Mabaraza huru ya habari duniani kukutana Tanzania

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Ernest Sungura akizungumza wakati wa mafunzo ya menejimenti kwa waandishi waandamizi wanawake Tanzania.
Muktasari:
- Wakati mkutano huo ukitarajiwa kufanyika Julai 14 – 17, 2025, vyombo vya habari na waandishi wa habari wamehamasishwa kuandaa kazi zilizoleta mabadiliko katika jamii kwa ajili ya maonyesho katika mkutano wa mabaraza huru ya habari duniani.
Dodoma. Mkutano mkuu wa mtandao wa mabaraza ya huru ya habari duniani unatarajiwa kufanyika nchini Julai 14 hadi 17, 2025 jijini Arusha ambapo vyombo vya habari vimetakiwa kuandaa maonyesho ya kazi zilizoleta mabadiliko katika jamii na Taifa.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura ameyasema hayo leo Mei 26, 2025 wakati wa kufungua mafunzo ya menejimenti kwa waandishi wa habari waandamizi wanawake jijini Dodoma.
Amesema mkutano huo ambao MCT itakuwa mwenyeji, utayakutanisha mabaraza ya habari na utakuwa ni fursa ya wanahabari wa Tanzania kuonyesha kazi zao zilizochangia mabadiliko katika jamii na Taifa, na kushiriki katika mijadala mbalimbali itakayofanyika wakati wa mkutano huo.
Sungura ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Barani Afrika (NIMCA), amevihamasisha vyombo vya habari nchini na waandishi wa habari wakati utakapofika vijisajili ili viweze kushiriki kikamilifu.
Kuhusu mafunzo kwa waandishi wa habari waandamizi wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini, Sungura amesema yamelenga kuwajengea uwezo, kujiamini na kuwapa nyenzo muhimu za kuwa viongozi au wasimamizi wenye tija katika vyumba vya habari.

Mshauri wa Masuala ya Habari Edda, Sanga akizungumza katika mafunzo kwa waandishi wa habari waandamizi wanawake.
“Mafunzo hayo tumeyaandaa ili kuwaongezea ujuzi na maarifa wakati wa kuchakata habari ili ziwe na ujumuishaji wa masuala ya kijinsia, ni katika kuhakikisha maudhui yanakuwa na jicho la kijinsia,” amesema.
Akiwasilisha mada ya utangulizi katika usimamizi na majukumu muhimu na ujuzi wa wasimamizi bora wa mameneja wa vyombo vya habari, mshauri wa masuala wa habari, Edda Sanga amewataka mameneja wanawake katika vyombo vya habari kujiamini katika utekelezaji wa majukumu yao.
Pia, amesema mameneja hao wanatakiwa kuwa waadilifu katika kazi zao kwa kuhakikisha vyombo vyao vinakuwa na kazi bora.
“Media manager (mameneja wa vyombo) ni mtu muhimu kwa sababu wewe ndio kichocheo wa mambo yote mazuri kwa chambo chako, so (hivyo) siku zote unatakiwa kuwa na uelewa mpana wa mambo ya ndani ya ofisi na nje,” amesema.
Amewataka kuwa na umoja siku zote za kazi zao kwa kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za wanawake viongozi badala ya kuungana kuwagandamiza.
“Msifanye ushindani kwa ubaya, kutaka aliye juu yako ashindwe, jaribuni sana kushirikiana katika kazi zenu,” amesema Edda.