Tanzania mwenyeji mkutano wa mabaraza ya vyombo vya habari Afrika

Muktasari:
- Mkutano huu unafanyika Tanzania wakati ambao takwimu za World press freedom index inayoratibiwa na Taasisi ya Reporters without boarders (RWB) (RSF) zinaonyesha Tanzania kufanya vizuri kwenye kuheshimu uhuru wa habari kwa kushika nafasi ya 97 kwa mwaka 2024, toka nafasi ya 142 kwa mwaka 2023.
Dar es Salaam. Wakati jitihada mbalimbali za kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini zikiendelea kufanyika, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa mabaraza ya habari Afrika.
Jitihada hizo zimeifanya Tanzania sasa kushika nafasi ya 97 katika nchi zinazozingatia uhuru wa vyombo vya habari ikiwa imepanda kutoka nafasi ya 142 mwaka 2023 kwa mujibu wa takwimu za World press freedom index inayoratibiwa na Taasisi ya Reporters without boarders (RWB)
(RSF)
Hayo yameelezwa na Mtendaji mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Julai 14 hadi 17, 2025 jijini Arusha.
Amesema mbali na mkutano huo, pia MCT imesema iko mbioni kufanya utafiti kuangazia mabadiliko ya sheria na uwepo wa bodi ya ithibati una maana gani na athari zipi katika tasnia ya habari.
Sungura amesema wanaandaa mkutano huo kwa mara ya kwanza kwa kushirikiana na Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika, Umoja wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kama mshirika mahususi.
“Mikutano mingine ya kimataifa itafanyika sambamba na mkutano huo ukiwamo wa East Africa Press Councils (EAPC), na World Association of Press
Councils (WAPC),” amesema.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 500 ambapo 150 watatoka nchi mbalimbali duniani.
“Mkutano huu unabebwa na kauli mbiu isemayo: Uboreshaji wa Sheria za Habari na Mawasiliano kwa Ajili ya Umahiri wa Uandishi wa Habari Afrika,” amesema.
Mambo yatakayoguswa ni mijadala ya kitaalamu kuhusu changamoto mbalimbali zinazoathiri tasnia ya habari na namna mabaraza ya habari kote duniani yanavyokabiliana na changamoto hizo.
Amesema pia kutakuwa na maonyesho ya habari kwenye Tehama.
“Kupitia maonyesho hayo yaliyo wazi ndani na nje ya nchi itawezesha walio na teknolojia zao kuzionyesha ili watu wa vyombo vya habari waweze kuona na kuamua kufanya mabadiliko ya teknolojia wanazotumia ikiwemo Akili Mnemba,” amesema Sungura.
Kupitia mkutano huo ndipo uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania.
Katika uzinduzi wa maadhimisho hayo wanachama wa MCT, wengi wao vyombo vya habari, taasisi za kihabari na vyuo vya uandishi wa habari watakuwa wakikumbuka na kujifunza jinsi gani walivyomudu kuzingatia weledi na maadili ya tasnia ya habari kwa kujisimamia.
Mkutano huo kwa mujibu wa Sungura unatarajiwa kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akitarajiwa kuwa mgeni maalumu wa mkutano huo kushuhudia tuzo mahsusi za miaka 30 ya MCT.
Mgeni mwingine mashuhuri ni Naibu Mkurugenzi Mkuu, Mawasiliano na Habari wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Dk Tawfik Jelassi , wakitarajia pia kuwapo kwa baadhi ya mawaziri wa sekta ya habari na mawasiliano kutoka katika mataifa ya Afrika kuhudhuria.
Akizungumzia utafiti ambao utaanza kufanyika baadaye mwaka huu, Sungura amesema miongoni mwa mambo yatakayoangaliwa ni sheria ya vyombo vya habari, sera ya habari ya mwaka 2003, tume ya uchumi wa vyombo vya habari, tathmini ya miaka 30 ya MCT.