Prime
Vifaa ndani ya SGR vyaanza kuharibiwa

Juni, 2024 baada ya kuanza kwa safari za treni ya mwendokasi (SGR) nilikusanya vijisenti nikaionja bana, maana si kodi zangu bana shwaa nikaingia Morogoro asubuhi, jioni nikarudi kwa raha zangu.
Hata hivyo kulikuwa na tafrani kadhaa ikiwamo siti kugongana yaani unakutana umepewa siti namba mbili na mwenzake anayo hiyo hiyo basi shida tupu.
Foleni nayo ya kuprinti tiketi ilikuwa balaa usipowahi stesheni dude linaondoka bado umepanga foleni hata ya kusubiri karatasi ya tiketi licha ya kuwa uliikata mtandaoni.
Kulikuwa ni vijichangamoto vya hapa na pale ambavyo vilimkera mlipakodi, akiwaza mabilioni ya shilingi yaliyowekwa katika mradi huo kutokana na kodi zake na wengine.

Wakati huo matangazo ya kwenye SGR (PA) yalikera maana watu walikuwa wakibagaza lugha tu, si ya wazungu wala ya kwetu, nafikiri walikuwa wakijisemea tu. Ila utanashati ulikuwa 100 kwa 100. Sasa mambo mengi ni starehe, mabadiliko ni makubwa hivi karibuni niliipanda tena bana, tiketi yako kwa simu ukifika getini wanaskani shwaa, wewe ndani, kidijitali tu kama mwendokasi ya Dar zamani, hamna kuharibu miti tena kama zamani labda kwa atakaye.
Yale mambo ya kugombania siti hivi sasa ni zilipendwa kila mtu ana siti yake, hata wale wahuni waliokuwa wanakata ya tiketi ya Dar – Pugu kwa buku halafu wanapitiliza mpaka Dodoma watakuwa wamepungua sasa hivi maana hamna kisingizo cha tiketi kupandana.
Ukijichanganya kufanya hivyo treni inaweza kufika pale Pungu ikamchukua mwenye tiketi yake kuanzia kituo hicho sasa wewe utaeleza ilikuwaje kuwaje, labda useme ulisinzia umepitiliza, ila sijui kama itasadia.
Hata yale mambo ya limezima, tumekwama dakika/masaa kadhaa siyasikii tena siku hizi itakuwa hali ya umeme nchini imeimarika au wamepata pawabenki.
Matangazo ya kwenye treni sasa hivi i safi kabisa, nafikiri wahudumu wamekumbuka notisi za masomo yao ya ukibinikruu. Hata hivyo kuna mlipakodi mwenzangu juzi nikitokea Dodoma aliniambia amekariri picha mjongeo zote zinazoonyeshwa.
Mwanzoni nilijua ni utani bana akaanza kuniambia baada ya video hii itaonekana hii halafu itafuata ile ya Rais akiwa kwenye treni halafu itafuta hii, na ikawa. Nikamwambia ipo siku nitaandika kwenye sanduku la maoni wawe wanatupa maudhui tofauti tofauti.
Nikawaza hivi treni haziwezi kufungiwa ving’amuzi kama ilivyo kwa mabasi ila nikajisema labda watazindua hiyo huduma siku ya dabi, au spidi yake hairuhusu nikajiuliza mwenyewe bila majibu.
Kwa ujumla huduma ndani ya treni zinaimarika kila leo isipokuwa za msongamano stesheni husuani Dar jioni, ila kwakuwa bado safari za Mwanza na kwingineko hazijaanza labda panatosha, zikianza watajenga stesheni nyingine au kuongeza ngazi sijui.

