TRC, ofisi ya mtaa wachukua hatua kivuko cha SGR kujaa maji

Muktasari:
- Katika kuvuka eneo hilo, wananchi hulazimika kulipa Sh500 hadi Sh1,000 ili kubebwa na vijana waliojiajiri kuifanya kazi hiyo huku wanafunzi wakitozwa Sh200.
Dar es Salaam. Kutokana na kujaa maji katika karavati ambalo wananchi wanalitumia kama kivuko kupita kwenye reli ya umeme (SGR) maeneo ya Gongolamboto jijini Dar es Salaam Shirika la Reli Tanzania (TRC) na ofisi ya serikali za mitaa wamechukua hatua kushughulikia tatizo hilo.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 15, 2025 na mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Gongolamboto, Moshi Mwaluko alipozungumza na Mwananchi iliyotaka kujua ni hatua gani imezichukua katika kushughulikia kero hiyo.
Hatua hii inakuja ikiwa ni siku moja imepita tangu Mwananchi kuonyesha kwa picha mnato na mjongeo namna wananchi wanavyopata adha ya kupita eneo hilo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Katika kuvuka huko, wananchi hulazimika kulipa Sh500 hadi Sh1,000 ili kubebwa na vijana waliojiajiri katika kuifanya kazi hiyo huku wanafunzi wakilipishwa Sh200.
Akieleza hatua walizochukua, Mwaluko amesema jana Aprili 14, 2025, wameiandikia TRC barua ya kuomba fedha kwa ajili ya kuondoa maji eneo hilo ambalo ndio tatizo kubwa.
Mwenyekiti huyo amesema baada ya kukaa chini na kupiga hesabu wamebaini bajeti nzima ya kutatua kero hiyo ni Sh9 milioni ambapo TRC imeahidi itawapatia Sh8.9 miloni huku nyingine ziliziobaki zitatolewa na ofisi ya mtaa kwa kushishirikiana na ofisi ya Diwani na ile ya Mbunge.
Amesema tatizo lililopo eneo hilo imesababishwa na namna eneo hilo lilivyokosewa kujengwa ambapo upande ambao maji yalitakiwa yaelekee kumeinuka hivyo kufanya mvua zinaponyesha maji kusimama kwa muda mrefu huku mengine yakielekea kwenye makazi ya watu.
Hata hivyo, alipoulizwa haoni ni hatari watu kuendelea kutumia eneo hilo wakati kuna sehemu imekatwa waya kwa ajili ya watu kuvuka, Mwaluko amesema:”Unajua tena tabia za binadamu, utamfanyia hiki, kesho atadai hiki, lakini pamoja na yote lile eneo kama maji yatatolewa hapana shida kupita kwa kuwa pameanza kutumika muda sasa.”
Kuandikwa kwa barua hiyo kumemethibitishwa pia na Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Habari wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Fredy Mwanjala ambaye amesema fedha hizo wanatarajia kuzitoa ndani ya siku chache zijazo.

Hata hivyo, amewasihi wananchi kutumia vivuko vilivyowekwa kwa kuwa vyote wanavyoviona vimewekwa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wakiwemo Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (Tarura).
“Haya malalamiko ya kuwa vivuko vipo mbali yako maeneo yote ambapo reli hiyo imepita, lakini tunajitahidi kutoa elimu kwa wananchi kila inapobidi na kufuata ushauri wa wataalam wetu ili kuona mradi haugeuki kuwa kero kwa watu.
“Kwani hata hilo eneo la karavati wanalotumia wananchi kuvuka halikuwa rasmi ila ni wananchi wenyewe walilikata na kupafanya kuwa rasmi,” amesema Mwanjala.
Walichosema wananchi
Baadhi ya wananchi waliozungumzia hali hiyo akiwemo Marina Chali, mkazi wa Ulongoni amesema sehemu hiyo imekuwa kero kwa muda mrefu tangu reli hiyo ilipojengwa.
Marina amesema shida wanapata zaidi wanawake haswa wenye watoto pindi wanapotoka kwenye shughuli zao za kujitafutia riziki au kufuata huduma upande wa Gongolamboto ikiwemo hospitali.
Angle Thomas mkazi wa Kisarawe, amesema karavati hilo limekuwa kimbilio la wengi kutokana na ukaribu wa kutokea kituo cha kupanda treni pindi wanapotaka kwenda mjini na kilichowekwa karibu na kituo Kipya.
“Pia karavati hili ni mwokozi kwa wale wanaokwenda kuunganisha usafiri wa daladala wakishuka na treni kuelekea Kisarawe, Chanika, Kigogo na maeneo ya Majohe ambapo baadhi ya daladala za Chanika na Kisarawe huwa zikiegeshwa hapo na hivyo kupata urahisi wa usafiri.

Musa Chuma, mkazi wa Gongolamboto anayefanya biashara ya kuuza nyama, amesema kwa wanaotoka Pugu imekuwa njia rahisi, kwa kuwa kuna bajaji zinazoishia hapo zikitokea mnadani Pugu.
“Hiki kivuko kwetu kimekuwa mwokozi, kwani kabla ilitulazimu kukodi bodaboda hadi Sh3000 kutokea mnadani, lakini sasa hivi Sh1000 tu unafika na hivyo kuokoa gharama,” amesema Chuma.
Walichokisema vijana wanaowavusha
Vijana ambao wamejiajiri kutokana na kero hiyo, wamesema kwao hawatamani mvua wala maji yaishe eneo hilo kwa kuwa ni eneo linalowasidia kuingiza kipato.
Steven Robert, amesema kwa siku huondoka na hadi Sh60,000 na wengine wamelazimika kuacha kazi zao za ujenzi na kuifanya kazi hiyo.
Ally Hassan anasema kuna wakati maji hayo yanakuwa mengi yanafika hadi kiunono na hapo ndipo hupandisha bei na kufika hadi Sh1000 kwa kila mtu huku siku za kazi ndio haswa wanapata hela nyingi.
“Kiukweli hutakiwi kufurahia watu wakipata matatizo, lakini kwa hili sisi tunaona sawa kwa kuwa linatusaidia nasi tuingize hela,” amesema Hassan.