Siha. Serikali imeunda timu ya wataalamu kuchunguza tukio la mama mjamzito anayedaiwa kufariki wakati akijifungua katika Kituo cha Afya cha Ngarenairobi wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro, tukio lililoibua hasira za wananchi.
Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia Septemba 20, 2023 baada ya mjamzito huyo, Dainess Massawe (35) kudaiwa kujifungua kwa upasuaji, lakini ikadaiwa daktari anayedaiwa kufanya upasuaji huo alifanya kwa uzembe.
Kichanga kilichozaliwa amehamishiwa hospitali ya Wilaya ya Siha kwa uangalizi.
Taarifa nyingine ambazo hazijathibitishwa na mamlaka yoyote, zilidai pengine daktari huyo alikuwa ‘amechangamka’ wakati alipoitwa kwa dharura kuokoa maisha ya mwanamke huyo baada ya kupata uchungu na kupelekwa kituoni hapo.
Mganga Mkuu (RMO) wa mkoa wa Kilimanjaro, Dk Jeiry Khanga alisema wameshapeleka wataalamu kufuatilia tukio la kifo cha mwanamke huyo na kwamba watakapokamilisha watapeleka taarifa hizo kwa mamlaka husika.
"Tangu jana tulipeleka wataalamu wanafuatilia kuhusu kifo hicho na nitalitaarifu kwa mamlaka zinazohusika," alisema Dk Khanga.
Hata hivyo, hakutaka kuingia kwa undani wa taarifa hiyo, akisema mwenye mamlaka ya kulizungumzia ni mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, ambaye naye alithibitisha kutumwa kwa timu hiyo.
"Tumepata tukio moja la mama mjamzito kupoteza maisha katika kituo cha afya cha Ngarenairobi aliyepoteza maisha kwa kujifungua na wananchi walihamaki kutokana na tukio hilo na wengine walikwenda katika kituo hicho, lakini hatua tulizochukua ni kuwatuliza wananchi.
"Timu ya wataalamu wa afya kutoka wilaya hiyo ilikwenda pale kupata taarifa za awali za tukio hilo na kuangalia hasa ni nini kilichosababisha kifo hicho, lakini pia ilikuwa na timu huru ya watu kutoka mkoani,” alieleza mkuu huyo wa wilaya.
Alisema baada ya hapo watachukua hatua kutokana na mapendekezo yatakayotolewa.
Mume, wananchi wafunguka
Akisimulia tukio hilo, mume wa marehemu, Elikunda Ikera alisema mke wake alipofikishwa hospitalini hapo akiwa na uchungu, alishindwa kupata huduma kwa wakati, licha ya wagonjwa waliokuwepo wodini kuita madaktari.
Ikera alidai Septemba 19 saa nne usiku, mke wake alikuwa amezidiwa na walipofika hospitali, mkewe alipiga kelele kuomba msaada na wakati huo hakukuwa na daktari hata mmoja katika kituo hicho.
“Kelele zilipigwa sana ili madaktari waweze kujitokeza lakini hakuna, ikabidi wagonjwa watusaidie kupiga kelele, kelele zilipokuwa nyingi akatokea daktari mmoja akaanza kuwapigia wenzake simu.
"Tulifika hospitali saa nne usiku lakini daktari alikuja saa saba usiku akiwa amechangamka. Walimchukua mke wangu na kumpeleka chumba cha upasuaji, walimfanyia upasuaji wakamtoa mtoto na kisha akarejeshwa wodini,” alisema.
Alisema wakiwa wanamsubiri mgonjwa, walipata taarifa kuwa amefariki na walipoanza kudai mwili tangu saa 3 asubuhi walikuja kupewa saa 12 jioni na wakati wanatafuta gari, daktari mmoja aliwaambia watafute ambulance.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Loveness Mmbaga alisema: "Tukiwa msibani tulipata taarifa mwenzetu amefariki, ikabidi sisi tuwe wakali tukaenda pale kituoni, kilichotukasirisha ni mwili kuwekwa pale muda mrefu.”