Kibano waandishi wanaoingia kwenye siasa

Muktasari:
- Wadau watoa mitazamo tofauti, wengine wataka wasirudi kwenye taaluma, huku wengine wakitaka wapangiwe majukumu mengine.
Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeweka msimamo kwa waandishi wa habari waliotangaza na wale wenye nia ya kuingia kwenye siasa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kutoendelea kufanya kazi za uandishi wa habari.
Msimamo wa bodi hiyo umekuja kipindi ambacho baadhi ya waandishi wa habari tayari wameshatangaza nia ya kutaka kugombea ubunge na udiwani katika majimbo na kata mbalimbali nchini kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Msimamo wa bodi hiyo umetazamwa kwa sura tofauti na baadhi ya wadau wa tasnia ya habari, wengine wakishauri uwe mkali zaidi kwa kutoruhusu mwanataaluma atakayeingia kwenye siasa kurudi kuendelea na kazi ya uandishi baada ya uchaguzi na wengine kuwa na maoni tofauti.
Wakati kukiwa na maoni tofauti juu ya msimamo huo, baadhi ya vyombo vya habari nchini tayari vina utaratibu wa kutoruhusu wafanyakazi wake kuingia kwenye siasa na kurudi kazini baada ya kinyang'anyiro, licha ya msimamo wa bodi kutoa mwanya wa kurudi kazini ikitokea umeshindwa siasa.
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Tido Mhando akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Julai 26, 2025, amesema msimamo wa kutoendelea na shughuli za uandishi wa habari kwa mwanahabari atakayeingia kwenye siasa, akisisitiza wote wenye nia hiyo wajiweke kando na kazi ya uandishi.
"Utaratibu ni kwamba wakati huu wale waandishi wa habari wenye nia na waliokwishatangaza nia ya kugombea kwenye uchaguzi mkuu wanatakiwa kujiweka pembeni na shughuli za uandishi wa habari mpaka outcome (matokeo) yao itakapotokea.
"Hii ina maana kwamba kama ameweka nia ya kugombea, kuna hatua za kuteuliwa. Katika kipindi chote cha mchakato huyu mwandishi wa habari anatakiwa afuate utaratibu na kuacha kufanya shughuli za uandishi wa habari," amesisitiza Tido.
Amesema pamoja na kwamba katika mataifa mengine, mwandishi wa habari anapoingia kwenye siasa moja kwa moja harudi kwenye taaluma, kwa Tanzania bodi imeona atakayekwaa kisiki huko, arejee kuendelea na taaluma yake.
"Ikiwa ameshindwa kuchaguliwa huko kwenye siasa, basi atarudi kuendelea na kazi, lakini si kuwa mwandishi wa habari wakati huohuo akiwa mgombea, hii hairuhusiwi.
"Bodi imeweka utaratibu huo, ingawa huko duniani ukiamua umeamua moja kwa moja, ukishindwa haurudi. Sisi tukasema katika kipindi hiki akifanikiwa ataendelea na siasa, asipofanikiwa atarudi kwenye tasnia," amesema.
Amesema lengo la kuweka utaratibu na msimamo huo ni kuondoa sintofahamu ya kuonekana kuna harufu ya upendeleo kwa mwanahabari ambaye yupo kwenye kinyang'anyiro cha siasa.
Kwa mujibu wa Tido, mwandishi wa habari anapoingia kwenye siasa moja kwa moja anakuwa amejichagulia upande aliopo, hivyo kuonyesha pia upendeleo katika kufanya kazi za uandishi wa habari jambo ambalo kitaaluma halitakiwi.
"Hicho ndicho tunachotaka kukiepuka katika tasnia, pamoja na kwamba mwisho wa siku huyo mwandishi wa habari aliyeingia kwenye siasa atakuwa amefahamika yupo upande gani hata baada ya mchakato.
"Lakini kipindi ambacho yupo kwenye kinyang'anyiro hatakuwa na product (bidhaa) ya kihabari anayoitoa, hii itasaidia kuondoa sintofahamu na watu kuhoji kwamba huyo mwandishi wa habari amefanya hiki kwa sababu hii," amesema.
Amesema baada ya mchakato wa uchaguzi kupita, kama mwandishi aliyeingia kwenye siasa hatakuwa amefanikiwa na akarudi kwenye taaluma, matokeo hayo yataendelea kumwathiri katika chombo anachofanyia kazi.
"Wapo watakaosema mwandishi huyo ni wa chama fulani halafu anaandika hivi, hiyo ndiyo itakuwa reaction (matokeo) kwenye chombo chake cha habari. Katika hili, inabidi tu tuvumiliane."
Utekelezaji
Akielezea mkakati wa utekelezaji wa hilo, Tido ambaye ni mwandishi mkongwe aliyefanya kazi ndani na nje ya nchi, amesema bodi katika kulisimamia na kuuzingatia utaratibu huo wametoa na wanaendelea kutoa taarifa kwa uongozi wa vyombo vya habari kote nchini kuzingatia msimamo huo kwa wanahabari wao watakaoingia kwenye siasa.
