Prime
Huyu ndiye Hashim Lundenga ‘Anko’ aliyeamini katika sanaa

Dar es Salaam. Tanzania imeingia kwenye majonzi mazito kufuatia kifo cha gwiji katika sekta ya burudani, sanaa na michezo, Hashim Lundenga.
Lundenga amefariki dunia leo Aprili 19, 2025, baada ya kuugua kwa muda mrefu na atazikwa Jumatatu Aprili 21, katika makaburi ya Kidatu, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Hashim Lundenga au maarufu kwa jina la “Anko Hashim” si jina tu, bali ni alama ya mapinduzi ya kijamii, kiutamaduni na hata kiuchumi kwa vijana wengi wa Kitanzania kupitia tasnia ya urembo na burudani kwa ujumla.
Kwa wengi walioishi na kushuhudia kazi zake, jina la Lundenga linabeba kumbukumbu ya mashindano ya Miss Tanzania.
Hata hivyo, mchango wake haukuishia hapo. Aligusa maisha ya wasanii, wanamichezo, waandishi wa habari na hata viongozi wa kisiasa kwa namna ya kipekee – akitumia jukwaa la sanaa kama nguzo ya kuijenga jamii.
Lundenga alianza maisha yake ya kikazi kama muajiriwa katika kampuni ya kiwanda cha nguo cha Urafiki.
Huko ndiko alipoanza kujulikana kama mpenda burudani, akiwa mmoja wa waasisi wa Chama cha Disco Tanzania (TDMA) –kilichokuwa kinashughulika na mashindano ya muziki wa disco na burudani mbalimbali nchini.
Kupitia TDMA, Lundenga alianza kama katibu wa chama hicho kabla ya kupanda hadi kuwa mwenyekiti.
Katika nafasi hii, aliweza kuendesha mashindano ya disco ambayo yalitikisa miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Mashindano hayo yaliwavutia vijana wengi na kutoa majukwaa kwa vipaji vipya kujitokeza.
Hii ilikuwa ni hatua ya mwanzo tu kwa Lundenga – mtu ambaye daima aliamini kuwa sanaa na burudani vinaweza kuwa chombo cha mabadiliko katika jamii.
Mwanzo wa Miss Tanzania
Katika harakati zake za kutafuta njia mpya za kukuza vipaji na kuinua wasichana wa Kitanzania, Lundenga alikuja na wazo la kuandaa mashindano ya Miss Tanzania.
Wazo hilo liliwekwa kwenye utekelezaji mwaka 1993, na hatimaye mnamo mwaka 1994, shindano la kwanza la Miss Tanzania likaandaliwa na kufanyika kwenye Hoteli ya White Sands.
Mrembo Aina Maeda aliibuka mshindi wa kwanza kabisa wa taji hilo.
Lundenga alifanikiwa kuandaa mashindano haya kwa kushirikiana na Prashant Patel, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania kwa kipindi hicho.
Huu ulikuwa mwanzo wa historia mpya nchini – historia ya kuwawezesha wanawake kupitia sanaa ya urembo na utamaduni.
Changamoto na mapambano
Mwaka 1995, Lundenga alikumbana na changamoto kubwa ya kwanza katika safari yake ya Miss Tanzania.
Mshindi wa mwaka huo, Emily Adolf, alikuwa mwanafunzi na hilo likaleta mgogoro mkubwa na Serikali. Ilifikia hatua ambapo mashindano yalitishiwa kufungiwa.
Hata hivyo, Lundenga hakukata tamaa. Akiwa pamoja na washirika wake, walipambana vilivyo kulinda heshima ya mashindano hayo.
Hatimaye walifikia makubaliano na Serikali kuwa hakuna mwanafunzi ambaye ataruhusiwa kushiriki tena katika mashindano ya Miss Tanzania – makubaliano yaliyoweka msingi imara wa utaratibu mpya wa mashindano hayo.
Kupandisha hadhi ya mashindano
Baada ya mgogoro huo, Lundenga alijikita katika kuyapandisha hadhi mashindano ya Miss Tanzania. Aliingia kwenye mbio za kusaka wadhamini ili kuyawezesha kuwa na mvuto na tija zaidi.
