Safari treni ya SGR Dar -Dodoma kuongezwa, Naibu Spika ashauri

Muktasari:
- Usafiri huo umekuwa tegemeo la watumishi na wafanyabiashara kutokana na muda unaotumika kutoka eneo moja kwenda lingine licha ya tetesi kuwa kuna baadhi ya miundombinu imeanza kuhujumiwa.
Dodoma. Serikali ipo mbioni kuongeza safari za treni ya mwendokasi (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ili kufikia safari nne kwa siku.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Juni 5, 2025 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge, ambapo amesema miongoni mwa safari zinazoongezwa ni treni ya kichwa cha mchongoko.
Hata hivyo, kwa sasa safari za treni hiyo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma ni nne, ila kutoka Dodoma kwenda Dar bado ni tatu.
Waziri Mkuu alikuwa anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Asha Abdallah Juma, maarufu Mshua ambaye ameuliza ni lini Serikali itaongeza safari za treni za SGR kwani zimekuwa ni msaada mkubwa.
Mshua amesema kwa sasa mtu anaweza kulala Dodoma lakini akasafiri kwenda Zanzibar na kisha chai ya jioni akajikuta anakunywa tena Dodoma, jambo ambalo halikuwa rahisi lakini imewezekana.
Waziri Mkuu amesema kinachoangaliwa kwa sasa ni wingi wa watumiaji wa usafiri huo pamoja na mazingira wezesha ya namna wanavyoweza kuratibu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amekiri usafiri huo kuwa ni msaada na mkombozi na kwamba Serikali ililiona hilo tangu ulipoanzishwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli na baadaye Rais Samia Suluhu Hassan na ndiyo maana wameendelea kuimarisha ujenzi wa treni hiyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amemuomba Waziri Mkuu wakaangalie jinsi ya kubadilisha ratiba kwenye muda wa asubuhi wa treni kuondoka Dar es Salaam ili iwe inaingia Dodoma saa 1.30 asubuhi, badala iliyopo sasa ambapo ya kwanza inaingia jijini humo zaidi ya saa 2 asubuhi.
Zungu amesema jambo hilo litasaidia watumishi wa Serikali na wabunge kuwahi shughuli na vikao wanapokuwa nje ya Dodoma, kwani wote wameona usafiri huo ndiyo kimbilio lao la moja kwa moja.