Magereza yatangaza mpango wa kujitosheleza kwa chakula

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo akijibu maswali ya wabunge leo Mei 14,2025 bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Katika kuhakikisha kuwa Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula limekuja na mpango mkakati wa miaka mitano.
Dodoma. Jeshi la Magereza Tanzania limeandaa mpango mkakati wa miaka mitano (2025/2026 – 2029/2030) wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na mahabusu.
Wazo hilo kwa mara ya kwanza lilitolewa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, akiwa katika ziara Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani Juni 22, 2017.
“Nimechoka kuwalisha wafungwa, mtu afungwe halafu anunuliwe chakula. Nimeshatoa maagizo, wafungwa hawa wakalime ili waogope kufungwa,” alisema Rais Magufuli.
“Wakajifunze kulima, wajue kufungwa ni kufungwa na neno kufungwa ni kufungwa kweli. Tukianza kuwapunguzia maeneo magereza, mnataka wakalime wapi,” alihoji.
Leo Jumatano, Mei 14, 2025, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo akijibu swali la msingi la Mbunge wa Lulindi (CCM), Issa Mchungahela ameeleza kuanza kwa mpango huo wa miaka mitano.
Mbunge huyo amehoji Serikali ina mpango gani madhubuti wa kuwatumia wafungwa kuzalisha chakula chao wenyewe badala ya kununua.
Akijibu swali hilo, Sillo amesema Serikali kupitia Jeshi la Magereza imeandaa mpango Mkakati wa miaka mitano (2025/2026 – 2029/2030) wa kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na mahabusu.
“Mpango huo unatekelezwa kwa kuboresha kilimo cha umwagiliaji ambacho kitaongeza uzalishaji wa mazao ya chakula hadi kufikia tani 46,267 za mahindi, tani 6,359 za Mpunga, tani 7,757 za maharage, na tani 1,750 za Mafuta ya kula ifikapo Juni, 2030,” amesema.
Katika swali la nyongeza, Mchungahela amesema wafungwa wamekuwa wakiishi kwa ruzuku inayotolewa na Serikali, lakini wakitoa nje wamekuwa wakiishi kwa shida sana.
“Je Serikali ina mkakati gani wenye tija utakaowapatia mazao mengi ili wapate kutosheleza mahitaji yao na lakini pia na kupata mitaji pale wanapotoka nje,”amehoji?
Akijibu swali hilo la nyongeza, Sillo amesema mkakati wa Serikali ni huo wa miaka mitano wa kuhakikisha wanazalisha chakula cha kutosha kwa wafungwa na mahabusu walioko magerezani, lakini hata kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali.
“Ndani ya miaka mitano tuhakikishe uzalishaji unakua na tija inaongezeka,”amesema Sillo.