Latra kutangaza watoa huduma wa tiketi mtandaoni walioidhinishwa

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Latra, watoa huduma ambao mfumo wao wa tiketi mtandao hausomani na mifumo ya Serikali hawataruhusiwa kuendelea na shughuli wanazofanya
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) inatarajiwa kuanzia kesho Julai mosi, 2025 kutangaza orodha ya watoa huduma wa tiketi mtandao wa mabasi waliofanikiwa kuunganisha mfumo wao na wa Serikali.
Kwa mujibu wa Latra, watoa huduma ambao mfumo wao wa tiketi mtandao hausomani na mifumo ya Serikali hawataruhusiwa kuendelea na shughuli wanazofanya.
Hatua hii inakuja baada ya Latra kutoa notisi ya miezi miwili ikiwataka watoa huduma wote wa tiketi mtandaoni kuunganisha mifumo yao na Mfumo wa Tiketi za Usafiri wa Latra pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Mashine za Kielektroniki za Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (EFDMS) kabla ya Julai mosi, 2025.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Latra, Salum Pazzy amesema timu ya wataalamu inaendelea kukamilisha uhakiki wa watoa huduma waliokidhi vigezo.
“Huduma za mabasi zitaendelea kama kawaida, lakini kuanzia leo tutachapisha orodha ya watoa huduma waliothibitishwa. Orodha hii itasambazwa kwa waendeshaji wa usafiri, kampuni zilizotambuliwa pekee ndizo zitakazoruhusiwa kutoa huduma za tiketi mtandaoni,” amesema.
Pazzy amesema ni watoa huduma wachache hadi sasa ndio wamekamilisha usajili na kuunganisha mifumo yao na mifumo ya Serikali.
Amesema utekelezaji wa agizo hilo ni sehemu ya mwendelezo wa usimamizi wa kanuni za tiketi za kielektroniki za Latra za mwaka 2024, zilizochapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 20 la Januari 12, 2024.
Mpango huu unalenga kuimarisha usimamizi wa sekta ya usafiri wa nchi kavu, kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato na kuboresha ubora wa huduma kwa abiria.
Pazzy ameongeza waendeshaji watatumia mifumo yao binafsi endapo itakidhi matakwa ya kisheria au kushirikiana na watoa huduma waliothibitishwa na Latra.
Aidha, amebainisha Latra kwa kushirikiana na Kitengo cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi, wataendelea kufanya ukaguzi nchi nzima kuhakikisha masharti ya leseni, usalama, uwekaji wa alama kwenye mizigo na matumizi ya tiketi mtandaoni kama inavyotakiwa kisheria intekelezwa.
Hadi sasa baadhi ya watoa huduma waliosajiliwa ni Kampuni ya Logix, Kampuni ni Itule, Kampuni ya Busbora, Duarani Innovate Ltd, Web Corporation Tanzania Ltd, Hashtech Tanzania Ltd, Kampuni ya Otapp Agency Ltd, Sepa Tech Ltd,
Kampuni nyingine ni Iyishe Ltd (Adventure Connection), Global, Mkombozi Infotech , Meerkatz (Kidia One), Abood Bus Services, Borita Company Ltd, na Exabytes Africa Ltd.