Jitihada hizo zilipewa baraka kubwa mwaka 1997, baada ya kampuni ya sigara ya Aspen kuingia kama mdhamini mkuu. Mshindi wa mwaka huo, Saida Kessy kutoka Arusha, alizawadiwa gari – hatua iliyoongeza hamasa ya mashindano hayo kwa vijana wa kike nchi nzima.
Ujio wa zawadi hizo kubwa haukuishia kwenye magari tu. Katika miaka ya baadaye, Lundenga aliweza kuwaalika wasanii wa kimataifa kama TKZee kutoka Afrika Kusini ili kuongeza mvuto wa burudani katika usiku wa mashindano.
Mwaka wa mapinduzi – 2005
Kwa wengi wanaofuatilia historia ya Miss Tanzania, mwaka 2005 unatajwa kama mwaka wa mapinduzi makubwa.
Ni mwaka ambao Nancy Sumari aliibuka mshindi wa shindano hilo chini ya udhamini wa kampuni ya Ocean Sandals (OK Plast).
Nancy alizawadiwa nyumba maeneo ya Tabata – zawadi ambayo ilibeba ujumbe mkubwa kwa jamii kuhusu thamani ya vipaji vya wanawake.
Nancy hakusimama hapo tu – alienda mbele kushinda taji la Miss World Africa na kuwa miongoni mwa warembo 10 bora duniani. Hili lilikuwa tukio la kihistoria ambalo liliweka Tanzania kwenye ramani ya dunia kupitia sanaa ya urembo – yote chini ya udhamini, uongozi na maono ya Anko Hashim.
Zaidi ya urembo
Licha ya mafanikio ya Miss Tanzania, mchango wa Lundenga haukuishia kwenye urembo. Katika kuhakikisha kuwa warembo wanakuwa na fikra ya maendeleo, Lundenga aliwashauri warembo kuanzisha taasisi za kusaidia jamaa.
Kupitia taasisi hizo, warembo waliweza kujihusisha na shughuli za kijamii hata baada ya msimu wao kumarika. Mfano wa warembo hao ni Brigitte Alfred ambaye alianzanisha taasisi yake ijulikanayo kwa jina la BAF ambayo ilisaidia katika mapambano kupinga fikra potufu dhidi ya albino mwaka 2013.
Pia Lundenga alitumia jukwaa hilo kusaidia wasichana kupata ajira, nafasi za masomo nje ya nchi, na hata fursa za ujasiriamali. Alikuwa muumini mkubwa wa kuwawezesha wanawake na vijana kwa ujumla.
Aliwahi kusema: “Mrembo si sura tu, bali ni akili, maadili na dhamira ya kusaidia jamii yake.” Kauli hiyo iliakisi namna alivyotumia sanaa kama chombo cha mabadiliko ya kweli.
Lundenga pia alikuwa mshauri na mlezi wa mashindano ya vipaji mbalimbali, na mara kadhaa alishirikiana na vyombo vya habari na taasisi binafsi kuhakikisha vijana wanapata fursa za kuonyesha uwezo wao.
Kifo cha Hashim Lundenga ni pigo kubwa kwa Tanzania. Ni pengo ambalo halitazibika kirahisi.
Familia, marafiki, wadau wa burudani na wasanii wamepoteza mlezi, rafiki na kiongozi. Kwa walio wengi, yeye ni kama baba wa sanaa ya kisasa nchini – mtu aliyeona mbali kuliko wenzake na kutengeneza njia ambapo haikuwepo.
Wengi wa warembo waliopita katika mashindano ya Miss Tanzania wameendelea kuwa viongozi, wafanyabiashara, mabalozi wa mashirika ya kimataifa na wanaharakati wa maendeleo ya jamii.
Haya yote ni matunda ya mbegu alizopanda Lundenga kwa moyo wa dhati.
Lundenga ameacha alama isiyofutika. Maisha yake ni somo la maono, uvumilivu, kujituma na imani kwa vijana. Ametufundisha kuwa sanaa ni zaidi ya burudani – ni chombo cha kuleta mabadiliko.
Tutaendelea kumkumbuka si tu kwa mashindano ya Miss Tanzania, bali kwa maisha aliyoyaishi – maisha ya huduma kwa jamii.
Pumzika kwa amani “Anko” Hashim Lundenga, gwiji wa sanaa, burudani na maendeleo ya vijana Tanzania. Taifa litakukumbuka daima.