Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walichokubaliana Rais Samia, Chapo wa Msumbiji

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Daniel Chapo wa Msumbiji wamezungumzia masuala mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi, miundombinu na usafirishaji.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uhusiano imara wa kidiplomasia na kihistoria kati ya Tanzania na Msumbiji hauakisi ushirikiano na uhusiano wa kiuchumi uliopo kati ya mataifa hayo.

Kwa kutambua hilo, amesema mataifa hayo yamekubaliana kushirikiana kutafuta mbinu za kurahisisha ufanyaji biashara kati ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kwa lengo la kukuza uchumi.

Sambamba na hilo, amesema wamekubaliana kuwa na vituo vya pamoja katika mipaka ya mataifa hayo, ikiwa ni sehemu ya hatua ya kufanikisha kuimarisha kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo.

Mkuu huyo wa nchi, ameyasema hayo leo, Alhamisi Mei 8, 2025 katika mkutano na wanahabari saa chache baada ya mazungumzo ya ana kwa ana kati yake na Rais Daniel Chapo wa Msumbiji, ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia jana.

"Tumekubaliana licha ya ujirani na uhusiano mzuri wa kihistoria tulionao, bado ushirikiano wa kiuchumi haujaenda sambamba na ushirikiano wa kidiplomasia," amesema Raia Samia.

Katika hilo, amesema wamekubaliana kushirikiana kurahisisha mazingira ya biashara kuwafanya wafanyabiashara wawe huru pande zote na hivyo kukuza uchumi.

Amesema ili kufanikisha hayo, wamekubaliana kuwa na vituo vya pamoja katika mipaka ya mataifa hayo, kadhalika kuanzisha tume ya pamoja ya kiuchumi na itakayofuatilia makubaliano ya ushirikiano ili kukuza uchumi haraka kwa pande zote.

"Uhusiano wa kiuchumi unakuzwa na kuimarika kwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji na tumekubaliana kujenga miundombinu yetu ya mipakani inayounganisha nchi zetu," amesema.

Hata hivyo, amesema Mei 6, mwaka huu, mawaziri wa mataifa hayo walikutana kujadili kuhusu miradi mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi wa pamoja.

Katika kikao chake na Rais Chapo, Rais Samia amesema amemweleza kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na baadaye ataitembelea baadhi ukiwamo SGR.

Ameeleza Tanzania na Msumbiji zimebarikiwa kuwa na utajiri wa gesi na katika kikao chao wamezungumza umuhimu wa kubadilishana uzoefu na kufanya tafiti za pamoja.

Kuhusu fursa za uchumi wa buluu, amesema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya rasilimali.

Kwa kutamba kuwa uchumi unategemea kilimo, amesema wamekubaliana kubadilishana uzoefu na kufanya tafiti za pamoja katika Kilimo hasa cha korosho.

Sambamba na hayo, amempongeza Rais Chapo kwa ushindi wake katika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana nchini Msumbiji, pia amemshukuru kwa hatua ya kukubali mwaliko wa kutembelea Tanzania.

"Tanzania na Msumbiji ni ndugu wa damu ndio maana jamii za wamakonde, wamakua na wayao wanapatikana pande zote na haishangazi kuona tamaduni zinafanana," amesema.

Amesema uhusiano wa mataifa hayo, uliimarishwa na waasisi wa mataifa hayo kwa kufanya kazi kwa karibu enzi za harakati za ukombozi.

Amesema Frelimo ilizaliwa mwaka 1962 jijini Dar es Salaam na Tanzania ilisaidia kuhakikisha Msumbiji inapata uhuru.

Amesema Msumbiji inatarajia kutimiza miaka 50 ya uhuru wake na kwamba Tanzania imealikwa kuhudhuria na kwamba itakwenda.

Kwa mujibu wa Rais Samia, wamejadiliana kuhusu amani, usalama na utengamano wa Bara la Afrika na wamekubaliana kuwa na masuala ya pamoja kukabili uhalifu.


Alichokisema Rais Chapo

Kwa upande wa Rais Chapo, amesema hiyo ni ziara yake ya kwanza akiwa na wadhifa huo, kwani awali alikuja nchini akiwa mgombea na wakati huo ilikuwa nchi ya kwanza kutembelea.

Amesema aliahidi kuwa baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Msumbiji angekuja Tanzania na tayari ameshatimiza ahadi hiyo.

Ameeleza ziara hiyo inaenga kukuza mahusiano ya kihistoria kirafiki na kindugu yaliyokuwepo kati ya mataifa hayo.

"Mahusiano ya kisiasa kati ya Tanzania na Msumbiji ni mazuri na ya pekee, pia kuna uhusiano kwenye ulinzi na usalama.

"Tumekubaliana kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika uchumi wa buluu na kesho tutatembelea Zanzibar ili kushirikiana katika sekta ya utalii na uchumi wa buluu," amesema.

Amesema watashirikiana katika maeneo ya kilimo, madini na nishati na kwamba Msumbiji ina utajiri mkubwa katika madini na kuna haja nchi hizo zishirikiane kwa ajili ya watu na ukanda kwa ujumla.

Rais Chapo amesema wamezungumza haja ya kuanzisha Jumuiya ya nchi zinazozalisha korosho na biashara, kadhalika uwekezaji wa pamoja.

Amesema Juni 15, mwaka huu wataadhimisha miaka 50 na Septemba mwaka jana walizindua mwenge wa uhuru na huo ni uzoefu wa kwanza unaolenga kuwaleta pamoja Wanamsumbiji.

Rais Daniel Chapo aliapishwa Januari 15, 2025, baada ya kushinda wadhifa wa urais katika uchaguzi mkuu wa uliofanyika Oktoba mwaja jana, kupitia chama cha Frelimo.

Katika uchaguzi huo, Chapo alishinda kwa asilimia 70.67 akimshinda mgombea binafsi, Venancio Mondlane aliyepata asilimia 20.3 ya kura zote.

Ushindi wa Chapo, umenifanya Frelimo ambacho ni chama rafiki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Tanzania, kushinda uongozi wa Taifa hilo kwa zaidi ya miaka 49 tangu Msumbiji ilipopata uhuru mwaka 1975.

Pamoja na mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan, Chapo ametembelea mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na visiwani Zanzibar ikiwa ni sehemu ya ziara yake.

Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Chapo nje ya Taifa lake, tangu aukwae wadhifa wa urais wa Msumbiji.


Mikataba iliyosainiwa

Katika hafla hiyo, mikataba miwili itasainiwa na hati za makubaliano nne kati ya Tanzania na Msumbiji.

Mikataba hiyo ni ule wa Uwili kati ya Tanzania na Msumbiji kuhusu uanzishwaji wa Kituo Cha Forodha cha Pamoja (OSEP).

Pia, Mkataba wa kubadilishana wafungwa kati ya Tanzania na Msumbiji.

Kadhalika, ilisainiwa hati ya makubaliano kubadilishana wanafunzi kati ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ya Tanzania na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Maendeleo ya Jamii ya Msumbiji.

Hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji kuhusu masuala ya utamaduni, hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba nchini (TMDA)  na Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Madawa ya Msumbiji na hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya TBC na Redio Msumbiji.