MCL, Serikali kujadili uongozi, miundombinu

Muktasari:
- Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Daraja la JP Magufuli ni kielelezo cha uwezo wa Tanzania, kama Taifa kufanya uamuzi na maendeleo yake yenyewe.
Dar es Salaam. Hivi unajua kila Dola moja ya Marekani (Sh2,573.67) inayowekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu, hasa madaraja, huchochea uwekezaji binafsi wa kati ya Dola nne hadi tano (Sh10,294.66 hadi Sh12,868.33)?
Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ya mwaka 2021, uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu hasa ya madaraja, unachochea uwekezaji binafsi na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa.
Ukiacha ripoti hiyo, ujenzi mathalan wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi), utapunguza asilimia 60 ya gharama za usafirishaji kati ya Mkoa wa Mwanza na nchi jirani kama inavyofafanuliwa katika taarifa ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ya mwaka 2023.
Taarifa ya Tanroads inaeleza kabla ya daraja hilo, magari yalilazimika kutumia vivuko kwa muda wa saa moja hadi tatu kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine, lakini sasa, zitatumika dakika nne hadi tano kuvuka.
Kwa sababu ya umuhimu huo, Serikali imeamua kutekeleza mradi wa Daraja la JP Magufuli, ikilenga kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kati ya Mwanza na maeneo mengine jirani kadhalika kukuza uchumi wa nchi.
Katika muktadha huohuo, Wizara ya Ujenzi inashirikiana na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kuratibu Jukwaa la Fikra, linalotarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wakijadili miundombinu na ustawi wa jamii, uongozi unaoleta matokeo na muunganiko wa kitaifa wa ukuaji uchumi.
Hatua ya kufanyika kwa jukwaa hilo inakuja wakati ambao utekelezaji wa mradi wa Daraja la JP Magufuli, umekamilika kwa asilimia 100 na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshalizindua na kuanza kutumika.
Daraja hilo lililogharimiwa na Serikali kwa asilimia 100, lina urefu wa kilomita 3.2, linaunganisha eneo la Kigongo wilayani Misungwi na Busisi, Wilaya ya Sengerema na kukamilika kwake kumerahisisha usafirishaji katika mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera na Kigoma, kadhalika nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Akizungumza kuelekea jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia anasema tukio hilo litafanyika leo Juni 22, 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ikiwa ni siku tatu baada ya uzinduzi wa daraja husika.
Hatua ya kufanyika kwa jukwaa hilo anasema inalenga kuthibitisha uhalisia kuwa, daraja hilo ni alama ya kuunganisha si tu pande mbili za Ziwa Victoria, bali pia watu, mikoa, uchumi na ndoto za Taifa.
"Tukio hili muhimu linafanyika siku tatu baada ya uzinduzi rasmi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo–Busisi), uliofanyika Juni 19, 2025. Hili si daraja la kawaida, ni alama ya kuunganisha si tu pande mbili za Ziwa Victoria, bali pia watu, mikoa, uchumi na ndoto za Taifa letu," anasema Rosalynn.
Mkurugenzi huyo anasema kaulimbiu ya jukwaa hilo mwaka huu ni “Kujenga madaraja, kujenga Taifa: Miundombinu kama kichocheo cha maendeleo jumuishi.”
Kwa MCL, anasema hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa chombo cha habari, si kwa kutoa habari tu, bali kuunganisha jamii na viongozi, kuchochea mijadala ya kitaifa na kufungua milango ya ushirikishwaji wa sera kwa uwazi.
"Jukwaa hili linawakilisha dhamira yetu ya kweli ya Jukwaa la Fikra la Mwananchi isemayo: ‘Kutafuta suluhisho la pamoja’ tunaamini majadiliano ya wazi na jumuishi ni msingi wa maendeleo ya kweli na endelevu," anasema.
Rosalynn anasema MCL inajivunia kuendelea kutekeleza ahadi ya kuliwezesha Taifa kwa maana ya kuwapa Watanzania majukwaa ya kushiriki, kusikika na kuleta mabadiliko kupitia fikra na maarifa.
Katika jukwaa hilo, anasema kutakuwa na hotuba kuu ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega na mijadala mitatu mikubwa.
Mijadala hiyo anasema itahusu miundombinu na ustawi wa jamii, uongozi unaoleta matokeo na muunganiko wa kitaifa na ukuaji wa uchumi.
Anasema washiriki watakuwa viongozi wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za maendeleo, wasomi, wataalamu, vijana na wananchi.
"Karibuni Mlimani City, Dar es Salaam Juni 22 (leo). Karibuni kwenye Jukwaa la Fikra. Kwa wale ambao hawatakuwapo, tutaonyesha tukio hili mubashara kupitia majukwaa yetu yote ya kidijitali ya Mwananchi na The Citizen. Kwa pamoja, tuendelee kujenga daraja la maono, matumaini na mshikamano wa kitaifa," anasema.
Akizungumzia Daraja la JP Magufuli wakati wa hafla ya uzinduzi wake Juni 19, 2025, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alimshukuru Rais Samia akisema wizara yake ilimuomba aridhie daraja hilo liitwe jina la hayati Rais John Magufuli naye akaridhia.
“Wakati unapokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wako daraja hili lilikuwa asilimia 25 tu na zaidi ya Sh152 bilioni zilikuwa zimelipwa, lakini umesimamia mpaka limekamilika kwa asilimia 100 likiwa na thamani ya Sh718 bilioni pamoja na thamani ya kodi, ambapo wewe umeweza kulipa zaidi ya Sh450 bilioni,” alisema Ulega.
Alisema daraja hilo ni kielelezo cha uwezo wa Tanzania, kama Taifa kufanya uamuzi na kufanya maendeleo yake yenyewe.
“Kanda ya Ziwa umeiwekea msisitizo mkubwa wa kiuchumi, sasa inakwenda kuchechemka na vijana watapata ajira… umetuelekeza tuondoe msongamano, Mwanza sasa ina msongamano tutajenga barabara ya njia nne, mbili zinazoingia na mbili zinazotoka. Tupo hatua ya mwisho ya utekelezaji,” alisema.
Watoa mada
Mbali ya Waziri Ulega kuwa mzungumzaji mkuu, jukwaa hilo litakuwa na majopo matatu ya wazungumza wakiwamo viongozi wa Serikali.
Jopo la kwanza litakaloongozwa na Mkurugenzi na Mwanzilishi wa BSM Washauri, Bakari Machumu, wazungumzaji ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Blandina Kilama na Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Jopo la pili litakaloongozwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda wazungumzaji ni Mbunge wa Geita Mjini, Joseph Musukuma, Mjumbe wa Kamati Kuu wa CCM Christopher Gachuma, Katibu Mkuu wa UVCCM Jokate Mwegelo na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.
Jopo la tatu litakaloongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba, wazungumzaji ni Balozi John Ulanga, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, Mkurugenzi wa Sahara Media Group, Anthony Diallo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa.