Mbunge ataka udhibiti unywaji pombe treni za usiku SGR

Mbunge wa Viti Maalumu, Mwantum Dau Haji, ameitaka Serikali kuchukua hatua za kudhibiti unywaji wa pombe ndani ya treni za Reli ya Kisasa (SGR), hususan zile zinazofanya safari za usiku, akisema hali hiyo inahatarisha utulivu na usalama wa abiria.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Alhamisi, Mei 15, 2025, Mwantum amesema kuwa wakati sigara imepigwa marufuku ndani ya treni hizo, pombe bado inaruhusiwa kunywewa waziwazi na kwa wingi.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi natembelea sana treni, natoka hapa naingia treni ya mchana jioni. Lakini ukiingia treni ya usiku, unaambiwa uvutaji wa sigara hauruhusiwi, lakini pombe inanywewa hadharani na inakuwa halali. Sijui kama Serikali inalijua hili au vipi,” amesema.
Mbunge huyo ameongeza kuwa unywaji wa pombe ndani ya treni unatishia amani ya safari, hasa kwa wanawake na familia wanaosafiri kwa kutumia huduma hiyo.
“Tunapendeza wenyewe tukikaa mle, vichwa vinaitika, usingizi unakuja, lakini sasa hivi pombe zimezidi. Ni bora Waziri akakaa kitako na timu yake, awaambie hawa wanaotoa huduma waangalie hili suala,” amesisitiza.