Mkuu wa mashtaka ICC ang’olewa akituhumiwa utovu wa maadili
Aliyekuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Khan
Muktasari:
- Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya ICC, Karim Khan, ameondolewa madarakani baada ya uchunguzi wa tuhuma za mwenendo usiofaa akituhumiwa ukatili wa kingono na matumizi mabaya ya madaraka, licha ya yeye kukanusha na kuahidi kupinga uamuzi huo.
Dar es Salaam. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), imeandika historia mpya baada ya nchi wanachama wake kumuondoa madarakani Mwendesha Mashtaka Mkuu, Karim Khan kufuatia uchunguzi uliobaini kile kilichoelezwa kuwa ni utovu mkubwa wa maadili na ukiukaji wa wajibu wake.
Uamuzi huo ulipitishwa Ijumaa, Julai 24, 2026, katika kikao maalumu cha Assembly of States Parties (ASP), kilichofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, Marekani, ambapo nchi wanachama zilipiga kura kuidhinisha hatua hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya ICC, uamuzi huo umetokana na hitimisho la uchunguzi ulioeleza kuwa Khan alikiuka maadili na wajibu wa ofisi yake baada ya kudaiwa kuingia katika uhusiano usiofaa na mfanyakazi wa ngazi ya chini wa mahakama hiyo na baadaye kujaribu kuzuia malalamiko yaliyowasilishwa dhidi yake.
Hata hivyo, Khan mwanasheria kutoka Uingereza ambaye alichaguliwa kuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa tatu wa ICC mwaka 2021, ameendelea kukanusha tuhuma hizo tangu zilipoibuka.
Kupitia mawakili wake, alisema atapinga uamuzi huo kwa kutumia njia zote za kisheria zinazopatikana.
"Nitapinga uhalali na usawa wa uamuzi huu kupitia njia zote za kisheria zinazopatikana," alisema Khan.
Tuhuma zilivyoanza
Madai dhidi ya Khan yalianza mwaka 2024 baada ya mfanyakazi wa ngazi ya chini wa ICC kuwasilisha malalamiko yaliyohusu madai ya mwenendo usiofaa wa kingono.
Awali, suala hilo lilichunguzwa na Kitengo Huru cha Usimamizi cha ICC (Independent Oversight Mechanism), lakini uchunguzi huo ulisitishwa baada ya mlalamikaji kutoshiriki kikamilifu katika mchakato.
Baadaye, Oktoba 2024, kesi hiyo ilikabidhiwa kwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Usimamizi wa Ndani (OIOS), ambayo iliendesha uchunguzi wa kina uliohusisha mahojiano na ukusanyaji wa ushahidi hadi Desemba 2025.
Baada ya uchunguzi huo kukamilika, taarifa iliwasilishwa kwa vyombo husika vya ICC, kabla ya kutathminiwa na jopo la majaji watatu waliokuwa na jukumu la kubaini kama mwenendo uliodaiwa ulifikia kiwango kinachoweza kusababisha kuondolewa madarakani kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.
Kifungu cha 46 cha Mkataba huo kinaruhusu viongozi wakuu wa ICC kuondolewa iwapo watapatikana na utovu mkubwa wa maadili, ukiukaji mkubwa wa wajibu au kushindwa kutekeleza majukumu yao. Aidha, kifungu hicho kinamtaka mhusika kupewa nafasi ya kujitetea kabla ya uamuzi wa mwisho kufikiwa.
UN yasema ICC ni taasisi huru
Umoja wa Mataifa, ambao ulikuwa mwenyeji wa kikao hicho, ulisisitiza kuwa haukuhusika katika uamuzi huo.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema ICC ni taasisi huru ya kimahakama na masuala yanayohusu uongozi wake yanapaswa kushughulikiwa na nchi wanachama kwa mujibu wa Mkataba wa Roma.
Kwa upande wake, Shirika la Human Rights Watch limesema hatua hiyo imeonyesha kuwa uwajibikaji unapaswa kutekelezwa kwa wote, bila kujali nyadhifa zao.
"Uamuzi huu unaonesha kuwa hakuna aliye juu ya uwajibikaji," amenukuliwa akisema Mkurugenzi wa Haki za Kimataifa wa shirika hilo, Liz Evenson.
Wakati huo huo, hatua hiyo inatajwa kupokelewa kwa mtazamo chanya na baadhi ya mataifa yaliyokuwa yakikosoa ICC, yakiwemo Marekani, ambayo si mwanachama wa mahakama hiyo. Marekani hapo awali iliweka vikwazo dhidi ya ICC na baadhi ya maofisa wake kufuatia uchunguzi wa madai ya uhalifu wa kivita unaowahusu maofisa wa Israel katika vita vya Gaza.
Nini kinafuata?
Kuondolewa kwa Khan hakufuti maamuzi yaliyokwisha kufanywa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wala hati za kukamatwa na uchunguzi uliokwishaidhinishwa na majaji wa ICC.
Kwa mujibu wa utaratibu wa mahakama hiyo, maamuzi hayo yanaendelea kuwa halali kwa sababu yanatokana na mamlaka ya majaji wa ICC, si ya Mwendesha Mashtaka Mkuu binafsi.
Kwa sasa, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka itaendelea kuongozwa na manaibu wa mwendesha mashtaka hadi mchakato wa kumpata mrithi wa Khan utakapokamilika.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Roma, Mwendesha Mashtaka Mkuu mpya atachaguliwa na Assembly of States Parties kupitia kura ya siri. Mgombea atatakiwa kuwa na sifa za juu za kitaaluma na maadili, uzoefu mkubwa katika sheria za jinai na mashtaka, pamoja na uwezo wa kutumia angalau moja ya lugha rasmi za kazi za ICC, ambazo ni Kiingereza au Kifaransa.
Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema mrithi wa Khan atakabidhiwa jukumu katika kipindi ambacho ICC inaendelea kukabiliwa na changamoto za kisiasa, ikiwemo ukosoaji kutoka baadhi ya mataifa makubwa na mjadala kuhusu nafasi ya mahakama hiyo katika kusimamia uwajibikaji wa uhalifu wa kimataifa.