Polisi yaweka kambi eneo la ajali iliyoua 28, Sh 3.4 bilioni kutolewa kwa wananchi

Kamati ya ulinzi na usalama mkoani Mbeya ikikagua eneo la njia ya mchepuko eneo la Iwambi inayoendelea ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika kukabiliana na ajali katika mlima Iwambi mkoani humo.
Muktasari:
- Jumla ya Sh 3.4 bilioni zimetengwa kwa ajili ya fidia kwa wananchi waliopo Mlima Iwambi watakaopisha ujenzi wa njia hiyo, huku Polisi wakiweka kambi saa 24 na kufanya doria kwa vyombo vya moto.
Mbeya. Siku chache baada ya ajali iliyoua 28 na kujeruhi wengine tisa, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limesema litaweka kambi ya saa 24 na kuweka kizuizi katika mlima Iwambi ili kukabiliana na ajali za mara kwa mara eneo hilo, huku Serikali ikianza kulipa fidia kwa wananchi kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Juni 7 saa 1 usiku, watu 27 walifariki papo hapo na mwingine mmoja kufariki wakati akipatiwa matibabu kufuatia ajali iliyohusisha magari matatu, ikiwa ni mwendelezo wa matukio ya ajali katika eneo hilo.
Baada ya ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera alielekeza Wakala wa Barabara mkoani humo (Tanroad) kuharakisha ujenzi wa njia ya mchepuko ambayo itatumika kwa magari madogo.
Akizungumza leo Juni 13, 2025 wakati wa ziara ya kamati ya ulinzi na usalama katika eneo hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Benjamin Kuzaga amesema tayari wameanza utekelezaji wa maelekezo ya serikali kwa kuweka kambi ya saa 24 katika mlima humo.

Amesema kambi hiyo inaenda sambamba na doria kwa vyombo vya moto ikiwa ni pikipiki, guta na kutoa msaada wa haraka inapotokea changamoto yoyote barabarani.
“Tutakuwa tunawasiliana ili inapotokea changamoto yoyote msaada unakuwapo, tutaweka mabomba ‘barriers’ katika eneo hili na tutafanya kazi saa 24 na doria kwa vyombo vya moto ikiwa ni pikipiki na guta” amesema Kuzaga.
Kwa upande wake ofisa mfawidhi mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini (Latra) mkoani humo, Mhandisi Shaban Mdende, amesema wameanza kufuatilia utekelezaji kujiridhisha na usalama katika barabara hiyo.

“Kutakuwa na pikipiki zitakazokuwa zinapishana, tumeridhishwa na hatua zilizochukuliwa na tutaendelea kufuatilia na kushauri kuhakikisha watumiaji wa barabara wanakuwa salama, hatutarajii kuona matukio haya yakiendelea iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake” amesema Mdende.
Meneja wa Wakala wa barabara mkoani Mbeya, (Tanroad), Mhandisi Masige Matari amesema hadi sasa kazi inaendelea ya kupanua njia ya mchepuko na kwmaba kuanzia kesho Jumamosi wataanza kumwaga moramu tayari kwa kuanza kutumika.
“Tayari serikali serikali imeshatoa fidia ya Sh 3.4 bilioni kwa wananchi kwa ajili ya kuanza kujenga mlima Iwambi na magari yakipita kushoto na kulia na kuondoa ile ya kupita sehemu moja na huenda ajali hizi zikabaki historia” amesema Matari.
Ameongeza kuwa hadi sasa mkandarasi yupo kazini, ambapo zoezi la kufunga taa kwa ajili ya kusaidia askari polisi kuendelea na doria unaendelea, akibainisha kuwa baada ya shughuli kuisha matukio ya ajali yataisha.

Naye mjumbe wa kamati hiyo, Mhandisi Rajabu Ghuliku amesema wameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali, akitoa matumaini kuwa kukamilika kwa ujenzi wa njia hiyo, utamaliza ajali mkoani humo.
“Tumefuatilia utekelezaji kuanzia eneo la Inyala kuhakikisha tunaondokana na ajali hizi, kamati imechukua hatua kila mmoja atimize wajibu wake, tumeridhishwa na ufungaji taa hizo zitachukua siku tatu nah ii itaenda kuwa suluhisho la ajali Mbeya” amesema Ghuliku.