Prime
Ripoti uchunguzi mauaji ya Milembe wa GGM yapokewa

Washtakiwa wa kesi ya mauaji ya Milembe Seleman aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu GGM wakiwa Mahakama Kuu Geita.
Muktasari:
- Kesi hiyo ilianza kusikilizwa jana, kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao ambapo shahidi wa pili na wa tatu waliieleza mahakama namna simu za marehemu Milembe zilivyopatikana kwenye shimo la choo.
Geita. Mahakama Kuu Kanda ya Geita imepokea ripoti ya uchunguzi wa sampuli za mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya Madini ya Dhahabu ya Geita (GGM), Milembe Seleman na kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa jana, kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao mahakamani ambapo shahidi wa pili na wa tatu waliieleza mahakama namna simu za marehemu Milembe zilivyopatikana chooni.
Leo Jumanne Aprili 9, 2024, Mahakama hiyo imeendelea na kesi hiyo na imepokea ripoti kutoka kwa shahidi wa tano wa upande wa mashtaka, lakini ikakataa kupokea kitabu cha picha baada ya kukubaliana na pingamizi la mawakili wa utetezi waliopinga kitabu hicho kisipokelewe kama kielelezo.
Washtakiwa katika kesi hiyo namba 39/2023 ni, Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Deus Pastoy, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55), ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe Seleman.
Milembe (43), aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha ugavi katika kampuni ya GGML aliuawa Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali mwilini, ikiwemo kichwani, usoni na mikononi.
Leo shahidi wa tano ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (ASP), Peter Joseph akiongozwa na wakili wa Serikali Grace Kabu, ameiieleza mahakama kuwa ndiye aliyefanya uchunguzi wa alama za vidole za mshtakiwa.
“Nilichunguza alama za X-Xi na zile za Ana A1 niligundua sampuli za alama ya vidole A ni ya kidole cha kati cha mkono wa kushoto wa Genja Deus Pastoy (mshtakiwa wa tatu) na tabia za alama za vidole zililingana kitabia na uhalisia wake,” amedai ASP Peter.
Shahidi huyo ameiomba mahakama ipokee ripoti ya uchunguzi ya alama za vidole aliyoiambatanisha na kitabu cha picha alizopiga kwa mfumo wa kielektroniki kwa kutumia kamera na kompyuta ili zikubalike kama kielelzo mahakmani hapo.
Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na Wakili Liberatus John anayemtetea mshtakiwa wa kwanza aliyeiomba mahakama isipokee kielelezo hicho akidai picha hizo zimekuzwa kwa kutumia mfumo wa kielektroniki kwa kutumia kompyuta.
“Mheshimiwa jaji ushahidi wa kielektroniki unakubalika chini ya kifungu cha 64A cha Sheria ya Ushahidi Sura namba 6, lakini ili ushahidi wa kielektroniki uweze kuingia mahakamani, lazima ufuate masharti ya kifungu cha 18(3) cha Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2025,” amedai Wakili John.
Amefafanua kuwa kifungu kinataka kabla ya ushahidi wa kielektroniki kupokelewa mahakamani, inabidi kompyuta iliyotumika iwepo pia.
Wakili mwingine wa utetezi, Erick Lutehanga ameungana na Wakili John kwa kukumbushia kesi ya Freeman Mbowe na wenzake saba dhidi ya Jamhuri iliyokuwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania masjala ndogo ya Dar es Salaam ya mwaka 2022.
Hata hivyo, Wakili Kabu ameiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo akidai halina mashiko kisheria kwa kuwa kitabu cha picha kina alama za vidole na alama hizo ni sampuli ambazo shahidi aliletewa kwa ajili ya uchunguzi.
Ameiambia Mahakama kuwa kompyuta ilitumika kama kioo kuangalia picha kutoka kwenye kamera na kuhusu ubora wa vifaa vilivyotumika ni suala la ushahidi, ambalo shahidi anaweza kuulizwa maswali.
Hata hivyo, katika uamuzi wake, Jaji Kelvin Mhina anayesikiliza kesi hiyo amekubaliana na pingamizi la upande wa utetezi na kukataa kukipokea kitabu hicho cha picha kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Shahidi wa sita ambaye ni ofisa tabibu wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Christopher Matola aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Milembe Seleman, ameieleza Mhakama kuwa chanzo cha kifo kilitokana na kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na majeraha makubwa ya kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Matola amedai kuwa mwili wa Milembe ulikutwa na majeraha makubwa kichwani na shingoni, mkono wake wa kulia, kiganja kimoja kilikuwa kimeondolewa na kingine hakina vidole vitatu.
Shahidi huyo amedai kuwa eneo la usoni kipande cha mfupa kilikatwa na kitu chenye ncha kali huku begani alikuwa na jeraha kubwa la kukatwa na mwili huo ulikuwa umetapakaa damu.
Kabla ya ushahidi huo, jana jioni ambapo shahidi wa pili H4050 Koplo Philemon na wa tatu Noel Ngasa (41) mwenyekiti wa Mtaa wa Mwatulole waliieleza mahakama kuwa Mei 7, 2023, Genja aliwapeleka eneo la Mwatulole ambako aliwaonyesha eneo la shimo la choo alikotumbukiza simu za marehemu.
Mashahidi hao walidai kuwa baada ya wazamiaji kuingia ndani ya shimo hilo walitoka na simu mbili aina ya Iphone na Sumsung.
Tayari mashahidi wanane kati ya 32 wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi wao wakiongozwa na mawakili wa Serikali Merito Ukongoji ,Grace Kabu wakisaidiana na Scolastica Teffe na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 10, 2024 ambapo shahidi wa tisa anatarajiwa kutoa ushahidi wake.