Wafanyabiashara wataja chanzo utoroshaji wa madini

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye uzinduzi wa maonyesho na kongamano la madini linalotarajiwa kufanyika mkoani humo kwa muda wa siku nne. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Mei 23 mwaka huu, almasi yenye thamani ya zaidi ya Sh1.7 bilioni ilikamatwa ikitoroshwa nje kupitia uwanja wa ndege wa Mwanza.
Musoma. Baadhi ya wafanyabiashara na wachimbaji wa madini mkoani Mara wametaja utitiri wa kodi kuwa sababu ya baadhi ya wenzao kutorosha madini kwenda nje ya nchi, huku wakiiomba Serikali kuondoa changamoto hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na wafanyabiashara hao, Jumatano Juni 4, 2025, wakati wakizungumza na Mwananchi nje ya kongamano na maonyesho ya madini linaloendelea mjini Musoma.
Wamesema kuwa tozo nyingi katika biashara ya madini zimekuwa kikwazo kwao na kuwashawishi baadhi ya wachimbaji kutafuta njia zisizo halali ili wapate faida.
Miongoni mwa tozo wanazolalamikia ni pamoja na asilimia 2 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), asilimia 0.3 ya ushuru wa huduma, asilimia 1 ya ukaguzi na asilimia 7 ya Serikali.
"Kwanza niseme kutorosha madini kwenda nje ya nchi kunafanywa na wale wasio wazalendo na ni jambo ambalo halikubaliki, lakini nafikiri Serikali inapaswa kuangalia kwa nini vitendo hivyo vinaendelea," amesema Wambura Mseti.
Mseti amesema kuwa ingawa Serikali imejitahidi kuboresha sekta ya madini, bado kuna changamoto, hasa tozo nyingi, ambazo zimekuwa kikwazo kwao, na hivyo umefika wakati Serikali ifanyie kazi mapendekezo yao ya kupunguza baadhi ya tozo hizo.
"Mfano sisi hapa tupo mpakani. Tukiangalia mazingira ya biashara kwa wenzetu ni tofauti sana na ya kwetu. Wao hawana hizi kodi nyingi, nafikiri ndiyo maana baadhi ya wenzetu hushawishika kutorosha madini kwa njia za panya," amesema Masubo Paulo.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wakicheza wakati wa uzinduzi wa kongamano na maonyesho ya madini mkoani Mara. Picha na Beldina Nyakeke
Amesema hakuna sababu ya kuwepo tozo nyingi kwenye biashara moja, ilhali mapato yote yanaishia serikalini. Alipendekeza kuwepo na tozo moja inayotozwa na Serikali kwa gharama nafuu ili kuwaondolea mzigo wachimbaji.
"Kuna asilimia ya Serikali, asilimia ya TRA, ushuru wa huduma na vingine vingi. Ukiangalia, mhusika mkuu ni yuleyule — Serikali. Sisi hatukatai kulipa kodi, tuko tayari, kwani tunajua faida zake kwa uchumi wa nchi yetu. Lakini kodi hiyo itufanyie ahueni na nasi tupate faida," amesema Paulo.
Kwa upande wake, Anna Mtatiro amewataka wachimbaji kutotumia utitiri wa tozo kama kigezo cha kutorosha madini, akieleza kuwa kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi wa nchi.
"Tuendelee kufanya mazungumzo na Serikali ili ituboreshee mazingira ya biashara. Wakati huo huo, tufanye biashara kwa mujibu wa sheria na taratibu. Tuache hizi tabia za kutorosha madini. Tufanye biashara halali huku tukipaza sauti kuhusu changamoto tulizo nazo," amesema.
Mfanyabiashara mwingine, Chogero Maro, amesema madai yao hayahusiani na wale wanaotorosha madini, na kuongeza kuwa yeyote anayekwenda kinyume na taratibu anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
"Kwanza tunatakiwa kuwa wamoja. Hakuna sababu ya wengine kuomba mazingira bora ya biashara wakati wengine wapo ‘bize’ kutorosha madini. Ni vema sote tukaunganisha nguvu kudai mazingira rafiki ili sote tunufaike. Huo ndiyo uzalendo," amesema Maro.
Licha ya malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema Serikali haitasita kumfutia leseni mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutorosha madini.
Amesema Serikali imeboresha mazingira ya sekta ya madini ili kuongeza mnyororo wa thamani, ikiwa ni pamoja na kufungua masoko ya uhakika yenye bei nzuri kwa wafanyabiashara wa madini.
Akifungua maonyesho ya madini yanayotarajiwa kufanyika kwa siku nne, Kanali Mtambi amesema anatamani kuwaona mabilionea wakitokea Mara kupitia sekta hiyo, ikiwa wachimbaji watafuata sheria na taratibu.
"Tunaboresha mazingira ya sekta hii. Mbali na masoko, tunataka tuchimbe kisayansi na kitaalamu zaidi. Kuna mitambo ya kuchoronga madini, wapo wataalamu wanaofanya utafiti kujua wapi pana madini na kiasi chake. Natoa wito kwa yeyote anayetaka kuwekeza kwenye sekta hii aje, tuko tayari," amesema.
Ameongeza kuwa wachimbaji wadogo ndio muda wao wa kufanya kazi, na Serikali ipo pamoja nao ili kuwawezesha kukua kutoka uchimbaji mdogo hadi wa kati, na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa.
Maonyesho hayo yameambatana na mafunzo juu ya teknolojia mbalimbali katika mchakato mzima wa uzalishaji wa dhahabu, na kutangaza fursa za uwekezaji kupitia sekta hiyo ndani ya Mkoa wa Mara.