Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Latra yawaweka njiapanda watoa huduma tiketi mtandaoni

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Kanuni za Tiketi Mtandao za mwaka 2024 zilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 20 la Desemba 1, 2024, mifumo yote ya tiketi inayotaka kufanya kazi nchini inatakiwa kupata kibali kutoka Latra.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imeweka bayana hatima ya watoa huduma wa mifumo ya tiketi mtandao kwa kuwagawanya katika makundi kulingana na hatua ya utekelezaji wa masharti ya kisheria.

Kwa mujibu wa Kanuni za Tiketi Mtandao za mwaka 2024 zilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 20 la Desemba 1, 2024, mifumo yote ya tiketi inayotaka kufanya kazi nchini inatakiwa kupata kibali kutoka Latra.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Julai 2, 2025 na  Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra, Salum Pazzy imeeleza kuwa kibali hicho hutolewa baada ya muhusika kukidhi vigezo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuwa na mfumo wenye ulinzi dhidi ya uvamizi wa kimtandao na uwezo wa kuunganishwa na mifumo ya Serikali.

“Mpaka Juni 30, 2025, kampuni tatu za mifumo ya tiketi mtandao tayari zimefanikiwa kukamilisha masharti yote muhimu na kuruhusiwa kufanya malipo ya vibali vyao,” amesema Pazzy.

Amesema kampuni hizo ni Ottap Agency Company Limited, Hashtech Tanzania Limited na Iyishe Company Limited ambapo amesisitiza baada ya kampuni hizo kukamilisha malipo, zitakabidhiwa vibali vya kutoa huduma za tiketi mtandao.

Pazzy amesema kampuni nyingine sita zimeonekana kuwa katika hatua nzuri lakini bado zina changamoto ndogondogo za kiufundi na kisheria. Hivyo, Latra imewapa siku 14 tu kuanzia Julai 1, 2025 kuhakikisha zinakamilisha masharti yaliyobaki.

Ametaja kampuni hizo ni AB Courier Express Limited, Busbora Company Limited, Logix Company Limited, Mkombozi Infotech Company, Sepatech Company Limited na Web Corporation Limited,  endapo hazitakamilisha matakwa hayo ndani ya muda huo, hazitaruhusiwa kuendelea kutoa huduma za tiketi mtandao.

Tofauti na kundi hilo, kampuni mbili zimeingia katika mtego wa mwisho wa onyo baada ya kubainika kuwa na changamoto kubwa zinazowakosesha sifa za msingi kabisa za kutoa huduma hizo.

Latra imezipa kampuni Duarani Innovative Company na Itule Company siku saba za matazamio kuhakikisha zimekamilisha matakwa muhimu la sivyo zitafungiwa rasmi.

“Baada ya muda huo uliotolewa kupita, ukaguzi wa mifumo yote utaanza mara moja na yeyote atakayebainika kutoa huduma bila kibali halali hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema.

Amesema wateja wataelekezwa kuhamia kwa watoa huduma waliotimiza vigezo ili kuepuka usumbufu wowote utakaojitokeza.

Latra imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ikishirikiana na wamiliki wa mifumo ya tiketi na wataalamu wa Serikali kuhakikisha mifumo yote inaunganishwa na tiketi mtandao wa Mamlaka (UTS) pamoja na mfumo mkuu wa tiketi (CeTS).

Amesema lengo kuu ni kuhakikisha taarifa zote za mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani zinaonekana kwa uwazi kwenye mfumo huo na abiria wanapata huduma kwa urahisi, usalama na kwa njia ya kisasa.

Mamlaka imewataka wasafirishaji na watumiaji wa usafiri kutumia mfumo rasmi wa Latra unaowawezesha abiria wa reli ya kisasa (SGR), Reli ya Kati (MGR) na mabasi kujiwekea tiketi popote walipo kwa njia ya simu janja au kompyuta.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo amesema wao walipeleka kampuni nne za ukatishaji tiketi waliotakiwa kufanyiwa mchujo na Latra.

“Wakati tunaanza utaratibu wa kukata tiketi tulitoa zabuni na tukapata kampuni nne ambazo tuliziwasilisha Latra moja wapo ikiwa ya Ottap hizo nyingine ambazo zimekuwa na changamoto itakuwa waliomba kwa wenyewe,” amesema Mwalongo.

Amesema muhimu hizo kampuni kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa na Latra ili kuondoa usumbufu kwa abiria.