"Matumaini yetu ni kwamba viongozi wa vyombo vyote vya habari watawajibika ili kutimiza wajibu wao," amesema Tido, akivipongeza baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vina utaratibu wa wafanyakazi wao wanaoingia kwenye siasa, vingine huwaondoa kazini moja kwa moja wale wanaotangaza nia.
Mitazamo ya wadau
Baadhi ya wadau wa tasnia ya habari wamekuwa na maoni tofauti kuhusu msimamo wa bodi hiyo, wengine wakisisitiza wanahabari watakaoingia kwenye siasa wasirudi kwenye tasnia, na wengine wakidai sheria, hasa wanaogombea udiwani, inawaruhusu.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema msimamo wa bodi utasaidia kuondoa sintofahamu ya upendeleo kwa wanataaluma wanaojiingiza kwenye siasa kufanya pia kazi ya uandishi.
Aidha, Balile ameshauri wale wanaoingia kwenye siasa wasirudi kwenye tasnia ya habari, akitolea mfano mwandishi aliyeondoka kwenye taaluma hiyo na kujiunga na vyama vya siasa, hataaminika kufanya kazi ya kiuandishi kwenye chama kilichokuwa ni mpinzani akiwa mwanasiasa.
"Utakaporudi kwenye taaluma na kwenda kuwahoji watu waliokuwa wapinzani ni dhahiri watakuona kama kibaraka na si mwanahabari. Msimamo ungekuwa atakayeingia kwenye siasa asirudi, abaki huko huko kwani ndipo ana mapenzi napo," amesema Balile.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (Dar-PC), Bakari Kimwanga, amekuwa na mtazamo tofauti akieleza kuwa kwa anayegombea ubunge ni sawa, lakini kwenye nafasi ya udiwani, ambako yeye ameifanyia kazi, sheria inaruhusu.
"Kwenye udiwani au ukiwa unagombea serikali ya mtaa kunataka uwe na shughuli halali inayokuingizia kipato, hiyo ni sheria, sasa kwa mwandishi wa habari anayekwenda kugombea huko, ukimwambia asifanye kazi maana yake unataka awe mwizi,” amesema.
Kimwanga aliyekuwa diwani wa Makurumula (CCM), jijini Dar es Salaam amesema: “Mimi nime-practice (fanya kazi) maeneo hayo (udiwani na uandishi). Kwenye udiwani mfano, unalipwa posho shilingi laki tatu na nusu, kwa mwaka mnakaa vikao vinne, haiwezekani usifanye kazi.
“Bodi imeshauri sawa ni kwa muda hadi mchakato upite, lakini kwenye sheria katika nafasi ya udiwani inakutaka uwe na shughuli ya kukuingizia kipato."
Mtazamo wa Tamwa
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Joyce Shebe amesema mwandishi kuingia kwenye siasa kutakuwa na athari chanya ikiwa atatoka moja kwa moja pasipo kurudi kwenye tasnia.
Amesema ikitokea mwandishi huyo amekosa na akarudi, apangiwe majukumu mengine ambayo si ya kuzalisha maudhui ili kutengeneza imani ya chombo cha habari kwa jamii.
"Ikitokea amerudi kwenye tasnia, athari hasi kwa huyo mwandishi ni nyingi zaidi. Kwanza kimaadili atatetereka, kuaminika kutashuka.
"Lakini huyo mwandishi ni binadamu kama binadamu wengine. Ana haki ya kugombea kama ambavyo mwalimu, daktari, mchumi na kada nyingine hutoka kwenye taaluma yake na kuingia kwenye siasa."
Amesema changamoto ya taaluma ya uandishi wa habari ni kuwa sauti ya wasiokuwa na sauti, hivyo ikitokea mwanahabari ameingia kwenye siasa kutakuwa na mgongano wa kimaslahi.
Shebe ameshauri vyombo vya habari kuweka utaratibu wa kuwasaidia waandishi wanaoingia kwenye siasa, na kisha kurudi kwenye taaluma, aidha kwa kuwapangia majukumu mengine au vinginevyo, kwa kujiwekea utaratibu kama ambavyo Bodi ya Ithibati imeanza kwa utaratibu wa kuwaondoa kwa muda kwenye majukumu ya habari.
Alichokisema Sungura
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura amegusia njia rafiki ya mwandishi wa habari aliyeingia kwenye siasa anaporejea kazini, basi ajikite kuwa columnist.
Amesema katika machapisho yake, chini ajitambulishe kama mwandishi aliyewahi kugombea au kuwa kwenye chama fulani, itasaidia kuonyesha mgongano wa kimaslahi dhidi yake.
"Vyombo vya habari na wanahabari wakati wa uchaguzi wanawahabarisha wananchi ili wafanye uamuzi kwa usahihi na thamani ya kura. Inapotokea mwandishi anaamua kuwa mwanasiasa, maana yake atazielezea sera za chama anachogombea,” amesema na kuongeza;
"Chama kingine kikileta sera kinyume na chama chake, usawa katika maudhui atakayoandika hautakuwepo. Na hata baada ya uchaguzi ni vigumu kumtenganisha mwanahabari huyo na chama, iwe ameshinda au ameshindwa," amesema.