Tanzania moja ya nchi 10 zinazohifadhi dhahabu nyingi Benki Kuu

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (mwenye shati jeusi) akiwa na viongozi wengine wakiongoza maandamano ya wachimbaji wadogo mjini Musoma ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya madini nchini. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Tanzania imefanikiwa kununua na kuhifadhi tani 3.7 za dhahabu katika kipindi cha miezi minane iliyopita.
Musoma. Tanzania imeingia kwenye orodha ya nchi 10 Afrika zenye akiba nyingi ya dhahabu zinazohifadhiwa katika benki kuu za nchi hizo baada ya kufanikiwa kununua na kuhifadhi tani 3.7 za dhahabu.
Kiasi hicho cha dhahabu kimenunuliwa ndani ya miezi minane iliyopita kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini, kifungu cha 59 ambapo pamoja na mambo mengine kimeelekeza wafanyabiashara wakubwa wa dhahabu kutenga asilimia 20 ya dhahabu na kuiuzia Benki Kuu Tanzania (BoT).
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Juni 6, 2025 mjini Musoma na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akihitimisha kongamano na maonyesho ya madini ambapo amesema ununuzi wa kiasi hicho cha dhahabu ni moja ya mipango mikakati ya Serikali katika kuboresha sekta ya madini ili kuinua uchumi wa nchi na watu wake.
Mavunde amesema, awali, Tanzania licha ya kuwa miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu, haikuwa na akiba ya kutosha ya dhahabu Benki Kuu.
“Sisi ni miongoni mwa nchi tano zinazozalisha dhahabu kwa wingi Afrika lakini tulikuwa tunakabiliwa na changamoto kubwa ya uhifadhi wa dhahabu benki kuu kwani hatukuwa hata kwenye kumi bora, nchi ya kwanza ilikuwa ni Algeria yenye tani 174 na ya kumi ilikiwa ni Msumbiji iliyokuwa na tani tatu,” amesema Mavunde.
Amesema ununuzi na uhifadhi wa dhahabu benki kuu ni suala endelevu na kwamba suala hilo litaendelea kufanyika kwa weledi hasa ikizigatiwa kuwa lina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Mavunde amesema Serikali ina mipango mikikakati mingi inayolenga kuboresha sekta ya madini nchini mipango ambayo itasaidia kuifanya sekta hiyo kuwa kinara katika kuchangia pato la Taifa na wananchi kwa ujumla.
Amesema mipango hiyo inahusisha kuboresha mazingira ya sekta ya madini madini wa ili kuwa na mnyororo wa thamani utakaonufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Waziri huyo amesema tayari mafanikio yameanza kuonekana ikiwa ni pamoja na ongezeko la mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa kutoka Sh162 bilioni mwaka 2015/16 hadi kufika Sh960 bilioni Mei, mwaka huu.
“Mapato yameongezeka kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ambapo pamoja na mambo mengine, hivi sasa tuna masoko 45 na vituo 109 vya kununua dhahabu na niwaambie tu kuwa asilimia 40 ya mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa linatokana na wachimbaji wadogo,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili shughuli zao ziweze kuwa na tija ambapo amepiga marufuku wamiliki wa leseni kutowaingiza wachimbaji wadogo kwenye maeneo yao isipokuwa kwa mikataba maalumu.
“Leseni sio mapambo kama mmiliki wa leseni ambaye uchimbaji wa maduara katika eneo lake lazima aingie mkataba kutoka ofisi ya madini ili ikitokea umepata mwekezaji hawa wenye maduara walipwe fidia kwa mujibu wa mikataba, sheria haiwatambui wenye maduara lakini hatuwezi kuwaacha hivi hivi, lazima tuwasaidie,” amesema Mavunde.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema mkoa huo unajipanga kuwa mkoa wa kwanza kwa uzalishaji wa madini nchini kutoka nafasi ya pili kwa sasa.
Amesema uwezo wa mkoa huo kufanya mapinduzi hayo upo kwani tafiti zinaonyesha mkoa huo una madini mengi hasa dhahabu lakini bado hayajachimbwa vema kutokanana changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa mbinu za uchimbaji wa kisasa na kisayansi.
Amesema maonyesho na kongamano hilo lililofanyika kwa mara ya kwanza mkoani humo ni moja ya mikakati ya kufanya mapinduzi katika sekta ya madini mkoani humo kwani wachimbaji na wadau wameweza kupata elimu juu ya matumizi sahihi ya teknlojia na namna ya kufikia teknlojia hizo.
“Kwa sasa sekta hii inachangia asilimia 18 ya pato la mkoa lakini tumejiwekea malengo kuwa miaka mitatu ijayo, sekta hii itakuwa inachangia zaidi ya asilimia 40 kwenye pato la mkoa wetu,” amesema.
Akitoa taarifa ya sekta ya madini mkoani Mara, Ofisa Madini Mkazi, Amini Msuya amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita jumla ya tani 58.9 ya dhahabu zenye thamani ya zaidi ya Sh6.9 zimezalishwa.
Amesema katika kipindi hicho pia jumla ya leseni 2,288 zimetolewa kwa wachimbaji wa madini ambapo kati ya hizo leseni 1,751 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo.
“Katika kipindi hicho pia serikali imekusanya zaidi ya Sh568.5 bilioni ambazo zimetokana na malipo mbalimbali kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza sekta ya madini ambapo kwa mwaka huu wa fedha tulipewa malengo ya kukusanya Sh176.3 ambapo hadi sasa tumekusanya Sh173.5 bilioni na tunaamini tutavuka malengo,” amesema.
Msuya ameongeza kuwa katika kipindi hicho, pia, jumla ya miradi 398 ya maendeleo ya jamii yenye thamani ya zaidi ya Sh33.8 bilioni imetekelezwa kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji, John Binna amewataka wachimbaji wadogo kuhakikisha wanaboresha shughuli zao ili kumiliki uchumi kupitia sekta ya madini kwa maelezo kuwa changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili hapo awali zimetatuliwa na Serikali.
Binna amesema umefika muda sasa wachimbaji hao wanatakiwa kubadili fikra na mawazo yao na kufikiri namna ya kuhama kutoka kuwa wachimbaji wadogo na kuwa wachimbaji wa kati na wakubwa kwani kwa sasa mazingira yao ya ufanyaji kazi yameboreshwa kwa kiasi kikubwa.
Amewataka wachimbaji hao kuachana na migogoro badala yake waelekeze nguvu katika kutumia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini kwa maelezo kuwa kwa muda mrefu wameshindwa kupata mafanikio kupitia sekta hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo migogoro.
“Tujipange kumiliki uchumi kupitia madini,tuache migogoro, serikali imefanya makubwa sana katika kuboresha sekta hii sasa kazi kwetu tutumie fursa hii hasa ikizingatiwa kuwa tulipeleka mapendekezo 22 kwa Rais ili kuboresha sekta hii na amepitisha mapendekezo 19,” amesema.
Katika hitimisho hilo, wachimbaji wadogo wamefanya maandamano ya amani ikiwa ni sehemu ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoboresha sekta ya madini nchini.