Prime
Kupotea kwa Mdude bado kitendawili, mkewe aiangukia Serikali

Muktasari:
- Siku moja baada ya tukio la kuvamiwa na kutoweka kwa mwanaharakati wa Chadema, Mdude Nyagali, mke wake ameomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhakikisha mumewe anapatikana, huku Polisi Mbeya wakisema uchunguzi unaendelea.
Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limesema linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu kutekwa na kupotea kwa mwanaharakati na kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagali, huku mkewe akiomba Serikali kuingilia kati kumtafuta mumewe.
Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia Mei 2, 2025, saa 8:00 usiku, nyumbani kwao eneo la Iwambi jijini Mbeya, ambapo watu wasiojulikana walivamia nyumba, kisha kuvunja mlango na kumchukua kwa nguvu, kabla ya kutoweka naye.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Mei 3, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema uchunguzi unaendelea, akibainisha kuwa kikosi cha kazi maalumu, kikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), kinafanyia kazi tukio hilo.
“Tunaendelea na uchunguzi, naomba wananchi watulie na washirikiane na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kupatikana kwa Mdude Nyagali na kuwabaini waliomteka,” amesema Kamanda Kuzaga.
Awali, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilidai kuwa waliomchukua Nyagali walijitambulisha kuwa ni askari polisi, madai ambayo Kamanda Kuzaga alikanusha Mei 2, 2025.
KIlio cha mke wa Mdude
Mke wa Nyagali, Sije Mbugi (31), amesema anaishi kwa hofu kubwa tangu mumewe alipotoweka, hivyo anaiomba Serikali na vyombo vya usalama kuhakikisha anapatikana akiwa salama.
“Naomba wanisaidie, mume wangu apatikane akiwa hai au hata kama amekosea, basi angefikishwa kwenye vyombo vya sheria, si kuchukuliwa kimyakimya. Hili linaumiza sana,” amesema Mbugi.
Kwa upande wa chama chake, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale, amesema hadi sasa chama hicho hakijapata taarifa rasmi kuhusu alipo kada wao na kwamba viongozi wamekutana kujadili hatima ya tukio hilo.
“Tunaendelea kumtafuta katika maeneo mbalimbali bila mafanikio. Jeshi la Polisi linapaswa kutoa kauli rasmi juu ya alipo na hatua zinazoendelea kuchukuliwa,” amesema Mbeyale.
Ameongeza kuwa tukio hilo limeleta hofu miongoni mwa wanachama wa Chadema na kuibua maswali mengi hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“Watu wana hofu. Hatuishi kwa amani. Tunalitaka Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla kuharakisha uchunguzi na kuwakamata waliohusika,” amesema.