Prime
Simulizi jinamizi la ajali kwa maeneo haya Mbeya

Muktasari:
- Kwa muda mrefu Mbeya imekuwa ikikithiri kwa ajali za mara kwa mara, kwa miaka mitano, zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.
Mbeya. Wakati zikiripotiwa ajali zinazoua makumi ya watu katika Mlima Iwambi jijini Mbeya, wakazi wa Mtaa wa Ndejele uliopo eneo hilo, wamesimulia namna walivyochoka kuokota maiti za ajali mara kwa mara, huku wakiitaka Serikali kuchukua hatua.
Wamesema eneo hilo limekuwa hatari kwa ajali za mara kwa mara zinazohusisha pikipiki, bajaji, hiace na magari ya abiria na kusababisha vifo na majeruhi.
Kauli hiyo imekuja siku tatu, wakati simanzi na vilio bado vimetawala kwa familia zilizopoteza ndugu na wapendwa wao katika ajali iliyoua watu 28 na kujeruhi wanane katika mlima huo, usiku wa Juni 7, 2025.

Kwa muda mrefu Mbeya imekuwa ikikithiri kwa ajali za mara kwa mara, kwa miaka mitano, zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikiripotiwa.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni kuweka foleni kwa ajili ya kupishana magari makubwa ‘lori’ na magari ya abiria kwa dakika 30 kwenye mteremko wa Iwambi na kuweka usalama wa askari katika njia hiyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Juni 11, 2025 Mwenyekiti wa Mtaa wa Ndejele eneo la Iwambi, Aida Kaminyoge amesema wamechoshwa kubeba maiti katika mteremko huo, akieleza namna bora ya kuondoa mzimu wa ajali hizo ni kumaliza ujenzi wa barabara ya mchepuko.

Amesema pamoja na ajali kubwa ikiwamo ya Juni 7, 2025 iliyoua watu 28, ajali nyingine hutokea zikihusisha bodaboda, hiace na magari mengine madogo hasa wakati wa usiku ambao askari wanakuwa hawapo.
“Hakuna namna nyingine zaidi ya kujenga njia ile ya vumbi itumike rasmi, si lazima magari yote yapite kwenye ule mteremko, ajali nyingine haziripotiwi kwakuwa idadi inakuwa ndogo ila kwa jumla ni maumivu sana kila siku kuona maiti barabarani.
“Ajali nyingi zinatokea usiku kwa sababu muda huo askari wanakuwa wameshaondoka, kinachofanyika utaratibu huvurugwa, magari makubwa, madogo, pikipiki vyote huondoka kwa pamoja, usalama huwa ni mdogo,” amesema Aida.

Naye Hilda Simon, mkazi wa Iwambi amesema eneo hilo bado changamoto ni nyingi, mbali na ufinyu wa barabara, kingo na alama za barabarani ni muhimu sana.
“Njia ni ndogo, kuna siku magari matatu yaligongana yakakosa uelekeo yakatumbukia korongoni, sasa tunachoka kuona wenzetu wanapukutika, Serikali iharakishe ujenzi wa njia nne,” amesema Hilda.
Huruma Mwambo, mkazi wa Inyala, amesema pamoja na Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) kuweka alama za barabarani, lakini miundombinu ya njia hiyo si rafiki na zaidi ni ufinyu wake akieleza kuwa hatima ya yote ni njia nne.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kajigili eneo la Simike, Meshack Bwambi amesema kero ya ajali za mara kwa mara katika eneo hilo inawapa wakati mgumu uongozi wa mtaa na wananchi kwa jumla.
Amesema baada ya ajali za mara kwa mara eneo hilo, walikutana watendaji wa Serikali kujadiliana na wananchi waliopo mita 30 waweze kuondoka ili kulinda usalama wao.
“Ilikuwa kikao cha mwaka jana, kuna viongozi wa Serikali walitoka Makao Makuu Dodoma, Tanroads wakafanya mkutano tukawaelimisha wananchi, wakafanya tathmini kwa ajili ya kutuhamisha kupisha ujenzi wa barabara ya njia nne.
“Makubaliano yalikuwa ndani ya kipindi cha miezi sita, lakini baadaye tulipokea taarifa kuwa hakuna pesa hivyo tuvute subira, hadi sasa wananchi walio eneo hilo roho ziko juu kwa kuwa wapo chini na barabara iko juu,” amesema Bwambi.
Mwenyekiti huyo anaongeza wanachoshauri Serikali ni kupanua barabara hiyo ili wananchi waliopo mita 30 kutokana njia kuu wapishe badala ya kubaki kwenye mita 22.5.
Gasper Mwankemwa, mkazi wa Simike amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba Serikali kupanua barabara akieleza kuwa, hatua iliyofikiwa sasa si mbaya kwa kuwa matarajio yao ni kuondokana na kupoteza wapendwa wao.
“Tumeona juhudi na hatua zilizofikiwa, tangu ile ajali iliyoua watu wengi hapa Tanroads walianza ujenzi wa ile njia nne, tunayo matarajio ujenzi huo utaisha kwa wakati na kuondokana na vilio vya mara kwa mara” amesema Mwankemwa.
Kauli ya Serikali
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera amesema kufuatia ajali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan anaelekeza Tanroads mkoani humo kutengeneza barabara ya vumbi.
Amesema maelekezo mengine ni kulipa fidia kwa wananchi wa eneo la Mbalizi zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya kupanua barabara hiyo na kutoa Sh500,000 kwa kila familia.
“Lakini si kwamba kutoa salamu hizo za pole zinaweza kukidhi uhai wa mwanadamu, bali ni vile kuguswa na hili lililojitokeza kwa jinsi alivyoguswa Rais Samia (Suluhu Hassan) na tutakuwa na kituo kikubwa cha ukaguzi wa magari makubwa yaendayo nje ya nchi.

