Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maji yaliyojaa kivuko cha SGR yaanza kuondolewa

Mafundi wakiwa wanaendelea na kazi ya kuchimba mfereji wa kuelekeza njia asili ya kupita maji.

Muktasari:

  • Ili kuweza kuvuka eneo hilo, wananchi hulazimika kulipa kati ya Sh500 hadi Sh1000, huku wanaotumia bodaboda wakilipia Sh2,000 umbali ambao wangelipa Sh1,000 kutokana na mzunguko wa safari.

Dar es Salaam. Maji yaliyokuwa yakituama katika kivuko kinachotumiwa na wananchi kwenye reli ya Umeme (SGR), maeneo ya Gongo la Mboto jijini humo yameanza kuondolewa.

Hivi karibuni Mwananchi Digital iliripoti kuhusu changamoto ya kujaa maji katika eneo hilo na adha wanayoipata wananchi kupita kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Ili kuweza kuvuka eneo hilo, mwananchi hulazimika kulipa kati ya Sh500 hadi Sh1,000 ili kubebwa na vijana waliojiajiri katika kuifanya kazi hiyo, huku wanafunzi wakilipishwa Sh200.

Siku moja baada ya kuripotiwa kwa hali hiyo Mwenyekiti Serikali za Mitaa wa Gongo la Mboto wake, Moshi Mwaluko, alieleza kuchukua hatua ya kushughulikia tatizo hilo, ambapo Mtaa uliandika barua kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuomba Sh8.9 milioni kwa ajili ya kuyaondoa maji hayo.

Leo Jumanne Aprili 22, 2025, Mwananchi ilifika katika eneo hilo na kukuta mafundi wakiwa wanaendelea na kazi ya kuchimba na kuyaelekeza maji hayo kwenye njia yake asili ambayo awali ilikuwa imezibwa.

Maji yakionekana kupungua ukilinganisha na mwanzo.

Pia, bodaboda ambazo awali zilikuwa haziwezi kupita, sasa zinapita zikiwa zimebeba abiria na maji kuonekana kupungua kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza na Mwananchi, Mwaluko amesema kazi hiyo ilianza tangu Ijumaa wiki iliyopita baada ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuidhinisha fedha walizoomba za kuifanya kazi hiyo.

“Hii kazi inayoendelea ni baada ya Gazeti la Mwananchi kuripoti kadhia hii ya maji kutuama, ambapo TRC ilichukua hatua ya haraka wakatusaidia kutupa fedha tuliyoomba.

“Ni kutokana na kazi hiyo, mpaka sasa maji zaidi ya asilimia 80 yaliyokuwa yametuama hapa yametoka, kwa kweli tunashukuru,” amesema Mwaluko.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo amesema mpango uliopo ni kujengwa kwa daraja la kudumu kwa kuwa njia hiyo siyo ya kudumu na wanaamini TRC italifanya hilo kwa haraka.

Wakizungumzia hatua hiyo, baadhi ya wananchi, akiwemo Veronika Mbawala amesema hali ya kujaa maji ilikuwa ikiwaathiri wajasiriamali, kwani pamoja na mizigo yao ilibidi walipe Sh1,000 ili kubebwa mgongoni na kuvushwa eneo hilo.

Amesema hatua ya kuondolewa maji sasa itawasaidia, kwa kuwa walikuwa wakipata tabu kuvuka.

Naye Kevin Venance, mwendesha bodaboda amesema maji hayo yalikuwa yakiwasumbua kwani sehemu ya kwenda Sh1000 ilibidi wawalipishe watu Sh2,000, kwa kuwa ilibidi kuzunguka kwa kupita barabara nyingine.

“Pia kwa miezi zaidi ya mitano maji haya kutuama, ilifika mahali yakawa yanatoa harufu, jambo ambalo ni hatari kwa afya za watu,” amesema.

Wenye bodaboda na baiskeli wakiwa wanapita katika kivuko.

Msimamizi wa mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Thadei Paul amesema wanachokifanya katika kazi hiyo ni kujenga mfereji wa maji ambao unatokea chuo cha Kampala na kuelekeza maji kwenye njia yake asili.

Kuhusu kivuko cha kudumu, amesema hivi karibuni changamoto hiyo itatatuliwa kwa kuwa mkandarasi tayari ameshakabidhiwa eneo kwa ajili ya kuanza kazi.