Enewei, kama nilivyoelezea uzuri wa ndani ya treni siku niliyojichanganya leo nitazungumzia tena nilichokishuhudia katika safari zangu hivi karibuni ikiwa ni karibu mwaka mmoja tangu kuanza kwa safari SGR.
Usafi ndani ya treni na unadhifu wa wahudumu wa wahudumu viwango vimeendelea kuwa vilevile, Kudosi (tiki ndefu) isipokuwa wakati mwingine kunakuwa na uchelewaji kidogo wa kukusanya uchafu baada ya kutoa huduma ya chai na vitafunwa.
Hata hivyo hii ni kero kwenye mabehewa ya watu wa uchumi wa chini ambayo nafasi zake zimebanana lakini kule kwa mabwanyenye mambo safi, labda sababu ya uchache wa watu lakini pia haikeri kwa kuwa meza ni kubwa.
Kilichomsikitisha mlipakodi zamu hii ni kuona SGR yake wameshaanza kuivunja na mbaya zaidi inavunjwa na walipa kodi wenyewe badala ya kulinda kodi zao wanazozilipa kwa taabu na wakati mwingine kwa manung’uniko makubwa.
Kama kawaida yangu nikiingia kwenye SGR huwa lazima nivute tule tumvinyo twangu walau tuwili hivi. Nimeagiza kamekuja ka kwanza nimefungua tu nikataka nikatundike pale pa kuweka vinywaji kuangalia hivi, walipakodi washavunja.
Nikaangalia kwa jirani yangu nako tayari pamevunjwa basi ikabidi nishikilie muda wote uzuri kalikuwa ni ka kwanza na siku hiyo mchana sikugusa vitu kabisa hivyo mikono ilikuwa bado ina nguvu za kutosha.
Uzuri treni ilikuwa hiana watu wengi kuna mshikaji wangu aliniambia yuko namba saba nikatoka namba tano nikaenda walau tupige stori maana aliniambia katika kiti cha wawili yuko peke yake.
Ili kufikia namba saba kwakuwa nilikuwa nimekaa nyuma ikabidi nikatishe behewa langu lote (namba 5) nikakatiza namba 6 kisha nikaingia namba 7, njiani niliona viti kadhaa vina hali kama ile ya kwangu.
Nikamwambia huyo mshikaji wangu ngoja kuna kitu niangalie nikatembea mpaka namba 10 nikawa naangalia hali ya viti nikagundua vingi vimevunjwa, nikasikitika sana nikajua labda nimepanda treni isiyo ya wastaarabu, wakati wa kurudi nitapanda ya jioni.
Bana wewe mambo ni yale yake, ziadi nikawa na jicho la kuangalia hali ya kodi zangu nikagundua kuwa na kuta za hivyo vitu zimejaa mikwaruzo pengine ni yale madude yao wanayosukumia vinywaji na vitafunwa.
Lakini nikasema siku nikipanda ndege nitaangalia nao kama viti vyao vina mikwaruzo, mpaka leo sijabahatika kupanda ila kuna binamu yangu anafanya kazi kwenye kodi zetu za angani nikampigia simu nikamuuliza vipi akanitumia picha akaniambia huku hamna mikwaruzo.
Nikawaza yale madude sio saizi husika au yamechongwa kienyeji kiasi cha kuacha mikaruzo lakini akili nyingine ikaniambia labda angani hakuna mtikisiko sana kama standadi geji Dar – Dodoma.
Yaani watu wanavunja kodi zao bila kujali wala uchungu, tena kila sehemu pameelekezwa uzito na matumizi yake sahihi hata sehemu ya kutundika koti kuna maelekezo mahususi, meza imeandikwa na kuelekezwa watu wasilale ila huwa wanaupiga pale hata hawaogopi kuvunja.
Akili ikaniambia nenda ofisi kuu chapu uone hali yake, lakini katika mabehewa kadhaa niliyooingia nilikuta ofisi hizo bado zimetunzwa vizuri, sinki zimepoteza tu hali ya upya lakini hakuna kuharibika.
Nawakumbusha tu hizo treni zimegharimu mabilioni ya shilingi za nchi yetu ambazo zinatokana na kodi zetu, kuharibu treni ni sawa na kuchukua kumi alfu yako uliyoipata kwa taabu kisha ukaichana chana.
Tusichane bana kumi afu zetu tuzitunze vizuri maana dude hilo tulikichakaza hatutajivunia kodi zetu lakini pia serikali itachukua kodi zetu kwenda kutengeneza, na hata ikibidi ikikosa pesa za kufanya hivyo haiwezi kutekeleza matrilioni ya mradi huo itachimba hata mfukoni kwetu (itatoza kodi zaidi).
Walipakodi wenzangu, tuchunge kodi zetu, ni kodi nyingi zile, tusipovunja tutanufaika zaidi, tukivunja tutakuwa tunajichoma wenyewe. Waendeshaji wazidi kuboresha huduma nasi tuutunze mali yetu.
Eeeehhh nilikuwa nimesahau hili, siku ukipatwa na behewa ambayo limekodiwa na wafunzi wa wana kikoba fulani na wamekula vitu kidogo, aisee utajuta, hata ukitoa taarifa wahudumu ni kama hawana mwongozo wowote wa kudhibiti hilo, unaweza kuhisi umedharauliwa.
Mambo ni mawili tu upate hasira utukane hovyo hovyo, au uamue uitishe kinywaji kilichochangamka ili na wewe uchangamke, ukere wengine ambayo walijua kwenye SGR kuna utulivu. Nafikiri hivi karibuni kutakuwa na kanuni maana kuna mmama mmoja baada ya kuwa nimechangamka nilimkera kwa kelele na kausingizi kake nusu anipe laana.