“Kwa maana hiyo, magari yote yaendayo umbali mrefu yatakuwa na upande wake na madogo yawe na sehemu yake, hili nalitaka lifanyike ndani ya siku tatu kuanzia leo (juzi) ili kunusuru maisha ya wenzetu,” amesema Dk Homera.
Tanroads kazini
Meneja wa Tanroads, Masige Matari amesema baada ya maelekezo ya Serikali, tayari wameanza ujenzi wa barabara ya mchepuo iliyopo Iwambi kutokea Mbalizi.
Amesema ujenzi wa njia hiyo yenye urefu wa Kilomita 7.3 wameazimia kukamilika ndani ya siku saba kutoka Juni 9, walipoanza ujenzi wake na kwamba wanaamini watakamilisha kwa wakati.
“Tumekuwa na maamuzi ya wakati, kwa kuwa hata ile njia nne eneo la Simike baada ya ajali tulianza utekelezaji sawa na maelekezo yaliyotolewa juzi kwa njia ya mchepuko pale Iwambi.
“Njia hiyo ya kilomita 7.3 tunatarajia ndani ya siku saba tutakuwa tumemaliza, hivyo tuwaombe wananchi na watumiaji wa barabara kuwa na subira kwa kipindi hiki tukikamilisha kazi,” amesema Matari.
Pamoja na matukio hayo ya ajali kukithiri, lakini yapo maeneo korofi zaidi ambayo mara nyingi hutokea ajali na kusababisha aida vifo au majeruhi.
Iwambi
Iwambi ni eneo ambalo limekuwa maarufu kwa kuchukua uhai wa watu, ikiripotiwa kuwa sehemu hatarishi zaidi kwa ajali na idadi kubwa ya vifo na majeruhi.
Kwa miaka mitano, tangu mwaka 2018 takribani watu 70 wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa katika eneo hilo licha ya hatua zilizochukuliwa na serikali.
Julai 2, 2018 watu 20 walifariki dunia, huku wengine 40 wakijeruhiwa kwa ajali iliyohusisha zaidi ya magari matatu, ikiwa ni lori ambalo lilikuwa na mzigo kuligonga gari la abiria na kusababisha mengine mawili kupoteza muelekeo.
Juni 23, 2024 watu tisa walifariki na wengine 23 kujeruhiwa, ajali iliyohusisha magari matatu, ambapo lori lililigonga ubavuni gari la abiria na kugusa lingine na kisha kutumbukia korongoni.
Juzi Juni 7 mwaka huu, watu 28 walifariki dunia na wengine 10 kujeruhiwa baada ya lori kufeli breki na kugonga magari mawili yaliyokuwa na abiria na kusababisha vifo na majeruhi hao.
Licha ya namba hizo kufikia 71 eneo hilo kumekuwa na ajali nyingi zinazochukua uhai wa mtu mmoja au wawili mara nyingi zaidi ikilinganishwa na eneo jingine.
Shamwengo
Agosti 16, 2023 eneo la Shamwengo watu 19 walifariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa baada ya gari kampuni ya Evarest Fretch Ltd kuligonga basi la Super Rojas na kusababisha vifo na majeruhi hao.
Ajali nyingine iliyotikisa ilikuwa Februari 27 mwaka huu ikihusisha msafara wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Rajabu ambako watu sita walifariki dunia wakiwamo waandishi wa habari na aliyekuwa Katibu wa CWT Mkoa wa Mbeya.
Pia, eneo hilo linalopakana na Mlimanyoka katika Kata ya Inyala, kunatajwa kuwa sehemu yenye hatari zaidi kutokana na jiografia yake kwa kuwa na kwa kona nyingi na kubwa.
Hata hivyo, katika maeneo hayo baadhi yake hayana alama barabarani, kingo na usalama mdogo licha askari wa kikosi cha usalama barabarani kuweka kambi wakiongoza magari.
Simike
Eneo hili lenye mteremko mkali kuelekea mkoani Songwe na nchi jirani ya Zambia, panatajwa kuwa sehemu korofi kutokana na historia yake ya kutokea ajali za mara kwa mara, pale magari yanapofeli breki.
Moja ya ajali kubwa ambayo iliacha simanzi na taharuki ni Juni 5, 2024 watu 16 walifariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa kufuatia lori kufeli breki na kuparamia basi la abiria aina ya Coster iliyokuwa ikitokea mkoani Songwe.

Pia, inaelezwa zipo ajali ndogo ndogo za kujeruhi na kuua zikiwamo za bodaboda na mabasi ya abiria, zikizua hofu kwa wakazi walio karibu na barabara hiyo.
Ajali nyinginezo zilizowahi kutokea na kuacha simanzi ilikuwa Septemba 27, watu 12 walifariki dunia na wengine 23 kujeruhiwa baada ya gari aina ya fuso kufeli breki wakati wafanyabiashara wakielekea mnadani huko Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Pia, ipo ajali iliyotokea Juni 6, 2024 basi la Kampuni ya AN Classic liliua watu 11 na wengine 44 kujeruhiwa eneo la Lwanjiro Wilaya ya Mbeya Vijijini ikielekea mkoani Tabora.