Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabaraza ya Habari Afrika kukutana Arusha

Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), Ernest Sungura (aliyevaa miwani) akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 2,2025 kuhusu mkutano huo,kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha(APC), Claud Gwandu.

Muktasari:

  • Dk Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Arusha. Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa pili wa mabaraza ya Habari Afrika 2025, ulioandaliwa na Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA) kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Mkutano huo wa siku tatu utaanza Julai 14 hadi 17,2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ambapo Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajiwa kumwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 2, 2025 jijini Arusha, Katibu Mtendaji wa MCT ambaye pia ni Mwenyekiti wa NIMCA, Ernest Sungura amesema mkutano huo utashirikisha washiriki zaidi ya 500 kutoka mataifa 19 wanachama wa umoja huo.

Amesema mkutano huu unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kukuza ushirikiano wa kitaasisi, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuimarisha uhuru na uwajibikaji wa vyombo vya habari barani Afrika, ambapo washiriki wengine watatoka nje ya Bara la Afrika.

“Katika mkutano huo tulitarajia Rais Samia awe mgeni rasmi ila atawakilishwa na Dk Mpango na mkutano huo utaongozwa na kauli mbiu isemayo “Uboreshaji usimamizi wa vyombo ya habari na mawasiliano ni msingi wa weledi wa uandishi wa habari”,” amesema.

Sungura amewataja miongoni mwa wageni maalumu watakaohudhuria mkutano huo ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Zanzibar, Dk Hussein  Mwinyi, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Dk Tawfik Jelassi na mawaziri wa habari wa Kenya, Uganda, Zambia na Nigeria.

“Katika mkutano huo mada mbalimbali ikiwemo matumizi ya akili mnemba na masuala ya kijinsia na ulemavu yanavyopaswa kupewa kipaumbele yatajadiliwa. Pia, MCT tutazindua maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake,” amesema.


Mwongozo wa MCT kuhusu uchaguzi mkuu

Aidha, Baraza hilo limetoa mwongozo kwa wanachama, waandishi wa habari na umma wakati wa uchaguzi ambapo Sungura amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 21 (1) inampa raia haki ya kugombea nafasi za kisiasa.

“Hii inajumuisha haki ya kupiga kura na kugombea katika chaguzi mbalimbali, kwa hiyo waandishi wa habari wana haki ya kugombea nafasi za kisiasa kama ilivyo kwa raia wengine.”

“Hata hivyo, kuendelea kuwa mwandishi wa habari huku ukijihusisha na siasa ni kinyume cha maadili ya taaluma hii. Mwongozo unaelekeza kwamba mwandishi anayegombea nafasi ya kisiasa anapaswa kuondoka kwenye chumba cha habari ili kuepuka mgongano wa masilahi na kupoteza uaminifu wa umma,”

Katibu huyo amesema waandishi wa habari wanaojihusisha na siasa kwa kugombea nafasi za uongozi huku wakiendelea na kazi yao, wanakabiliwa na athari kubwa kwa taaluma yao na tasnia ya habari kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu, ametoa wito kwa waandishi kuhakikisha wanajisajili kupitia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), ili kutambulika kisheria na kuimarisha hadhi ya taaluma hiyo nchini.