RC Mtambi: Achaneni na imani za kishirikina machimboni

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma juu ya maonyesho ya kwanza ya madini yanayotarajiwa kufanyika mkoani humo kwa muda wa siku nne. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- RC Mtambi ametoa agizo hilo leo Jumatatu Juni 2, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano na maonyesho ya madini yanayotarajiwa kufanyika mkoani Mara kwa siku nne kuanzia kesho.
Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewataka wachimbaji wa madini hasa wadogo kuepuka kufanya shughuli zao kwa kutegemea imani za kishirikina badala yake wafanye kisayansi na teknolojia ili kupata tija zaidi.
Kanali Mtambi ametoa agizo hilo leo Jumatatu Juni 2, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano na maonyesho ya madini yanayotarajiwa kufanyika mkoani Mara kwa siku nne kuanzia kesho.
Mtambi amesema hakuna sababu ya wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa kubahatisha kwa kuwa, kulingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia mambo mengi hasa yanayohusu uchimbaji yamerahisishwa, hivyo wachimbaji hao wanapaswa kutumia utaalamu huo ili kuboresha shughuli zao.
"Dhana potofu zilizopitwa na wakati kwamba mganga ana uwezo wa kumsaidia mchimbaji kupata madini kama ingekuwa kweli basi huko kwenye machimbo kungejaa hao waganga, niwaase wachimbaji waachane na mambo haya wafanye mambo kisayansi bahati nzuri Serikali pia imewekeza nguvu nyingi kwenye sekta ya madini, hivyo uwekezaji huu basi ulete tija," amesema.
Kuhusu maonyesho hayo ya kwanza kufanyika mkoani Mara, Kanali Mtambi amesema zaidi ya washiriki 5,000 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki huku lengo likiwa ni kutangaza fursa za uwekezaji kupitia sekta ya madini mkoani Mara.
Amesema Mkoa wa Mara una madini mengi ambayo bado hayajatumika vema kuimarisha uchumi wa mkoa na watu wake, hivyo Serikali ipo haja ya kuandaa maonyesho hayo ili kuwavutia wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika sekta hiyo.
Amefafanua kuwa, wakati wa maonyesho hayo kutakuwa na mafunzo kwa wachimbaji wadogo juu ya uchimbaji wa kisasa wenye tija na namna ya kutumia fursa zilizopo kuboresha uchumi wao na wa mkoa.
"Kwa sasa pato la mkoa wetu ni Sh6 trilioni na kwenye pato hili sekta ya madini inachangia asilimia 18 lakini tunaamini kuwa, baada ya maonyesho haya na fursa zilizopo zikitumika vizuri mchango wa sekta ya madini katika pato la mkoa utakuwa zaidi ya hapo," amefafanua.
Baadhi ya wakazi wa Musoma wameipongeza Serikali kwa uamuzi wa kuandaa maonyesho hayo yatakayosaidia kuboresha uchumi wa mkoa kupitia sekta ya madini.
"Kuna watu hawajui namna gani wafanye ili waweze kutumia fursa ya uwepo wa madini kwenye mkoa wetu kwa hiyo, kupitia kongamano hilo wengi watapata uelewa wa nini kifanyike ili watumie fursa zilizopo," amesema Josiah Musa.
Mkazi mwingine, Imani Opanga amesema kongamano hilo pia litasaidia kuondokana na imani za kishirikina kwa wachimbaji wadogo kwani upo uwezekano kuwa baadhi yao wachimbaji wanafanya shughuli zao kwa imani hizo kutokana na kutokuwa na uelewa juu ya uchimbaji wa kisasa na kisayansi.
"Tunaambiwa kwa sasa kuna vifaa vinaweza kutumika kupima na kubaini madini yapo sehemu gani na kwa kiasi gani, kwa hiyo wachimbaji wakipata elimu ya kutosha juu ya vifaa hivyo na namna wanavyoweza kuvipata basi ni dhahiri kuwa wataanza kutumia njia hizo za kisasa," amesema Sadiki Mohamed.