Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BoT yaja na mfumo wa kukomesha mikopo umiza

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza katika uzinduzi wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya wateja wa huduma za fedha na mazingira ya majaribio ya teknolojia ya fedha, jijini Dodoma. Picha na Sharon Sauwa.

Muktasari:

  • Mfumo wa fedha uliozinduliwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba utasaidia kutatua changamoto ya mikopo yenye masharti kandamizi

Dodoma. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amezindua mfumo mpya wa kifedha unaolenga kushughulikia na kutokomeza changamoto zinazowakabili watumiaji wa huduma hizo ikiwamo suala la mikopo umiza na kausha damu.

Mfumo huo umetajwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha kunakuwapo na uwazi, uadilifu na ulinzi kwa wateja wa huduma za kifedha, hususan wale wanaoathirika na masharti kandamizi ya mikopo kutoka kwa taasisi zisizosimamiwa ipasavyo.

Changamoto za mikopo yenye masharti kandamizi, maarufu kama mikopo umiza, komandoo, pasua moyo, kichefuchefu na kausha damu, zimekuwa zikitajwa kama chanzo cha matatizo mbalimbali ya kijamii ikiwamo watu kufilisika, kujiua, ndoa kuvunjika na hata kuathirika kisaikolojia, kutokana na wakopaji kushindwa kumudu masharti yake magumu.

Uzinduzi wa mfumo mpya wa kushughulikia changamoto hizo umefanyika leo, Alhamisi Juni 5, 2025, jijini Dodoma.

Mfumo huo unajumuisha mazingira ya majaribio ya teknolojia ya fedha pamoja na mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha, uliopewa jina la Sema na Benki Kuu.

Mfumo huo unalenga kulinda haki za wateja, kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi katika sekta ya fedha.

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Dk Mwigulu amesema Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2020/21 hadi 2025/26 pamoja na mpango mkakati wa uchumi wa kidijitali wa Tanzania, unatilia mkazo umuhimu wa uchumi unaojumuisha sekta mbalimbali huku uchumi wa kidijitali ukichukua nafasi muhimu.

Amesema kupitia mfumo wa mazingira ya majaribio ya fedha  wanakusudia kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano miongoni mwa nchi zinazoendelea katika ubunifu wa teknolojia na masuala ya fedha, kwa kuweka mazingira yanayovutia uwekezaji wa kurudia na kuwapa uwezo vijana kushiriki katika kukuza uchumi.

Kwa upande wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha, mfumo utatoa fursa maalumu katika kutatua malalamiko ya utumiaji wa huduma za kifedha kwa ufanisi na uwazi.

“Naamini kwamba mfumo huu utakuwa suluhisho la malalamiko mbalimbali ambayo tumekuwa tukiyasikia ikiwamo mikopo umiza. Jambo ambalo litaongeza imani ya umma katika kutumia huduma rasmi za fedha na kuboresha uwajibikaji kwa watoa huduma za fedha wanaosimamiwa na Benki Kuu,” amesema.

Amesema wengi wanaingia katika changamoto ya mikopo umiza, wanaingia katika taratibu huo kwa kuangalia urahisi wa kupata fedha bila kujali changamoto wanazoweza kuzipata kutokana mikopo hiyo.

“Watu wanaingia (katika mikopo), ndani ya miezi mitatu unatakiwa urudishe zaidi ya mara tatu, umefanya kitu gani? Yaani kwenye maisha yako umepambana kupata Sh2 milioni, Sh1 milioni mpaka ukaona ukakope, halafu katika kukopa unakubali kupewa kwa sharti la kwamba ndani ya mwezi mmoja urudishe,” amesema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Emmanuel Tutuba amesema ni ukweli usiopingika licha ya juhudi nzuri za kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha hapa nchini bado kuna changamoto mbalimbali.

“Baadhi ya changamoto hizo ni kutokuwa na mazingira rafiki kwa ukuaji wa teknolojia na ubunifu katika mifumo ya utoaji wa huduma rasmi,” amesema.

Changamoto nyingine ni idadi kubwa ya watoa huduma wasiokuwa rasmi, kiwango cha chini cha elimu ya fedha kwa watumiaji mbalimbali hapa nchini na uhusiano hafifu baina ya watoaji na watumiaji wa huduma rasmi za kifedha nchini.

Tutuba amesema BoT kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la watumiaji jumuishi wa huduma za  fedha limechukua hatua ambazo zimewezesha kuzinduliwa kwa mifumo hiyo.

Tutuba amesema mifumo hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma za kifedha nchini na kukuza matumizi ya teknolojia ya fedha na kumlinda mtumiaji wa huduma rasmi za fedha.

Amesema hatua hiyo itaongeza uwajibikaji na kuchochea matumizi ya huduma jumuishi za fedha zenye ubora, usalama na kwa gharama nafuu na mifumo hiyo inadhibiti utakatishaji wa fedha haramu.

Kuhusu mfumo wa kushughulikia malalamiko, Tutuba amesema Benki Kuu imeanzisha mfumo huo kama sehemu ya jitihada za kuhakikisha usalama, ufanisi na uwazi kwa watumiaji wa huduma za kifedha nchini.

Ameeleza kuwa mfumo huo uitwao, "Sema na Benki Kuu," utawapa wananchi fursa ya kuwasilisha malalamiko yao moja kwa moja dhidi ya huduma mbalimbali za kifedha, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha ulinzi wa watumiaji na kuongeza uwajibikaji kwa taasisi za fedha.

“Mfumo wa Sema na Benki kuu utamwezesha kila mtumiaji wa huduma za fedha kufikia na kutumia wakati wote bila kujali mahali alipo na kutuwezesha pia, kuchukua hatua stahiki ili kuongeza ujumuishi wa huduma za kifedha hapa nchini,”amesema Tutuba.

Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo amesema mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha utaongeza ufanisi na uwazi katika kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma hizo ili kuongeza imani.

Amesema mfumo huo umeangalia watu wa aina zote na kueleza kuwa jitihada hizo za BoT zitachochea ustawi na ujumuishi wa huduma za fedha ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kitaifa wa huduma jumuishi za fedha ulioanza kutekelezwa mwaka 2023.


Hoja ya Bunge

Kufuatia hali hiyo, Bunge lilitoa agizo kwa Serikali kuwabana wakopeshaji wanaootuma ujumbe kwa ndugu, jamaa na marafiki wa mtu waliyemkopesha kwa lengo la kumdhalilisha.

Pia, limeeleza mikopo hiyo imekuwa chanzo cha mateso kwa wananchi, hususan wa kipato cha chini.

Kwa mujibu wa wabunge mikopo hiyo imekuwa ikiambatana na riba kubwa isiyoelezeka, masharti ya unyonyaji, pamoja na mbinu za kukusanya madeni zinazohusisha vitisho, udhalilishaji, uporaji wa mali na hata vipigo kutoka kwa baadhi ya mawakala wa taasisi hizo.

Wabunge wamesema  kuna wananchi ambao wamepoteza amani, wengine wameuza vitu vyao vya msingi kama friji, TV na hata vifaa vya shule vya watoto.

Kuna waliopigwa, waliofilisika na kuna waliokata tamaa kabisa ya maisha kwa sababu ya mikopo hii ya kinyonyaji.

Hata hivyo, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson ameeleza kuwa, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha haki za watumiaji wa huduma za kifedha zinalindwa na kwamba udhibiti wa sekta ya mikopo unapaswa kuimarishwa kupitia sera, sheria na mifumo madhubuti ya usimamizi.