuri zaidi ikiwa dhahabu yao itakidhi viwango vya kimataifa.

Ingawa dhahabu ya Tanzania husafishwa kwa ubora wa asilimia 99.99, utambuzi wa kimataifa unahitaji mhuri rasmi wa ithibati, ambao kwa sasa hupatikana kupitia taasisi kama Benki ya England.

Kupitia mpango wa kubadilishana dhahabu, Tanzania hupeleka dhahabu iliyosafishwa nje na kupokea dhahabu yenye ithibati rasmi kwa malipo ya gharama ya huduma hiyo, jambo linalosaidia nchi kuendelea kujenga akiba ya kimataifa, huku ikiendeleza sekta ya usafishaji ndani ya nchi.