Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waandishi waaswa kuheshimu usawa wa habari katika kipindi cha uchaguzi

Muktasari:

  • Uchaguzi ni nguzo muhimu ya demokrasia na kwa msingi huo, waandishi wa habari wanabeba jukumu kubwa kuliko hata wanasiasa, wakitakiwa kuwa waamuzi wa haki kwa kuhakikisha mchakato mzima unafanyika kwa uwazi, usawa na kuzingatia masilahi ya wadau wote.

Dar es Salaam. Wakati nchi ikitarajiwa kuingia katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, waandishi wa habari wametakiwa kutenda haki kwa wadau wote wa uchaguzi, na kuhakikisha wanaiacha nchi salama katika mchakato huo.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi Juni 21,2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC).

Profesa Mkumbo amesema kuwa uchaguzi ni kielelezo muhimu cha demokrasia, na kwa msingi huo, waandishi wa habari wanabeba dhamana kubwa kuliko hata wanasiasa, ikiwemo kuwa kama waamuzi (marefa) wa kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa haki, uwazi na uwiano kwa wadau wote.

"Lakini, pia Rais ameshaeleza nia ya kufanya uchaguzi wa haki na kidemokrasia ili kuiacha nchi ikiwa na amani na umoja, hivyo nanyi mnapofanya kazi zenu msisahau Taifa linapaswa kuwa salama na lenye amani," amesema Profesa Mkumbo.

Aidha, amesema kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao, waandishi wa habari wanapaswa kuwa makini na wadau wakuu wawili wakiwamo Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), kwa kuzingatia majukumu na mamlaka yake kisheria, na vyama vya siasa pamoja na wanasiasa, ambao ni sehemu muhimu ya mchakato wa kidemokrasia.

"Mfano Kitila akihutubia leo umeripoti habari yake, akihutubia mwingine ripoti pia. Nasema hivyo kwa kuwa vyama  mpaka sasa hivi nchini vipo  19, hivyo lazima uwatendee haki wote hawa," amesema Profesa Mkumbo ambaye ni Mbunge wa Ubungo.

Akizungumzia kuhusu klabu hiyo ya waandishi, Profesa Mkumbo amewataka kudumisha demokrasia kwa kuwa  bila kufanya hivyo hawatakuwa na nguvu ya kuwazomea  wanasiasa.

Pia, amewataka kuwa wawazi katika matumizi ya fedha kwa kile kilichoingia na kutoka na kushauri ikiwezekana wawe na mkaguzi wao wa ndani ili kuweka mambo hayo sawa.

Katika ujumbe wake kwa waandishi hao, Profesa Mkumbo amesema wanatakiwa wajue kuwa Serikali inawapenda na kuwathamini na tayari imejihakikishia kuwawezesha katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwalinda kama wadau muhimu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa DAR-PC, Bakari Kimwanga amesema kuwa suala la uchaguzi ni la kikatiba, na hivyo wao hawawezi kulizuia.

Ameongeza kuwa ndio maana katika mkutano huo walikuja na kaulimbiu isemayo: “Shiriki Uchaguzi kwa Kuzingatia Misingi na Taaluma,” ili kuhimiza waandishi wa habari kutekeleza wajibu wao kwa weledi na uzingativu wa maadili ya taaluma yao.

Kimwaga alitumia nafasi hiyo pia kumuomba Waziri huyo mwenye dhamana ya uwekezaji kuangalia namna waandishi nao watakavyoshiriki kwa karibu katika uwekezaji.

Aidha Kimwanga pia alitaka awafikishie ombi la kuongezwa walau siku kumi za kujisajili bodi ya Ithibati, kwa kuwa muda uliotolewa ulikuwa mdogo.

"Hata ulipaji wa bili mbalimbali  hufanyika mwisho wa mwezi, hivyo kwa kuwa sisi imekuwa ghafla na tarehe kuangukia katikati ya mwezi tunaomba tuongezewe siku 10 ili ikifika Julai Mosi tunaanza kwa usajili, tunajua nyie mawaziri mnasemezana huko tunaomba utufikishie ombi letu hili," amesema mwenyekiti huyo.

Awali Kaimu Mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Andrew Msechu, akiwasilisha hali ya utendaji wa klabu hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu waingie madarakani akisema, wamefanikiwa kuboresha mifumo ya Tehama ambapo sasa wanachama wanaweza kuhuisha taarifa zao mtandaoni bila kulazimika kwenda ofisini, lakini wapya nao wanaweza  kujisajili huko.

Pamoja na mafanikio hayo amesema bado klabu hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha kama zilivyo taasisi zingine na kuahidi kwamba wataendelea kuzitafutia ufumbuzi.

Naye Mwakilishi wa Umoja wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC), Musa Yusuph amesema kama mlezi wa klabu nchi wamefarijika kuona mkutano huo ukifanyika kwa amani kwa kuwa huko nyuma ilikuwa ni kawaida kusikia uwepo wa migogoro.

"Zamani ukisikia klabu ya Dar ina mkutano, mnajiuliza safari hii nini kinaenda kutokea, mara usikie mtu kafunga ofisi, mara kabadili nywila ya barua pepe ya klabu na mambo mengine,"amesema Yusuph.