Prime
Mahakama yapokea picha za CCTV mauaji mfanyakazi GGM

Wananchi wa Mtaa wa Mwatulole mjini Geita wakiangalia eneo ambalo mwili wa Milembe Suleman ulikutwa.
Muktasari:
- Milembe (43), aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha ugavi GGML aliuawa usiku wa kuamkia Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili.
Geita. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita imepokea picha za mjongeo (video) zilizonaswa na kamera maalumu za usalama (CCTV) kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Geita(GGM), Milembe Seleman.
Picha hizo zimewasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi kupitia shahidi wake wa nane H 3827 Ditektivu Koplo Salum Ally ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa kisayansi katika idara ya picha kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023, inasikikizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina.
Milembe (43), aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha ugavi GGML aliuawa usiku wa kuamkia Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali mwilini, ikiwamo kichwani, usoni na mikononi.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni, Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Deus Pastoy, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55), ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe Seleman.
Akitoa ushahidi wake jana jioni, Koplo Ally akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Merito Ukongoji amesema Juni 5,2023 akiwa kazini alipokea bahasha yenye kielelezo kutoka kwa Koplo Jofu ikitoka kwa Mkuu wa Upelelzi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Geita(RCO).
Ameeleza kuwa, ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na barua na diski mweko (flash disc) na kwamba barua hiyo ilitaka ufanyike uchunguzi wa picha hizo za CCTV za mjongeo na za mnato .
Koplo Ally ameeleza kuwa baada ya kupokea na kuweka namba na kuandika kwenye kitabu maalumu kilichopo kwenye chumba cha maabara za picha, alizipeleka kwa mkuu wake kwa ajili ya kupanga mtu wa kufanya uchunguzi.
Hata hivyo, shahidi huyo ameeleza kuwa Agosti Mosi, 2023 alirudishiwa jalada na mkuu wake akimtaka aendelee na uchunguzi na kuandika taarifa ya uchunguzi.
Koplo Ally amefafanua kuwa Polisi Geita walitaka kupata majibu ya vitu viwili ambavyo ni ulinganisho pamoja na uthibitisho wa picha hizo na kwamba uchunguzi wake ulibaini kuwa picha hizo ni halisi.
Shahidi huyo amedai hakuweza kulinganisha picha hizo kutokana na CCTV kuwa mbali (zilinaswa kutokea mbali) , hivyo endapo angezivuta (kuzikuza) zingepoteza uhalisia wake.
Alipoulizwa na Wakili wa Serikali Merito Ukongoji kuwa alitambuaje kama picha hizo ni halisi, shahidi huyo alidai video hizo zilikuwa na kivuli, zina rangi na eneo husika (zilikonaswa) likionekana na rangi yake asilia.
Video hizo saa zilioneshwa mahakamani kupitia televisheni iliyoandaliwa kwa lengo hilo, zilionesha saa11:36 watu watatu wakiingia ndani ya geti, saa 11:47 dereva bajaji anakuja na 11:53 watu wanne ambao ni wanaume watatu na mmoja aliyevaa dela wanatoka na kupanda bajaji.
Hata hivyo, alipoulizwa na Wakili Laurent Bugoti wa upande wa utetezi kama anawatambua watu hao shahidi huyo amedai hawatambui na pia eneo zilikopigwa pia hazitambui kwa kuwa sio yeye aliyefanya upelelezi.
Jana mapema, shahidi wa tano katika kesi hiyo amedai alama za vidole katika chupa iliyokutwa eneo la tukio la mauaji hayo zilifanana na alama za vidole vya mshtakiwa wa tatu.
Shahidi huyo PF 25416 Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (ASP) Peter Joseph, kutoka Maabara ya Sayansi Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Peter akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Grace Kabu ameieleza Mahakama kuwa ndiye aliyefanya uchunguzi wa alama za vidole zilizokuwa kwenye sampuli za aina ambili alizopelekewa kuzifanyia uchunguzi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Geita.
Amebainisha kuwa, Mei 12,2023 alipokea kutoka kwa Detektivu Sajent Hashim, vielelezo vya X-X1, ambavyo vilikuwa ni sampuli ya alama za vidole zilizopatikana eneo la tukio.
Vielelezo vingine vilikuwa na alama A-A1 ambazo ni sampuli za alama za vidole zenye jina la Genja Deus Pastory (mshtakiwa wa tatu) na alitakiwa kuchunguza alama za vidole katíka sampuli zilipatikana eneo la tukio kama zinaendana na alama za sampuli zilizochukuliwa Polisi Geita.
"Niligundua alama ya vidole kwenye sampuli X-X1 inalingana kitabia na uhalisia wake na alama za vidole katika sampuli A-A1, ambazo ni alama za kidole cha kati cha Genja Pastory.
"Sina shaka alama za vidole zilizochukuliwa eneo la tukio na zilizochukuliwa kituo cha polisi ni za Genja Pastory."
Baada ya maelezo hayo shahidi huyo aliiomba Mahakama ipokee ripoti ya uchunguzi ya alama za vidole iliyoambatanishwa na kitabu cha picha alizopiga kwa mfumo wa kiektroniki kwa kutumia kamera na kompyuta ili zikubalike kama kielelezo mahakamani hapo.
Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na Wakili Liberatus John anayemtetea mshtakiwa wa kwanza akiiomba Mahakama hiyo isipokee kitabu hicho cha picha kwa kuwa picha hizo zimekuzwa kwa kutumia mfumo wa kielektroniki kwa kutumia kompyuta hivyo kuufanya uwe ushahidi wa kielektroniki.